WAFANYABIASHARA mkoani Mbeya wamezua kizaazaa wakigoma kufungua
maduka wakipinga agizo la Mamlaka ya Mapato nchini (TRA)
linalowataka kununua mashine za kielektroniki kwa ajili ya kukatia
risiti za wateja pindi wanapowauzia bidhaa.
Katika sokomoko hilo lililotokea jana na kusababisha taharuki kwa muda
kadhaa, wafanyabiashara hao wanadai kuwa gharama za mashine zitolewe na
serikali.
Eneo la Soko la Sido ambalo lina wafanyabiashara wengi na tegemeo
katika uchumi wa Jiji la Mbeya, walifunga biashara zao kwa muda
usiojulikana.
Kadhia hiyo inakuja siku moja tangu Mkuu wa Mkoa huu, Abbas Kandoro,
akutane na viongozi wa wafanyabiashara kutoka Soko la Sido na kuwataka
viongozi kuwataarifu wenzao wasitishe mkutano ambao walitaka kuufanya
jana katika uwanja wa Shule ya Msingi Ruanda Nzovwe.
Kandoro alifikia uamuzi wa kukutana na viongozi hao baada ya kupata
taarifa kupitia gari la matangazo ambalo lilikuwa likipita na kuzunguka
katikati ya jiji na kuwataka wafanyabiashara hao kufunga maduka na
kufika mkutanoni ili kujadili suala zima la mashine hizo.
Taarifa zinadai kuwa baada ya Kandoro kusikia matanagzo hayo,
aliliagiza Jeshi la Polisi kumkamata dereva wa gari hilo pamoja na
Mwenyekiti wa Soko la Sido na kuwaweka rumande kwa muda usiojulikana.
Baada ya wawili hao kuwekwa ndani, lilitolewa agizo la kuzunguka tena
mitaani kwa kutumia gari hilo ili kuwatangazia wafanyabiashara hao kuwa
mkutano huo umesitishwa.
Uamuzi wa kusitisha mkutano huo ulipuuzwa na wafanyabiashara hao ambao
jana waliendelea na maandilizi ikiwa ni kukodi gari jingine la
matangazo kupita mitaani kuwahimiza wenzao kujitokeza kwa wingi.
Hatua
hiyo iliufanya uongozi wa mkoa kuwasambaza polisi mitaani kuzuia mkutano
huo. Mabomu ya machozi na maji ya kuwasha vilitembezwa kwa
wafanyabiashara hao ambao walikuwa wamekusanyika huku maduka yao yakiwa
yamefungwa.
Mabomu hayo ya polisi yaliwaathiri wanafunzi wa Shule ya Msingi
Kagera na kuwafanya wataharuki na kuanza kukimbia hovyo huku wengine
wakizirai.
Kufuatia hali hiyo, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Ayoub Kiwanga, Ofisa
Mtendaji wa Kata ya Ilomba, Erasto Mwakaponda na Diwani wa kata hiyo,
Dickson Mwakilasa, walikubaliana kuwakabidhi wanafunzi hao kwa wazazi
wao waliofika shuleni hapo kuwajulia hali baada ya kupokea taarifa za
kupigwa mabomu.
Wakizungumza na Tanzania Daima, wafanyabiashara hao walisema kuwa
wanashindwa kuelewa nguvu kubwa ambayo inatumiwa na polisi wakati hakuna
vurugu zozote katika eneo hilo.
Alex Oswald, kwa niaba ya wenzake alisema kuwa wao waliamua kufunga
maduka kwa hiari yao na kwamba lengo la mkutano lilikuwa kutoa msimamo
wa kuiomba serikali itoe mashine hizo bure.
Naye Peter Tweve, alisema kuwa kimsingi wao hawajagoma kutumia mashine
hizo bali wanataka wawekewe bure, kwani si kila mfanyabiashara anaweza
kuinunua mashine hiyo ambayo kwa sasa inauzwa kwa sh 800,000.
Alipotafutwa Kandoro kuelezea tukio hilo, aligoma akisema kuwa yupo
katika kikao, pia Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Diwani Athumani,
simu yake iliita bila kupokewa.
Wiki moja iliyopita, Mkurugenzi wa Elimu ya Kodi wa TRA, Richard
Kayombo, alitoa taarifa kuwa wafanyabiashara wenye mapato ya zaidi ya sh
45,000 kwa siku wanapewa hadi Oktoba 14, mwaka huu wawe wamenunua
mashine hizo.
|
No comments:
Post a Comment