Thursday, April 18, 2013
DC TUNDURU AMWAGIZA MKURUGENZI KUWACHUKULIA HATUA WATUMISHI WAZEMBE
Na Steven Augustino, Tunduru
MKUU wa Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma Chande Nalicho amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halamashauri ya Wilaya hiyo kuwachukulia hatua ikibidi hata kuwafukuza kazi Watumishi wasio wajibika zikiwa ni juhudi za Serikali kuinua taaluma Wilayani humo.
Nalicho alisema hayo wakati akifungua Mkutano wa kutathmini matokeo kidato cha pili,Nne na Sita uliofanyika katika ukumbi wa klasta Mjini hapa na kuongeza kuwa hali hiyo imetokana na Serikali kubaini kuwa watumishi wa kada zote Wilayani humo hawako tayari kufanya kazi kwa kujituma hali iliyopelekea Wilaya hiyo kuwa nyuma kielimu.
“Viongozi ndio wasiopenda kufanya kazi, wamebakia kulalamikia mishahara tu na ndiyo maana katika Wilaya hiyo imeendelea kuwa nyuma kielimu” alisema Nalicho na kumtaka Mkurugenzi awachukulie hatua za kinidhamu.
Alisema inashangaza kuona kuwa Wilaya ikiwa imekithiri kwa utoro wa wanafunzi lakini inapotokea ofisi yake inahitaji taarifa za matukio hayo hata Maafisa tarafa ,watendaji wa kata na viongozi wa vijiji wengi wanapoulizwa juu ya idadi ya wanafunzi waliofauru na kucahaguliwa kujiunga na masomo ya sekondari wanadai kutokuwa na takwimu zake.
Nalicho aliendelea kubainisha viashiria vingine vya viongozi hao kutowajibika kuwa ni pamoja na kuwepo kwa takwimu kubwa za utoro uliokithiri ambazo hazifanyiwi kazi ambapo alitolea mfano Shule ya msingi Njenga ambayo takwimu zinaonyesha kuwa mwaka 2010 ilifaulisha wanafunzi 41 waliokwenda shule walikuwa 3, mwaka 2011 waliofauru 46 walioendelea na masomo 7 na mwaka 2012 walifaulu 17 waliokwenda shule hadi sasa 1.
Nae Mwenyekiti wa Huduma za jamii na uchumi Diwani Athumani Nkinde pamoja na kukiri kuwa zipo Shule za Sekondari ambazo zilijengwa kisiasa na kutolea mfano shule za Sekondari Nampungu ambayo inaonesha kutelekezwa na wananchi kwa kutopeleka wanafunzi
Nkinde alipigilia msumali wa moto kwa kuzitaka mamlaka kuchukua hatua za kisheria kwa wanafunzi na wazazi wao kwavile kusoma ni lazima
Akizungumzia mikakati ya kuinua taaluma na kuiondoa idara yake katika kashfa ya kupeleka Sekondari wanafunzi wasiojua kuandika kusoma na kuhesabu Kaimu afisa elimu wa Shule za Msingi Mwl. Fraviani Nchimbi alisema kuwa Wilaya inaendelea kujidhatiti kwa kutumia mitihani ya majaribio katika kata pamoja na kuendesha mafunzo ya mada ngumu kwa walimu zikiwa ni juhudi za kuinua taaluma kwa wanafunzi.
Awali akisoma taarifa ya matokeo ya ufaulu wa wanafunzi katika kipindi cha mwaka 2011 na 2012 Afisa elimu Sekondari Mwl. Ally Mtamila alisema kuwa mbali na Wilaya hiyo kufanya vibaya lakini idadi ya walimu imeongezeka kutoka walimu 213 mwaka 2011 na kufikia 282 mwaka huu ongezeko ambalo pia limeongeza idadi ya walimu na kufikia wastani wa zaidi ya walimu 10 kwa kila shule ya sekondari Wilayani hapa.
Mwisho
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment