About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Saturday, October 26, 2013

DKT NCHIMBI APIGWA MAWE SONGEA NA MSAFARA WAKE


Waziri wa mambo ya Ndani ya Nchi Dkt Emmanuel Nchimbi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini

Na Stephano Mango,Songea

MSAFARA wa Waziri wa mambo ya Ndani ya Nchi Dkt Emmanuel Nchimbi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini Wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma wapigwa mawe na wananchi waliojitokeza kuzungumzia kero ya daraja la Matarawe ambalo linadaiwa kusababisha vifo vya watu zaidi ya watatu katika mwezi huu wa octoba mwaka huu

Wananchi hao wa kata ya Matarawe  Manispaa ya Songea,wakiwemo waendesha  Pikikipiki maarufu kwa jina la Yebo Yebo  walifunga barabara kwa  zaidi ya masaa mawili na kufanya fujo za kung’oa kingo za daraja  pamoja na kuweka  magogo na mawe  katikati ya daraja na kuchoma matairi moto  ili Mbunge huyo asipite mpaka atoe majibu ya kina kuhusu daraja

Hali hiyo ililazimisha Jeshi la polisi kuwatawanya  wananchi hao kwa kuwafyatulia mabomu ya machozi kwa lengo la kuzuia uharibifu zaidi na kuufanya msafara upite wakati ukirudi kutoka kwenye Mkutano wa hadhara wa Matarawe baada ya kuzuiriwa wakati wa kwenda na wakati wa kurudi ambapo hadi sasa watu nane wanashikiliwa na Jeshi hilo kutokana na vurugu hizo.

Tukio hilo limetokea jana kati ya saa kumi  hadi saa kumi na mbili jioni  ambapo wananchi hao wakiwa na hasira walifanya fujo hizo  wakiwa na lengo la kumshinikiza Mbunge wa Jimbo la Songea  mjini ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Dkt.Emmanuel Nchimbi  awasaidie kupanua daraja  la mto Matarawe ambalo ni dogo kwani kwa  muda mrefu limekuwa likisababisha ajalli mara kwa mara katika eneo hilo kutokana na ufinyu wa daraja hilo.

Awali  Mbunge huyo akiwa katika ziara yake ya siku ya pili akitokea  mtaa wa Liumbu kata ya Mletele  kukagua shughuli mbali mbali za maendeleo pamoja na kuzungumza na wananchi akiwa anaelekea kata ya matarawe  kwenye mkutano wa hadhara ndipo alikutana na umati mkubwa wa wananchi wakiwemo  waendesha piki piki  walikuwa wamezuia njia na kusimama njiani ili asikilize kero zao kutokana na watu kufa mara kwa mara ambapo siku moja kabla ya mbunge huyo kufanya ziara kuna kijana aliyetambulika kwa jina la Mashaka Nuhu mkazi wa Matarawe akiwa anaendesha piki piki alitumbukia mtoni na kufariki dunia papo hapo.

Hata hivyo Dkt.Nchimbi alilazimika kusimama na kushuka kwenye gari yake  akiwa ameongozana na viongozi mbali mbali wa  chama na Serikali akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Songea Joseph Joseph Mkirikiti  ambapo Mbunge huyo aliwapa pole kwa ajali zinazotokea na kwa watu ambao wamepoteza ndugu zao alizungumza nao na kuwataka wawe na subira  wakati ombi lao linashugulikiwa, majibu ambayo wanachi hao hawakulizika nayo

“Natoa pole sana kwa msiba na ajali ambazo zimetokea nimewasikia, na ninaahidi  nitawajengea daraja  hili ,kama nimeweza kujenga barabara hii kwa kiwango cha lami bila maandamano wala kufungiwa barabara nitashindwa daraja? hivi ni vitu vinavyozungumzika  hili ni jambo dogo hivyo naomba  twende kwenye mkutano wa hadhara na tutaongea vizuri zaidi , kwani ni kweli daraja ni finyu na linahitaji kufanyiwa maboresho zaidi, ‘alisema Dkt. N chimbi.

Dkt.Nchimbi akiwahutubia Wananchi  kwenye mkutano wa hadhara  uliofanyika kwenye viwanja vya  Shule ya sekondari ya kutwa ya matarawe  amesema,amesikitishwa na tukio hilo kwani tabia hiyo haipendezi ,haikubaliki na haina maadili na aina
tija kama wangekuwa na busara wangefika kwenye mkutano na kutoa kero zao badala ya kufanya fujo ambapo ameliagiza jeshi  la polisi kuwasaka wahusika wa fujo hizo.

Amesema, ni kweli daraja hilo ni dogo ila siyo ustarabu kufunga barabara kwa masaa mawili kwani wamesababisha shughuli mbali mbali za maendeleo kusimama kutokana na barabara hiyo kufungwa  na kwamba tayari ameshamuagiza Mhandisi wa halmashauri ya Manispaa hiyo kufanya tathmini ili kujua gharama zinazohitajika ili liweze kupanuliwa.

Mapema Diwani wa kata ya Matarawe James Makene aliungana na kundi kubwa la wananchi hao na alimweleza Nchimbi kuwa  hiyo ni changamoto ambayo wakazi wa matarawe  wamekuwa wakilia kila mara hivyo wanahitaji msaada wa kupanua daraja hilo ambalo limeonekana kuwa ni kero ya muda mrefu.

Kwa upande wake kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma Deusdedit Msimeki ameeleza kuwa kufatia vurugu hizo tayari watu nane wanashikiliwa na wanaendelea kuhojiwa zaidi ili kuwabaini vinara wengine wa fujo waliowashawishi wananchi kufanya fujo hizo .
MWISHO.

Thursday, October 3, 2013

MASHINE ZA TRA ZAZUA BALAA, WENGINE WASHUSHIANA MKON'GOTO



Na Kenneth Ngelesi

WAFANYABIASHARA mkoani Mbeya wamezua kizaazaa wakigoma kufungua maduka wakipinga agizo la Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) linalowataka kununua mashine za kielektroniki kwa ajili ya kukatia risiti za wateja pindi wanapowauzia bidhaa.

Katika sokomoko hilo lililotokea jana na kusababisha taharuki kwa muda kadhaa, wafanyabiashara hao wanadai kuwa gharama za mashine zitolewe na serikali.

Eneo la Soko la Sido ambalo lina wafanyabiashara wengi na tegemeo katika uchumi wa Jiji la Mbeya, walifunga biashara zao kwa muda usiojulikana.

Kadhia hiyo inakuja siku moja tangu Mkuu wa Mkoa huu, Abbas Kandoro, akutane na viongozi wa wafanyabiashara kutoka Soko la Sido na kuwataka viongozi kuwataarifu wenzao wasitishe mkutano ambao walitaka kuufanya jana katika uwanja wa Shule ya Msingi Ruanda Nzovwe.

Kandoro alifikia uamuzi wa kukutana na viongozi hao baada ya kupata taarifa kupitia gari la matangazo ambalo lilikuwa likipita na kuzunguka katikati ya jiji na kuwataka wafanyabiashara hao kufunga maduka na kufika mkutanoni ili kujadili suala zima la mashine hizo.

Taarifa zinadai kuwa baada ya Kandoro kusikia matanagzo hayo, aliliagiza Jeshi la Polisi kumkamata dereva wa gari hilo pamoja na Mwenyekiti wa Soko la Sido na kuwaweka rumande kwa muda usiojulikana.

Baada ya wawili hao kuwekwa ndani, lilitolewa agizo la kuzunguka tena mitaani kwa kutumia gari hilo ili kuwatangazia wafanyabiashara hao kuwa mkutano huo umesitishwa.

Uamuzi wa kusitisha mkutano huo ulipuuzwa na wafanyabiashara hao ambao jana waliendelea na maandilizi ikiwa ni kukodi gari jingine la matangazo kupita mitaani kuwahimiza wenzao kujitokeza kwa wingi. 

Hatua hiyo iliufanya uongozi wa mkoa kuwasambaza polisi mitaani kuzuia mkutano huo. Mabomu ya machozi na maji ya kuwasha vilitembezwa kwa wafanyabiashara hao ambao walikuwa wamekusanyika huku maduka yao yakiwa yamefungwa.

Mabomu hayo ya polisi yaliwaathiri wanafunzi wa Shule ya Msingi Kagera na kuwafanya wataharuki na kuanza kukimbia hovyo huku wengine wakizirai.

Kufuatia hali hiyo, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Ayoub Kiwanga, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Ilomba, Erasto Mwakaponda na Diwani wa kata hiyo, Dickson Mwakilasa, walikubaliana kuwakabidhi wanafunzi hao kwa wazazi wao waliofika shuleni hapo kuwajulia hali baada ya kupokea taarifa za kupigwa mabomu.

Wakizungumza na Tanzania Daima, wafanyabiashara hao walisema kuwa wanashindwa kuelewa nguvu kubwa ambayo inatumiwa na polisi wakati hakuna vurugu zozote katika eneo hilo.

Alex Oswald, kwa niaba ya wenzake alisema kuwa wao waliamua kufunga maduka kwa hiari yao na kwamba lengo la mkutano lilikuwa kutoa msimamo wa kuiomba serikali itoe mashine hizo bure.

Naye Peter Tweve, alisema kuwa kimsingi wao hawajagoma kutumia mashine hizo bali wanataka wawekewe bure, kwani si kila mfanyabiashara anaweza kuinunua mashine hiyo ambayo kwa sasa inauzwa kwa sh 800,000.

Alipotafutwa Kandoro kuelezea tukio hilo, aligoma akisema kuwa yupo katika kikao, pia Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Diwani Athumani, simu yake iliita bila kupokewa.

Wiki moja iliyopita, Mkurugenzi wa Elimu ya Kodi wa TRA, Richard Kayombo, alitoa taarifa kuwa wafanyabiashara wenye mapato ya zaidi ya sh 45,000 kwa siku wanapewa hadi Oktoba 14, mwaka huu wawe wamenunua mashine hizo.