About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Thursday, September 19, 2013

WAANDISHI WAKWIDWA , WANYANYASWA NA KUPOKEA KIPIGO




Na Dixon Busagaga, Moshi

WAKATI watuhumiwa wanne zaidi wakiongezwa katika kesi ya mauaji ya mfanyabiashara wa madini ya tanzanite mkoani Arusha, Erasto Msuya, waandishi wanaoiripoti jana walionja joto ya jiwe kwa kukwidwa na kutaka kunyang’anywa vitendea kazi vyao.

Tafrani hiyo ilitokea katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mjini Moshi saa 5:30 wakati kesi hiyo inayowakabili washtakiwa saba wanaodaiwa kushiriki kupanga na kutekeleza mauaji ya Msuya ilipofikishwa mbele ya mahakama kwa ajili ya kutajwa.

Akizungumzia tukio hilo, mmoja wa waandishi hao, Fadhili Athuman alisema kuwa walipata wakati mgumu walipojaribu kuchukua picha za ndugu wa Msuya.

Athuman alisema kuwa baada ya kupiga picha kadhaa, alikwidwa na wanafamilia hao, wakitaka kumpora kamera huku mwandishi mwenzake akishikwa na kupigwa kibao.

“Baada ya kesi kuahirishwa iliibuka tafrani, walitaka kuninyang’anya kamera ili wafute picha nilizokuwa nimepiga. Mwenzangu yeye alikamatwa na kupigwa vibao kabla askari wa kikosi cha FFU kumuokoa,” alisema.

Kwa mujibu wa mmoja wa watu wa karibu na familia ya Msuya ambaye aliomba kuhifadhiwa jina, wamechukizwa na hatua ya baadhi ya waandishi kutochapisha picha za watuhumiwa, na badala yake zinatolewa za wanafamilia hiyo.

Hali ya taharuki ilianza mapema baada ya chumba kilichozoeleka kuendeshea kesi hiyo kubadilishwa kwenda kwenye chemba kutokana umati wa watu uliohudhuria kuwa mkubwa.

Wakati huo huo, vilio viliendelea kutawala mahakamani hapo baada ya kesi hiyo kuahirishwa. Mama mzazi wa Msuya, Marry Msuya alipoteza fahamu na kukimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC.

Awali mbele ya Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Ruthi Mkisi, mawakili wa serikali, Stella Majaliwa akisaidiwa na Janeth Sipule waliieleza mahakama kuwa washitakiwa wanne wameunganishwa katika kesi hiyo na kufikia saba.

Majaliwa aliwataja waliounganishwa kuwa ni mshitakiwa wa nne hadi saba ambao ni Jalila Zuberi, Karimu Kihundrwa, Sadiki Jabiri (Chusa) na Joseph Mwakipasile ambao wote walifika mahakamani hapo.

Hakimu Mkisi alisema kesi hiyo imeahirishwa kutokana na upelelezi kutokamilika na hivyo kutaka washitakiwa hao kurudi rumande hadi Oktoba 2, mwaka huu.

Agosti 21, mwaka huu, washitakiwa watatu; Sharifu Mohammed, mkazi wa Kimandolu Arusha, Shaibu Mpungi, mkazi wa Kijiji cha Songambele wilayani Mererani na Musa Mangu mkazi wa Shangarai kwa Mrefu Arusha, walifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza.

Washitakiwa wote saba waliondolewa mahakamani hapo chini ya ulinzi mkali wa askari wenye silaha za moto wakiwa ndani ya gari lenye namba za usajili T 743 ADC lenye vioo vyeusi.

Msuya aliuawa Agosti 7 mwaka huu saa 6:30 mchana kwa kupigwa risasi 13 kifuani, kando ya barabara kuu ya Arusha – Moshi katika eneo la Mjohoroni wilayani Hai.

No comments:

Post a Comment