Sunday, June 16, 2013
KITUO CHA SAUTI YA JAMII SONGEA CHAPEWA MSAADA WA KOMPYUTA NA TGNP
Na, Stephano Mango, Songea
WANAWAKE waliopo pembezoni wametakiwa kukithamini na kukitumia Kituo cha taarifa na maarifa ili kuweza kupaza sauti zao kikamilifu katika changamoto zinazowakabili kwenye ujenzi wa tapo la ukombozi wa wanawake kimapinduzi
Wito huo umetolewa jana na Afisa Habari na Mawasiliano wa Mtandao wa Jinsia Tanzania ( TGNP) Lilian Kitunga alipokuwa akikabidhi msaada wa Kompyuta,printer, moderm na muda wa maongezi vyenye thamani ya shilingi milioni 1.9 kweny Ofisi ya Sauti ya Jamii Kituo cha Taarifa na Maarifa Songea
Kitunga alisema kuwa msaada huo unapaswa kutumiwa kwa malengo kusudiwa ya mawasiliano kwa kuwafikia watu mbalimbali, kujenga nguvu ya pamoja katika kuleta mabadiliko chanya kwa kutumia ujumbe mfupi wa simu (sms) kwa gharama za Tgnp ili kuweza kuunganisha nguvu katika kuhabarishana na kuchukua hatua za kuwajibisha mamlaka na kuleta mabadiliko chanya
“Sauti ya Jamii itatumia teknolojia ya bulk sms kwa kutuma ujumbe kwenye simu kwa kutumia Kompyuta kwa zaidi ya watu 10,000 kwa wakati mmoja kwa lengo la kupashana habari za ujenzi wa vuguvugu la kimapinduzi” alisema Kitunga
Alifafanua kuwa kwa zaidi ya miaka 18 sasa, Tgnp imejikita katika harakati za kupigania haki za binadamu hasa wanawake na makundi yaliyopo pembezoni, usawa wa kijinsia, pamoja na ujenzi wa vuguvugu la ukombozi wa wanawake kimapinduzi katika ngazi zote za kijamii
Alisema kuwa Tgnp kwa kushirikiana na wada wengine ilibaini kuwa mbinu za kupeana taarifa kwa wakati baina ya vikundi na asasi za kimataifa ni tatizo kubwa ambalo linakwamisha jitihada za ujenzi bora wa tapo la ukombozi wa wanawake wa kimapinduzi
Alieleza kuwa ili kukabiliana na tatizo hilo moja ya mikakati iliyowekwa ni kuanzisha na kuviendeleza vituo vya Taarifa na Maarifa kwa kushirikiana na jamii ambavyo vitakuwa vitovu vya harakati katika ngazi ya jamii
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Sauti ya Jamii Kituo cha Taarifa na Maarifa Songea Fatuma Misango alisema kuwa mradi huo ulibuniwa na Tgnp utaongeza chachu ya kuleta mabadiliko katika jamii na kuboresha mahusiano na mitandao ya kupashana habari kati ya Wanaharakati, Vikundi na Mitandao katika ngazi ya Jamii hadi Taifa ili kupunguza pengo kati ya wanao faidi taarifa muhimu na wale ambao hawapati taarifa hizo
Misango alisema kuwa kuanzishwa kwa Kituo hicho kutasaidia kunoa uelewa wa wanawake waliopo pembezoni wa uchambuzi wa masuala ya kimfumo, Kisera na kimuundo na kutumia chambuzi hizo katika kudai uwajibikaji na mabadiliko yenye mrengo wa ukombozi wa wanawake wa kimapinduzi
MWISHO
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment