Afisa Kazi Ruvuma Oddo Hekela
Na Stephano Mango,Songea
WANANCHI wametakiwa kuwapima Wabunge na Madiwani wao ili kuweza kubaini ubora wao katika ushirikishaji wa wananchi katika eneo lake la uongozi katika kuleta maendeleo ya nchi kwa kutumia dhana shirikishi
Wito huo umetolewa jana na Afisa Kazi Ruvuma Oddo Hekela kwenye mdahalo wa wazi wenye lengo la kupata taswira ya uwajibikaji wa viongozi kwa wananchi wao ulioitishwa na Mtandao wa Asasi za Kiraia Wilaya ya Songea(Sonngo)kwa ufadhiri wa Shirika la The Foundation For Civil Society
Hekela alisema kuwa Mbunge na Diwani wote ni wawakilishi katika eneo lao la kazi ambao wamebeba jukumu la kuhamasisha wananchi katika kutekeleza majukumu ya maendeleo hivyo ushirikishwaji bora ndio maendeleo bora
Alisema kuwa ili kupima ubora wa Mbunge na Diwani lazima upime uwezo wa ushirikishwaji wa wananchi katika eneo lake ili kuweza kuleta maendeleo ya nchi kwani wote ni wawakilishi wa wananchi katika Serikali ya watu hivyo wajibu wao unafanana
Alieleza kuwa miongoni mwa majukumu ya Mbunge akiwa jimboni ni kukaa ofisini na kuhudumia wananchi kwa kusikiliza hoja zao ili aweze kuzitatua au kuzipeleka sehemu husika kwa hatua zaidi,kufanya ziara kwa wananchi ili kuweza kujua mikakati ya maendeleo,kufuatilia utekelezaji wa miradi ya kitaifa jimboni kwake inayotekelezwa na Serikali kuu kusikiliza maoni ya wananchi kuhusiana na utekelezaji wa miradi hiyo
Alieleza zaidi kuwa majukumu yake mingine akiwa jimboni ni pamoja na kusimamia utekelezaji wa sera mbalimbali kwa kutoa tafsiri ya sera zenyewe ili wananchi wazielewe,kutoa elimu na kuwahamasisha wananchi ushiriki wao katika miradi ya maendeleo
Kwa upande wake Katibu wa Mtandao wa Sonngo Mathew Ngarimanayo alisema kuwa Viongozi wanapaswa kutimiza wajibu wao kikamilifu katika kuhakikisha Sera mbalimbali zinawanufaisha wananchi ili kuweza kupunguza umaskini wa kipato unaowakabili na kuweza kuchangia pato la Taifa
Ngarimanayo alieleza kuwa ni jambo la aibu kuona Mbunge anazunguka mjini huku wapiga kura wake wanahangaika kutokana na sera mbalimbali kutokuwa wazi na wakati mwingine kushindwa kumnufaisha mwananchi kutokana na kuwa katika mazingira magumu ya upatikanaji wake na zimewekwa katika lugha ambayo mwananchi mnyonge hawawezi kuielewa
MWISHO
No comments:
Post a Comment