Friday, September 14, 2012
HOFU YA KUTAKA KUMUUA MUFTI SIMBA YATANDA
• Waziri amng’oa kigogo NECTA kumlinda Ndalichako
na Waandishi wetu
WAKATI baadhi ya Waislam wakipanga kuandamana kuvamia ofisi ya Mufti wa Tanzania, Sheikh Issa Bin Shaaban Simba, hofu ya kutaka kuuawa kwa kiongozi huyo wa dini imetanda nchini.
Kutokana na tishi hilo, Jeshi la Polisi limetoa onyo kali kwa kundi lolote la Kiislamu lililopanga njama za kuvamia ofisi ya Mufti leo kwa lengo la kumdhuru na kumuondoa madarakani.
Habari zinasema kuwa kundi hilo limepanga kufanya maandamano bila kibali na kuibukia katika ofisi za Bakwata kwa lengo la kumng’oa Mufti Simba.
Akizungumzia tishio hilo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema kuwa polisi wamechukua hatua mbalimbali kukabiliana na kundi linalotaka kuvamia ofisi za (BAKWATA) na Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA) na tayari washukiwa wawili kati ya kumi wamekamatwa kwa mahojiano.
Kamanda Kova alisema hatua hiyo imefikiwa baada ya kupokea malalamiko kutoka Bakwata na kufungua jalada la kesi dhidi ya kundi lenye lengo la kutumia nguvu na mabavu hali inayoashiria uvunjifu wa amani.
Kova alisema kuwa ni jukumu la serikali kupitia vyombo vya dola kuhakikisha uwepo wa usalama wa taasisi yoyote iliyosajiliwa kisheria.
“Ni wajibu wetu kuwalinda viongozi walioko madarakani mpaka pale taratibu za kiutawala na Kikatiba zitakapowaondoa madarakani,” alisema Kova.
Pia Kova aliwasihi wananchi na wafuasi wa makundi hayo kutofuata mkumbo katika kutekeleza azma hiyo na kueleza kuwa jeshi hilo haliwalindi Bakwata pekee, bali viongozi wote na yeyote anayetaka kumuondoa kiongozi madarakani aende mahakamani au afuate taratibu na kanuni za taasisi husika.
Hivi karibuni Mufti alinukuliwa na gazeti moja la kila siku akieleza kuwapo kwa kundi la wanaojiita Waislamu lenye lengo la kumuondoa madarakani na kusema kuwa yeye yupo kisheria na kwamba kundi hilo haliwezi kumuondoa kwani Waislamu si wa Dar es Salaam pekee.
Katika hatua nyingine, serikali imelazimika kumfukuza kazi Mkuu wa Idara ya Utafiti, Tathmini na Huduma za Kompyuta wa Baraza la Mtihani, Joseph Mbowe, kwa madai ya uzembe uliosababisha kurudiwa kwa mtihani wa Maarifa ya Kiislam.
Hatua hiyo imekuja takriban wiki moja imepita tangu maandamano ya Waislamu kwenda Wizara ya Mambo ya Ndani kufanikisha kuachiwa huru kwa wenzao waliokamatwa kwa sababu ya kususia sensa ambapo pamoja na mambo mengine, wiki hii walitishia kufanya maandamano kwenda kumng’oa Ndalichako na Mufti Simba.
Akitangaza kusimamishwa kazi kwa Mbowe, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo, alisema jana kuwa hatua hiyo imetokana na mapendekezo ya kamati ya wataalamu mbalimbali waliochunguza chanzo cha malalamiko ya kufeli kwa wanafunzi wa Kiislam waliofanya mtihani huo mwaka jana.
Kwa mujibu wa Mulugo, kamati hiyo ilibaini pasi na shaka kwamba tatizo la usahihishaji wa mtihani huo lilitokana na kasoro za kiutendaji na kiufundi na si vinginevyo, hivyo kupendekeza kuwajibishwa kwa mkuu wa kitengo cha kompyuta.
Alisema kamati hiyo ilihusisha wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar (kwa kuwa Necta ni taasisi ya Muungano) na Islamic Education Panel.
Wataalamu wengine walitoka Baraza la Wakuu wa Shule za Kiislam, Idara ya Usalama wa Taifa na Ofisi ya Waziri Mkuu (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa).
“Kamati ilipewa hadidu nane za rejea ikiwemo kupitia orodha ya wasahihishaji wa somo la Maarifa ya Kiislam kubainisi sifa zao, kupitia maoni yao na sampuli za karatasi za majibu ya watahiniwa ili kujiridhisha na usahihishaji wake.
“Kamati hiyo iliyoteuliwa na Waziri wa Elimu iliwataka wajumbe hao kulinganisha mchakato wa usahihishaji wa mwaka 2012 na miaka iliyopita, kuwahoji baadhi ya watendaji wa Necta waliohusika na ukokotoaji wa mtihani huo na kupendekeza nini kifanyike,” alisema naibu waziri huyo.
Alisema kamati iligundua kwamba tatizo la usahihishaji wa mtihani kwa kutumia kompyuta ulihusisha karatasi tatu za majibu badala ya mbili, hivyo kusababisha watahiniwa wote kupata alama za chini.
Mulugo alisema kamati iliona kwamba mfumo wa usahihishaji kwa kutumia kompyuta haukufanyiwa majaribio ili kujiridhisha huku ikiridhishwa na utendaji bora wa Necta hasa kwa kuandaa na kusahihisha mitihani.
Awali aliwaomba radhi watahiniwa wote kwa usumbufu uliojitokeza huku akiahidi kutorudiwa tena kwa kasoro hizo na kusisitiza kwamba licha ya kusimamishwa kazi, Mbowe atachukuliwa hatua zaidi za kiutendaji.
Kabla ya kuchukuliwa kwa hatua hizo, wizara ilipokea malalamiko kutoka kwa wakuu wa shule za Kiislam, hivyo aliwaomba wote kukubaliana na hatua zilizochukuliwa.
Chanzo Tanzania Daima
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment