About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Thursday, April 25, 2013

DC BABU UMESIKIKA, SHIRIKI KIKAMILIFU KUTATUA CHANGAMOTO ZINAZOLIKABILI JUKWAA


Na Stephano Mango, Songea

HIVI karibuni nilibahatika kutembelea Wilaya ya Rufiji iliyopo Mkoa wa Pwani kwa lengo la kwenda kujifunza namna Wakulima wa zao la Embe, Ufuta na Muhogo wanavyojihusisha na kilimo cha mazao hayo na tija yake katika ukombozi wa kiuchumi kwa jamii na Taifa kiujumla

Katika safari hiyo nilijifunza mambo mengi sana kuhusu kilimo cha mazao hayo ambayo yakiwekewa kipaumbele na wadau wake na Serikali, naamini kutokana na ushahidi uliopo kwa wakulima niliozungumza nao umaskini ungepungua kwa asilimia kubwa kwenye kaya nyingi zinazojihusisha na kilimo cha mazao hayo

Nina mengi sana ya kuelezea, lakini naomba wasomaji kwa leo nizungumzie ushirikiano uliopo kati ya Wakulima wa Embe, Ufuta na Muhogo, Mkuu wa Wilaya ya Rufiji Nurdin Babu na Wasimamizi wa Mradi wa Muvi Mkoa wa Pwani

Hakika ushirikiano huo utawezesha uzalishaji wa mazao hayo kuongezeka na upatikanaji wa masoko yenye uhakika kwani jukwaa ambalo wameliunda litawezesha kukabiliana na changamoto zilizopo na kusababisha upatikanaji wa maslahi bora

Jukwaa hilo ni muhimu sana katika maendeleo ya kilimo cha mazao hayo kwani watapata muda wa kujadiliana juu ya fursa, matatizo na changamoto wanazokabiliana nazo ili kuongeza tija kwa kila mmojawapo na kuepukana na unyonyaji unaofanywa na baadhi ya wajanja wachache kwenye minyororo ya thamani ya mazao hayo

Ili kulinda hali hiyo wajasiliamali hao wanalelewa kwa kiasi kikubwa sana na Mradi wa Muunganiko wa Wajasiriamali Vijijini (MUVI) ulioibuliwa kutekelezwa katika mikoa sita ya Tanzania bara, ukiwemo Mkoa wa Pwani na Ruvuma.

Kupitia mkopo ambao Serikali ya Tanzania ilipata toka shirika la IFAD ili kuinua hali duni ya wananchi wake ambapo fedha hizo ziko chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara katika shirika la SIDO kama watekelezaji wakuu

Mradi wa MUVI-Pwani unalenga kuwawezesha wajasiriamali wadogowadogo ili kuendeleza biashara zao zitakazo wawezesha kuinua vipata vyao ambapo mojawapo ya uwezeshwaji huo, ni kuimarisha ushiriki wa wadau mbalimbali katika minyororo ya thamani ya muhogo na embe, ili kuimarisha na kuongeza ubora wa mazao hayo.

Hivyo basi jukwaa la Majadiliano la wadau wa embe, muhogo na ufuta ni miongoni mwa jitihada za MUVI kwa kushirikiana na Halmashauri na wadau mbalimbali katika minyororo ya thamani ya mazao hayo ili kuwa na sehemu ya kukutana na kujadiliana namna ya kutatua kero mbalimbali

Kutokana na umuhimu huo Machi 26 mwaka huu, wadau hao walikutana mji mdogo wa Ikwiriri Wilayani Rufiji mkoani Pwani

Lengo likiwa wadau wakupokea na kujadili taarifa ya utekelezaji wa Mradi wa MUVI Pwani pia kupokea taarifa za wadau mbali mbali katika minyororo ya thamani ya embe, muhogo na ufuta. Kamati zilizotoa taarifa ni kamati ya wazalishaji, wasindikaji, pembejeo, fedha na mitaji.

Katika mkutano huo ambao uliwashirikisha wadau wengi zikiwemo taasisi za fedha ikiwemo Benki ya CRDB, watafiti, wasindikaji vyakula, wataalamu na viongozi wa Halmashauri ya wilaya na wadau wengine

Kwenye mkutano huo Mkuu wa Wilaya ya Rufiji Nurdin Babu alialikwa kuwa mgeni rasmi ambapo pamoja na mambo mengine aliyoyasema ni pamoja na … Nia yetu kubwa ya kukusanyika hapa leo hii, ni kwa ajili ya kufanya tathimini kupitia Jukwaa la Majadiliano kuhusu changamoto zinazokabili mazao matatu ambayo ni, embe, muhogo na ufuta

Pia alisema kwa fursa ya pekee tuliyoipata leo, ni vizuri tuzungumzie zaidi mazao ya muhogo na embe ambayo yana wanyonyaji wengi sana pasipo kujali nguvu nyingi inayotumiwa na wazalishaji hususani wakulima. Ninawasihi sana, tuuze mazao haya kwa faida za maendeleo kama vile kusomesha watoto, kujenga nyumba nzuri za kudumu na mambo mengine ya muhimu na si kuoa wake wengi wanaopelekea kuzorota kwa maendeleo.

“ Ndugu wakulima, siwezi kujitenga nanyi nawaahidi ushirikiano wa bega kwa bega ili tuweze kufikia malengo ya maendeleo endelevu ya wilaya yetu na watanzania kwa ujumla” alisema Babu

Hayo ndio yaliyonifanya niyatafakari kwa muda wa zaidi ya wiki mbili na kulazimika kuyaweka katika ukurasa huu ili wadau popote walipo waweze kuyajadili na kuyaenzi kwa maslahi ya jamii pana zaidi na Taifa kiujumla

Ni dhahiri wanarufiji wamejitahidi sana kuunda Jukwaa la Majadiliano la Wadau wa Muhogo, ufuta na Embe Rufiji ambalo lina malengo mbalimbali ambapo lengo kuu ni kuzalisha kwa wingi na kutetea thamani ya zao hilo katika masoko

Katika mradi huo wa Muvi unakabiliwa na changamoto ambazo zinapaswa kutatuliwa kwa haraka ili kuweza kuleta matokeo chanya kwenye Jukwaa hilo, na hapa ndipo ninapomuweka wazi Mkuu wa Wilaya ya Rufiji Nurdin Babu kushiriki kwa kina ndani na nje ya Serikali ili kufikia malengo ya wakulima hao, kwani alichokisema kwenye hotuba yake ya ufunguzi kimesikika

Na kilichobaki yeye kushiriki kutatua changamoto zinazowakabili wakulima hao ili kuweza kufikia malengo stahiki ya wanajukwaa ambao wanamatumaini mbalimbali katika jitihada za kilimo cha mazao hayo

Kwa mujibu wa taarifa ya utekelezaji wa Muvi Mkoa wa Pwani 2012/2013 kuna changamoto ambazo zinawakwaza kufikia malengo yao kwa wakati ikiwemo ,Mbinu za kisasa za uzalishaji ni mdogo, Ukosefu wa soko la mkataba, Kuinua kiwango cha usindikaji, Uzalishaji na usambazaji wa mbegu bora, Tozo zilizo na tija kwa wajasiliamali

Katika hilo ni vema Serikali mkoani Pwani ikajipanga kikamilifu kutatua changamoto hizo na jukumu kubwa la wanajukwaa kila mmoja kutimiza wajibu wake kwani Jukwaa la Majadiliano kwa mazao ya biashara ni muhimu sana kwa sababu wadau mbali mbali wanashirikishwa kuanzia ngazi ya chini hadi ya juu

Katika swala la huduma za fedha Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Ruvuma Devotha Likokola ambaye pia ni Mkurugenzi wa Vikoba Tanzania alikuwa ni miongoni mwa watu waliotoa mada siku hiyo

Pamoja na mambo mengine alisikika akiwashauri wanajukwaa kwa kusema ,,, huduma za fedha zilizo rasmi ni (12%) na wengine wanapata huduma zisizo rasmi. Aliendelea kwa kuzielezea huduma za fedha zinazotolewa na mabenki kama ya CRDB, NBC na NMB kuwa ni huduma rasmi kwa sababu zinasimamiwa na Benki Kuu ya Tanzania (B.O.T).

Likokola alisema kuwa huduma ambazo si rasmi alizitolea mfano kuwa ni SACCOS, FINCA, PRIDE, SELF, TUNAKOPESHA, na nyinginezo ambazo zinajumuisha (34%). Aidha aliendelea kwa kusema kwamba (36%) hawapo katika upande wowote iwe rasmi ama si rasmi.

Alizitaja njia kuu tatu (3) ambazo zinaweza kumpatia mtu pesa; nazo ni kufanya kazi/kilimo, kuajiriwa na kuwekeza na kuwataka kwamba wana Rufiji wakitaka kupatapesa, ni lazima wawe na pesa kwa kujiunga kwenye vikundi hasa Village Community Bank (VICOBA).

Kwa leo ninachoweza kusema tuanze upya kwa kuwa wajasiriamali mahiri chini ya Jukwaa bunifu kwani ujasiriamali ni ile hali, uwezo na mkakati au mchakato wa kubuni, kuanzisha, kuendesha na kumudu shughuli halali ya maendeleo ya kiuchumi

Tunahitaji ujasiliamali wa kujiamini, kuthubutu, kubuni na kuendeleza zao tokeo la ubunifu huo kwa kuleta faida chanya katika maisha yake, jamii na Taifa kiujumla kwani ujasiliamali ni nguzo muhimu kwa uchumi wa kisasa wa karne ya 21

Dhana ya ujasiliamali inatimia endapo hali ya kugundua au kubuni biashara mpya au kuiendeleza ile ya zamani kwa ajili ya kuwekeza na kutoa huduma stahiki kwa jamii pana, hivyo tuamue sasa kuwa katika hali hiyo katika jukwaa la dunia ili kuzifaidi fursa za uchumi za ndani na nje ya nchi

Uchumi wa dunia umebadilika, uchumi wa soko katika utandawazi ndio unashikilia mfumo wa kiuchumi wa dunia ili kuharakisha maendeleo kwa kutoa ajira mbadala kwa kujiajili, kujitegemea na kujenga uwezo wa kujiamini katika maisha na biashara kubwa dhana ya ujasiliamali chini ya Jukwaa inahitajika

Wahenga walisema huwezi kuzuia sikio lako kusikia lakini unaweza kuzuia mdomo wako usiseme, nami kwa hakika nasema nauzuia mkono wangu usiandike zaidi lakini siwezi kukuzuia msomaji kuendelea kusoma

Mwandishi wa Makala

Anapatikana 0715-335051

www.stephanomango.blogspot.com

No comments:

Post a Comment