Thursday, September 20, 2012
AMRI HALALI INAYOTUMIWA NA JESHI LA POLISI KUSABABISHA MAAFA KWA RAIA, INAMAANA GANI? TUTAFAKARI KATIKA MAKALA HAYA
MOJAWAPO ya majibu ambayo yamekuwa yakitolewa katika kuhalalisha matumizi ya nguvu dhidi ya raia, ni kuwa ‘raia wanapaswa kutii amri halali’.
Jibu hili wakati mwingine hutolewa likisisitiza kuwa serikali au vyombo vya dola vinapotoa amri, basi wale wanaoamrishwa wanatakiwa kutii tu “bila shurti”.
Kwamba wakati mwingine polisi inawapasa watumie nguvu dhidi ya raia kwa sababu raia wamekataa kutii amri halali.
Jibu hili limekuwa likitolewa hasa na wale ambao ni wapinzani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na watetezi wa serikali hii.
Wanasema kuwa CHADEMA ni chama cha vurugu na kuwa matukio mbalimbali ya mauaji na watu kuumizwa ambako kumefanywa na vyombo vya dola kwa kweli ni makosa ya CHADEMA kwa sababu “kama wangesikiliza na kutii amri wanazopewa na serikali matatizo hayo yasingewakuta.” Kuna hisia kwamba askari au mtumishi wa serikali akiamuru kitu basi raia hapaswi kuhoji bali anapaswa kutii kwa vile amri lililotolewa ‘kihalali.’
Uhalali wa amri unatoka wapi?
Kabla sijaangalia kama mtu anapaswa kutii amri anayopewa na ofisa wa serikali naomba nioneshe kwanza kitu kimoja muhimu sana. Amri haiwi halali kwa sababu imetolewa na mtu halali tu. Narudia tena hiyo kauli: Amri haiwi halali kwa sababu imetolewa na mtu halali.
Uhalali wa amri unatakiwa ukidhi vigezo kadha wa kadha hicho cha kutolewa na mtu au chombo halali ni moja tu na peke yake hakitoshi kumlazimisha mtu kutii.
Ile amri iwe halali, basi pamoja na kutolewa na mtu halali ni lazima itolewe kihalali.
Mfano mzuri ni mtu ambaye ana kesi yake katika mahakama na baada ya upande wa mashtaka kumaliza mashtaka yake basi Jaji anaamua kutoa hukumu. Jaji ni mtu halali wa kutoa hukumu mahakamani lakini bila kutoa nafasi kwa utetezi basi mazingira ya kutolewa “kihalali” yanakosekana.
Jaji hawezi baada ya kusikiliza upande wa mashtaka tu akaamua kumhukumu mtuhumiwa kifungo jela au kumwachilia. Katika taratibu za kawaida za kimahakama yule mtuhumiwa anatakiwa apewe haki yake ya kujitetea na kuonesha ushahidi au kuita mashahidi wote ambao wanaweza kumsadia asionekane mwenye hatia.
Pamoja na kufanya hivyo, bado kuna taratibu za mahakama za kupima uzito wa ushahidi (law of evidence) ambapo baada ya kusikiliza pande zote mbili na kuangalia ushahidi unaotolewa na pande zote mbili Jaji hatimaye anaamua kutoa hukumu kwa masuala yale tu ambayo yanahusiana na kesi au zaidi yale ambayo yanabishaniwa.
Lakini, licha ya kutolewa katika mazingira halali msingi mkubwa wa amri yoyote inayotolewa ni lazima itolewe ikiwa inaendana na ukweli. Amri ambayo inatolewa kwa uongo inaweza isisimame baadaye hasa ukweli ukijulikana.
Hii ndio sababu amri yoyote halali ikiwa inazingatia vigezo vingine vyote inatolewa bona fide (in good faith), yaani kwa kuamini kuwa anayeitoea anaitoa akiwa anaamini ni kweli. Kwa mfano, kama baadhi ya vitu ambavyo viliongoza amri kutolewa vinapokuja kugundulika kuwa havikuwa vya kweli, basi aliyetoa hukumu hawezi kulaumiwa kwa sababu yeye alipotoa hukumu au agizo aliamini kuwa anafanya kwa haki na kwa usawa kabisa.
Ni kutokana na hilo basi, yeyote anayetoa hukumu au amri yoyote ambayo anataka itekelezwe ni lazima yeye mwenyewe ajiridhishe kuwa yuko sahihi. Mfano mzuri ni wa mauaji ya Daudi Mwangosi.
Kwa wale ambao walipata nafasi ya kuangalia mchakato mzima wa matukio hadi mwisho wake wataona kuwa sababu ya polisi kuingilia mkutano wa CHADEMA pale Nyololo ilikuwa ni kutokana na kuamini kuwa mkutano ule ulikuwa siyo wa “ndani” (internal meeting).
Waandishi walijitahidi sana na kwa kweli wanastahili pongezi kumhoji kamanda Kamuhanda maana hasa ya “internal meeting”. Kamuhanda ambaye alinukuliwa kuwa ndiye alikuwa anatafsiri sheria zote pale alifanya kosa kubwa sana la kutopata ushauri kutoka kwa wenzake ili kujua kama maana ya “internal meeting” ni sawa na “inside meeting”.
Kwamba je, mkutano wa “ndani” unaweza kufanyika “nje” au kuwa na watu wengine “nje”. Kwa vile alikosa hekima ya kutafuta ushauri alijikuta anatoa amri ambayo kama nitakavyoonesha hapa chini haiikupaswa kutiiwa na yeyote kwa sababu ilikuwa imetolewa kwa makosa.
Dhamiri ya mwanadamu iko juu ya amri
Kitu ambacho ningependa kukiandika kwa kina kidogo ni kile ambacho naweza kukiita ni “ukuu wa dhamira ya mwanadamu”, yaani the supremacy of human conscious. Kati ya vifaa vyote ambavyo Mwenyezi Mungu ametujalia wanadamu hakuna kilicho cha juu zaidi na ambacho kinatafsiri uanadamu wetu kama dhamiri. Yaani, ile sehemu ya utu wa mwanadamu ambayo inamuamuria wema na uovu, na ambayo inamsukuma kukubali au kukataa.
Dhamiri ya mwanadamu ndio dira pekee ya maisha yake na kama dira hii imetengezwa vizuri (well formed), basi humuongoza katika maisha salama licha ya mikwaruzo ya hapa na pale.
Dhamiri hufunzwa tangu utotoni kwa mtoto kufundishwa mema na mabaya na kwa kadiri anavyozidi kukua hufundishwa kwa vitendo vya wema na kuepushwa kwa vitendo viovu.
Lakini, dhamiri isipoongozwa vyema toka utoto na katika maisha basi mwanadamu huenda akisukumwa kama mnyama akiongozwa na hisia na matukio. Lakini dhamiri hii ikiwa imefundishwa vizuri na kujizoeasha katika kufuata mema basi inajikuta ikitambua uovu na kuukataa. Sasa dhamiri ambayo imefundishwa vizuri kufuata mema haiwezi kulazimishwa kukubali uovu kwa gharama yoyote. Huu ndio ukuu wa dhamira.
Watu wameenda katika vifo vyao na wengine katika vifungo vyao vya muda mrefu kwa sababu hawakuwa tayari kusaliti dhamiri zao.
Nimewahi kuandika huko nyuma kuwa unaweza kuwafunga watu gerezani au unaweza kuwatendea watu vibaya ukiamini kuwa kwa kufanya hivyo utawanyamazisha lakini ukweli ni kuwa utawanyamazisha tu kama utaua dhamiri zao.
Lakini kama watu hao wanaamini katika ukweli wa dhamiri zao basi hakuna mateso, hakuna jela, hakuna vitendo ambavyo vinaweza kuwafanya wakubali uongo kuwa ukweli, uovu kuwa ni wema na uadui kuwa ni urafiki.
Sasa dhamiri ya mwanadamu imeumbwa kutii ukweli, wema na uzuri. Na iko tayari kukataa kutii amri isiyo halali au ambayo inamfanya asiwe kama mwanadamu.
Historia ina mifano mingi ya watu ambao walikataa kukubali uovu ili waoneakena vizuri. Kuanzia kwenye maandiko na katika historia wapo watu walioishi na kukataa kuishi pale ambapo dhamiri zao ziliwakataliwa.
Mifano ya marafiki wa Nabii Daniel (Meshak, Shedrack na Abednego) iko wazi. Wangeweza kuiabudia sanamu ya mfalme Nebukadneza na wangeishi kwa raha mustarehe. Lakini dhamiri zao ziliwakataliwa.
Kina Nelson Mandela na wenzake walikuwa na uwezo wa kukubali makosa madogo na kuomba radhi na kuahidi kuwa hawatafanya tena siasa ili kuepuka kifungo cha maisha. Lakini wote wakitii dhamiri zao (huku wakilipia gharama kubwa kwa familia zao) walikataa uongo na wakawa tayari kwenda jela. Miaka 27!
Katika taifa letu bado hatujapata watu ambao wako tayari kutii dhamiri zao kuliko kutii uongo. Tunachokiona sasa hivi wapo watu ambao wameanza kuamka na kudai kutii dhamiri zao kutokana na ukweli uliopo.
Kwa mfano CHADEMA wanapoamua kufanya mikutano ya ndani ambayo wanaamini wako sahihi hakuna amri yoyote ambayo inaweza kuwalazimisha kuacha kufanya hivyo hasa kama amri hiyo inatolewa ikiwa na mushkeli.
Kifo cha Mwangosi, binafsi ninakiona pia ni ushahidi wa ukuu wa dhamiri ya wanadamu. Mwangosi hakuwa na sababu ya kwenda kuwahoji polisi kwanini wanamshikilia mwandishi wa Nipashe. Angeweza kukaa pembeni na kusubiri wamalizane ili baadaye aulize.
Lakini dhamiri yake ilimkatalia. Ilimkatalia kwa sababu aliamini kuwa polisi hawapaswi kukamata waandishi wa habari na hawapaswi kutumia nguvu mahali ambapo hakuna tishio lolote la amani.
Kwangu mimi kinyume na wale ambao wanaona mwandishi wa habari aliuawa – ni kuwa uhuru wa dhamiri ya mwanadamu ulikataliwa na watawala.
Badala ya kumpa nafasi ya kumsikiliza walianza kumpiga na badala ya kumtuliza kwa kumwelewesha alilipuliwa. Alikuwa anasumbua watawala kwa maswali yake. Alitakiwa kutii tu bila ‘shurti’!
Hatupaswi kutii amri ambazo zina hatari kwetu au ni kinyume yetu
Hili ni kweli sana, tena sana. Mtu kwa vile ni polisi anavaa nyota nyota na anakuja na kimulimuli, hawezi kuja nyumbani kwako na kukuambia usilale na mwenza wako na wewe ukiwa na akili timamu ukaitikia “ndio afande!”
Rais Kikwete pamoja na vyeo vyote alivyonavyo hawezi akaamka asubuhi na kusema simpendi sana Dk. Slaa mkamateni na mumfunge maisha! HAWEZI!
Jaji Mkuu hawezi kuamua tu kuwa kwa vile Tundu Lissu amedai wapo majaji vilaza, basi ahukumiwe kwenda jela! Hawawezi kwa sababu hata wakijaribu dhamiri za wanadamu zinapaswa kuwakatalia!
Amri uliyo na shaka nayo ihoji
Ninachosema ni kuwa usikubali kutii amri ambayo una shaka nayo. Kwa mfano, polisi wa usalama barabarani akikusimamisha kwenye gari lako na kukuambia kuwa uteremke na urudi nyumbani ukitembea kwa vile gari lako amelichukua kwa jina la serikali, ni lazima uhoji. Utakuwa mtu mvivu wa kufikiri kama utaamua kuteremka na kukusanya vitu vyako na kumpatia ufunguo.
Hili ni kweli kwa wanasiasa wetu na hasa watu wa CHADEMA. Viongozi wa serikali wakitoa amri ambazo wanaziona zina matatizo kwao na hazina haki ni wajibu wao kukataa kuzitii. Lakini, wasikatae kwa sababu hawazipendi. Kama amri imetolewa kihalali na katika mazingira halali basi ni wajibu wa wale wanaopewa amri hiyo kuitii.
Lakini kutii amri halali yenye mazingira halali nako kunakikomo chake hasa kama mfululizo wa amri hizo unalenga kunyima haki za watu.
Kwa mfano, kama kila wakati CHADEMA wanaomba kibali kufanya mkutano wanaambbiwa “intelligentsia inaonesha kutakuwa na vurugu” au wanakataliwa wakati watu wengine wanapewa basi ni jukumu la CHADEMA kukataa kutii amri hiyo.
Huo ndio ukuu wa dhamiri ya mwanadamu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment