About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Wednesday, May 1, 2013

KWENYE TAIFA LA MBUZI HAKUNA MAANDAMANO WALA WANAMAGEUZI

JUZI nimeota ndoto ambayo licha ya kutafakari sana bado sijaweza kuipatia tafsiri yake.


Baada ya kujiuliza sana nimeona niwashirikishe wapendwa wasomaji ndoto yangu hiyo na labda nitapata watu wenye vipawa wanisaidie kunieleza maana ya ndoto hii.

Ni ndoto ambayo (kama ile njozi ya Mwanakijiji) imeniacha nikiwa na huzuni tele kwa yale ambayo niliyaona. Ndoto inahusu taifa la mbuzi.

Nilijikuta nimepata nafasi – kwenye hiyo ndoto - kutembelea nchi moja ambayo wananchi wake wote ni mbuzi.

Wote walikuwa mbuzi wakifanya shughuli mbalimbali za maisha. Wakulima, wafanyakazi maofisini, wasomi, maskini na matajiri kati yao wote walikuwa mbuzi.

Walikuwa ni mbuzi wa kila rangi, jinsi, makabila na dini. Japo walikuwa na tofauti zao hizo mbalimbali kitu kimoja kilikuwa dhahiri wote walikuwa ni mbuzi. Taifa hilo la mbuzi lilitawaliwa na chui.

Mbuzi wameshika hatamu


Chui waliamua aina na namna ya maisha ya mbuzi katika taifa lile na hakukuwa na namna yoyote ambayo mbuzi waliweza kutaka kitu tofauti na kile wanachotaka chui na wao wakakipata.

Kila ambacho chui walitaka walipata hata kama kingekuwa na madhara kwa mbuzi. Chui walishika hatamu ya uongozi wa kila kitu; walitawala Ikulu, Mahakama, Majeshi, Polisi, Bunge na hata Vyombo vya Habari.

Kote huko walikuwepo mbuzi wakifanya kazi na shughuli mbalimbali, lakini waliokuwa na umiliki walikuwa ni chui.

Kulikuwa na nyimbo zikiimbwa mara kwa mara kuwa chui wameshika hatamu. Na kwa kweli walishika hatamu bila wasiwasi.

Chui hawakuwahofia mbuzi hata siku moja na hivyo waliendelea kuwatawala wapendavyo. Kwenye hilo taifa la mbuzi; ambalo nililiona kwenye ndoto.

Chui walijenga zizi zuri la mbuzi

Kwenye hili taifa la mbuzi nchi nzima ni kama zizi la mbuzi. Zizi limejengwa vizuri, mipaka yake inaeleweka na chui wakijua kuwa ni maslahi yao kwa mbuzi kuishi zizini basi wameweka vyombo mbalimbali vya ulinzi kuwalinda ndani au kuzuia wanyama wengine wasiingie.

Hii haikatazi chui kuamua kula mbuzi wao. Mipaka imewekwa kwa ajili ya kulinda maadui wa nje tu na pale ambapo maadui wa nje wanatengeneza urafiki na chui basi hawaoni tatizo kuruhusu wageni hao kula na kutafuna vitoto vya mbuzi na kubeba mali za urithi wao.

Zizi hilo la mbuzi kwa kweli lilikuwa linavutia na kwa kuangalia kwa haraka haraka makundi mengi ya mbuzi yalikuwa yanafurahia kuishi ndani ya zizi hilo.

Wenyewe walikuwa wanasema kuwa chui ameleta ‘amani, umoja na mshikamano’ na hivyo mbuzi wote ni lazima washukuru na kulinda na kuienzi amani hiyo iliyoletwa na chui.


Mbuzi waliojipendekeza kwa chui kwa hakika waliishi na kujisikia kama vile na wao ni chui wadogo au siku moja watageuka kuwa chui.

Kwa kadiri nilivyowaona walikuwepo mbuzi ambao hata walianza kujipaka rangi rangi waonekane kama chui. Ati wengine waliacha kula majani na kuanza kula nyama.

Utawala wa chui kisaikolojia kwenye zizi la mbuzi

Taifa la mbuzi ambalo nililiona ndotoni, chui waliwatawala mbuzi kifikra, waliwafanya duni kiasi kwamba hawakuwa na kitu chochote ambacho wangeweza kufanya bila ya kutaka kupata baraka kutoka kwa chui; au uongozi wa chui.

Na hakuna kitu kibaya sana katika maisha ya kiumbe kama kutawaliwa kifikra. Niliwaza katika ndoto hiyo jinsi ambavyo wanadamu wanawatawala wanyama wengine kifikra na kuwafanya wafanye vitu ambavyo kwa hulka yao hawawezi kufanya.

Wanadamu wameweza kuwamiliki mbwa, ng’ombe, farasi, punda, paka na kuku. Lakini pia wanadamu wameweza kuwamiliki tembo na kuwafundisha.

Kitu ambacho wanadamu wameweza kuwafanya ni kutawala fikra na hulka za wanyama hao kiasi cha kuwamiliki na kuwaweka kwenye utumishi wa binadamu.

Ndivyo hivyo ilivyokuwa kwa chui dhidi ya wale mbuzi. Chui waliweza na zaidi ya kuweza kuwamiliki na kuwatawala mbuzi.

Walikuwepo mbuzi wapendwa wa chui

Nikaona pia jinsi baadhi ya mbuzi kutokana na njaa na hamu ya kutaka kuonekana ni wa muhimu walivyokuwa wanajipendekeza kwa chui. Hawa walikuwa wasaliti wa mbuzi wenzao.


Walikuwa wachongezi na mipango yote ya mbuzi kutaka kujikomboa ilijulikana kwa chui. Sababu ni uwepo wa mbuzi waliokuwa wanapenda kuonekana na chui.

Baadhi ya mbuzi waliamua kabisa kujitenga na mbuzi wenzao na kutwa kucha waliimba sifa za chui.

Ooh Chui wajenga nchi

Ooh Chui ndio nambari wani

Ooh Chui bila wao haiwezekani

Ooh Chui wadumu!!

Nyimbo kama hizo zilisikika hata kwa baadhi ya watoto wa mbuzi.

Na chui hawakuwa wanyimi. Waliwatuza mbuzi wasaliti na wale walionunuliwa. Mbuzi hawa walipewa vyeo katika kambi za chui, walipewa ajira na hata wakati mwingine waliwekwa kwenye Baraza la Chui na kwa hakika na wao walijiona wamefika. Mbuzi katika himaya ya chui.

Mbuzi hawatakiwi kujitambua wanaonewa

Katika hilo taifa la mbuzi kulikuwa na sheria nyingi sana na mazoea ya kila aina. Lakini kubwa kuliko yote ilikuwa ni marufuku kwa mbuzi kulalamika kuwa wanaonewa.

Mbuzi waliaminishwa kuwa chui wanawatawala kwa ‘nia njema’ na kuwa yote ambayo chui wanafanya ni kwa ajili ya kuwanufaisha wao mbuzi.

Elimu ya mbuzi ilikuwa duni, lakini chui walisema kuwa wanajitahidi kuongeza bajeti ili kuinua kiwango cha elimu. Chui walikuwa wakifanya haraka kuonesha idadi ya mashule ilivyoongezeka chini ya utawala wao na jinsi ambayo chini ya awamu nyingine ya utawala wa chui watoto wanaoenda shule kwa mara ya kwanza ni karibu asilimia 100 japo wanaofeli ni karibu asilimia hiyo hiyo.

Mbuzi wakilalamika kuhusu barabara, chui hawacheleweli kuwaonesha barabara mbalimbali zilizojengwa au ‘kuunganisha’ sehemu mbalimbali za zizi (ili mbuzi wasiwe na tatizo la kutoka upande mmoja wa zizi kwenda upande mwingine) au kujengwa kwa ‘kiwango cha lami.’

Na kweli niliona chui wakishindana kufungua barabara mbalimbali na madaraja makubwa. Niliona kwenye ndoto hiyo baadhi ya mbuzi waandamizi wakiwasifia chui kwa kuboresha barabara.

Chui walikuwa wanakula mbuzi na mazao ya mbuzi

Kitu pekee ambacho kilikuwa ni siri iliyo wazi ni kuwa chui walikuwa wanakula mbuzi na pamoja na mbuzi walijipa uhalali wa kila ambacho mbuzi wanazalisha.

Pamoja na yote ambayo chui walikuwa wanajisifia kuwa wameyafanya kwa niaba ya mbuzi, ukweli mmoja ulikuwa wazi, chui walikuwa wanawatunza mbuzi kwa ajili ya siku za kuwala.

Na siku hiyo ikifika chui walikuwa wanajua cha kuchagua. Walikuwa wanakula vile vilivyonona; japo hawakuwa na mwiko wa kula vilivyokonda.

Mbuzi wengine waliona hili na wakajaribu kulihalalisha kuwa kama chui anawatendea mema kiasi hicho na kuwatengenezea zizi lao vizuri basi wana haki (mara moja moja) ya kula mazao waliyoyapanda.

Yote niliyaona kwenye hiyo ndoto ya taifa la mbuzi. Nikaona na mengine.

Taifa la mbuzi halina migomo, maandamano wala kupinga utawala wa chui.

Kati ya vitu vilivyonishangaza sana katika taifa hili, japo kwa kweli havikunishangaza sana kwa vile najua tabia ya chui, ni kuwa mbuzi hawakutakiwa kuandamana au kugoma.

Mbuzi wachache walipojaribu kugoma tu, wengine hawakuwa tayari kuwaunga mkono kwa sababu wakiwaunga mkono chui watakasirika na kasheshe linaweza kutokea zizini.

Katika zizi hilo la mbuzi hakukuwa na migomo; mbuzi wagome halafu ‘wakale wapi’? Hivyo mbuzi niliwaona wakiendelea kulalamika chini kwa chini, lakini hawakuwa na ujasiri wa kupinga.

Maandamano ya mbuzi yaliwahi kujaribiwa lakini chui hawakuchelewa kuwashughulikia; na waliwashughulikia kwa kuwatuma watumishi wakubwa kabisa wa chui – mbwa.

Mbwa ambao waliamini kuwa wanaleta ulinzi maridhawa wa mbuzi – kumbe wanawatumikia chui.

Hili la mbwa nitalisema kidogo baadaye. Mbuzi hawaandamani zizini kwani chui hawapendi kupingwa; hawapendi kukosolewa na kwa hakika kabisa kama kuna kitu ambacho chui hawataki kabisa kionekane zizini ni aina yoyote ya mwamko wa mabadiliko ya kifikra.

Nasikia kuna mbuzi walishawahi kuwekwa kifungoni na wengine kubambikiziwa kesi kwa sababu tu walisema neno baya (wenyewe chui waliita la kichochezi) kwa wakubwa.

Katika kuhakikisha kuwa chui wanatawala kwa raha basi mfumo mzima wa kisiasa wameudhibiti vizuri sana.

Mbwa wa watawala hawajali mbuzi

Sasa katika vitu ambavyo nilivona kwenye ndoto ya hilo taifa la mbuzi, ni kuwa mbwa wanaolishwa na kutunzwa na chui hawajali kinachowatokea mbuzi.

Ikumbukwe kuwa mbwa wote ni watumishi wa chui na chui huamua mbwa ale nini, alale wapi na apate nini kama zawadi. Na mbwa wanavyopewa sifa kwa kweli hawana huruma. Wanaweza kumnga’ata yeyote, popote na kwa lolote kwa sababu tu wanaweza.

Baadhi ya mbuzi wamejaribu mara kwa mara kuwashawishi mbwa wageuke na kujali mbuzi. Bahati mbaya sana mbwa hawawezi kufanya hivyo kwa sababu utii wao uko kwa chui.

Ilitokea mara kwa mara ambapo chui mkuu alitoa zawadi mbalimbali kwa mbwa wakali zaidi na waliofanya kazi vizuri ya kuhakikisha zizi liko tulivu, lina amani.


Niliona baadhi ya mbwa wakipewa tuzo za mashada ya maua ati za utumishi uliotukuka.


Lipo Bunge la mbuzi

Kati ya mambo mengi ya ajabu niliyoyaona katika ndoto yangu ni lile Bunge la mbuzi. Katika Bunge hilo nilishangaa kuona kuwa mbuzi wanagombania kujipendekeza kwa chui.

Lilikuwa ni Bunge la ajabu kwani kuanzia spika hadi mtumishi wa Bunge hilo wote wamegawanyika au wanaunga mkono utawala wa chui au wanajaribu kutetea maslahi ya mbuzi.

Hata hivyo wanaojaribu kutetea maslahi ya mbuzi hawakuwa na nguvu zaidi ya kupiga kelele kwani mamlaka yote ya kuendesha mambo yalikuwa mikononi mwa chui.

Katika Bunge la mbuzi niligundua chui wametamalaki; lakini mbuzi nao walijitahidi kujitutumia na kuwasumbua chui. Chui ikabidi wabadili kanuni ili kuwadhibiti mbuzi.

Hata hivyo wapo mbuzi waliojitambua

Wakati usingizi ukikaribia kuniisha katika ndoto yangu nilishangaa kuona kikundi kikubwa cha mbuzi wamejikusanya chini ya jabali wakifanya mikakati ya mabadiliko ya utawala wao zizini.

Nilisogea kwa karibu na kuangalia na kutazama. Niliowadhania kuwa ni mbuzi kumbe walikuwa ni simba wanaotawaliwa na chui.

Walikuwa ni simba ambao walitawaliwa kifikra na chui kiasi cha kujisahau ukuu wao. Walikuwa ni simba ambao chui wamewalazimisha kuvaa ngozi za mbuzi.

Lakini si tu kuvaa ngozi za mbuzi, pia kufikiria kama mbuzi, kuishi kama mbuzi katika zizi la mbuzi.

Nilichoona ni taifa la simba lililogeuzwa la mbuzi likitawaliwa na chui kama taifa la mbuzi.

Siku moja mmoja wa wale simba akiwa katika Bunge la mbuzi alilalamika kidogo na kudai kuwa inawezekana vipi ‘akili ndogo (za chui) kutawala akili kubwa (za simba)?’ Chui walikasirika.

Mbuzi mmoja ambaye kwa kweli ni simba alijaribu kuunguruma kidogo na kusema: “Chui mkuu dhaifu”! Ungeona jinsi chui walivyotaharuki. Kwa mbali nilianza kuona matumaini kwamba yumkini simba wameanza kujitambua kuwa wao siyo mbuzi.

Usingizi ukanitoka bila ya kujua hitimisho la hilo taifa na kama kuna uwezekano hilo taifa lipo duniani.

Nilipokaa kitandani nikitweta huku nikinywa maji ya baridi nikakumbuka kisa nilichokisikia utotoni.

Kuliwahi kutokea kuku kujikuta ametamia mayai ya mwewe pamoja na mayai yake. Jinsi alivyopata mayai ya mwewe sikumbuki, lakini vifaranga vyote vilipototolewa yule kuku alivilea vyote vizuri kabisa na vyote vilikuwa pamoja kama ndugu.

Kwa kadiri vilivyokuwa vikikua ndivyo tofauti yao ilivyozidi kuonekana. Hata hivyo vile vifaranga vya mwewe viliishi kama vifaranga vya kuku.

Na vyenyewe vilikuwa vinatafuta vijidudu ardhini kwa kutifuatifua kama vifaranga vya kuku. Cha kushangaza japo labda si sana, ni kuwa mwewe walipopita angani kuku alikimbia na vifaranga vyake pamoja na vile vya mwewe. Vyote vilijificha.

Hadi siku moja akatokea mmbeya mmoja ambaye aliona vifaranga vya mwewe vikiishi kama kuku na kuwaogopa mwewe.

Ilifika mahali hata wakati wa kunywa maji vile vimwewe vidogo navyo viliinua jicho juu kuangalia kama kuna mwewe. Mmbeya huyo aliwaita chemba wale vifaranga wa mwewe na kuwaonesha kioo wajiangalie. Nusura wakimbie walipoona wanaangaliana na mwewe.

Ndipo wakatambua ukweli kuwa wao si kuku ni mwewe. Hawakuamini lakini wakajaribu kuruka. Ilikuwa rahisi kwao kuliko walivyotarajia na walijihisi kama minyororo fulani imeachilia. Na walipoenda juu wale ‘ndugu zao’ walianza kuwakimbia. Mwewe hageuki kuku kwa kufugwa.

Simba hata avishwe ngozi ya mbuzi hawi mbuzi. Ila kama anaamini ni mbuzi nani atamfungua?

‘Well’ ni matumaini yangu taifa la mbuzi halipo duniani!

No comments:

Post a Comment