About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Sunday, January 2, 2011

UJENZI WA MNARA WA MASHUJAA WALIONYONGWA NA WAJERUMANI NI KIELELEZO MUHIMU CHA KUWAENZI



Na, Stephano Mango, Songea

ENEO waliponyongwa viongozi na askari 67 walioshiriki kupigana vita vya Majimaji februari 27,1906 linatarajiwa kujengwa mnara wa kumbukumbu ili kuweka alama ya kudumu na wananchi waweze kupatambua na kupaenzi kikamilifu.

Philip Maligissu ambaye ni Mhifadhi kiongozi wa Makumbusho ya Taifa ya Majimaji Songea,akizungumza na Waandishi wa Habari ofisini kwake hivi karibuni anasema, eneo hilo ni muhimu sana kwa historia ya nchi yetu ambalo lipo nyuma ya ukumbi wa Songea Club  hivyo ni lazima uwekwe alama ya kudumu itakayotambulika kiurahisi na kuvuta hisia za mawazo ya watanzania wengi kwenda kupatembelea.

Alisema kuwa mnara huo unatarajiwa kuwa kumbukumbu muhimu na adhimu ya mashujaa wa vita vya majimaji,askari wanaopigana vita vya kagera na kufa kwa ajali njiani kwenye mlima wa Lukumburu wakiwa wanarudi nyumbani baada ya ushindi na  mashijaa waliopigana vita ya pili ya dunia.

Alieleza kuwa eneo hilo ni kumbukumbu muhimu katika historia,utamaduni na utalii ambapo ujenzi wa mnara utakapokamilika utawekwa majina ya mashujaa hao kwenye vibao vya shaba ili watu waweze kusoma na kuwaelewa wapiganaji hao.

Maligissu alibainisha kuwa kutawekwa fensi nzuri fupi na imara itakayowawezesha watu kuingia kwa utaratibu maalumu na kufanya shughuli za utalii na kupata elimu stahiki ya kihistoria na kuhusu uhuru wa mtanzania na mwafrika kwa kutumia vielelezo halisi.

Binafsi nakubariana na wazo la kujenga mnara katika eneo hilo,kwani historia ya mapambano ya kupinga utawala wa wakoloni na uhuru wa nchi yetu haiwezi kukamilika bila kuwataja mashujaa wa vita ya majimaji waliopoteza uhai wao kwa kuitetea nchi na hadhi yao kuanzia Julai 1905 hadi Agosti 1907.

Jina hilo la vita vya majimaji lilitokana na imani ya matumizi ya dawa iliyochanganywa na maji,punje za mahindi na mtama zilizosadikika kuwa zingempa mpiganaji kinga ya kutodhurika kwa shambulio la risasi za Wajerumani chini ya uhamasishaji wa mganga kinjekitile ngwale.

Vita hivyo vilidumu kwa miaka miwili kuanzia 1905 hadi 1907 na waanzilishi wa mwanzo wa vita hivyo walikuwa machifu na Mganga wa jadi katika jamii ya  wangindo na wamatumbi.

Baadaye vuguvugu hilo lilienea kwenye jamii nyingi ikijumuisha jamii za wamatumbi,wangindo,wamwera,wapogoro,wandendeule,wabena,wasangu,wangoni na nyingine,

Inaeleweka wazi kuwa toka mwanzo wakoloni kutoka ujerumani walijawa na shauku ya kunyonya raslimali kutoka makoloni yao ndio maana walilazimisha jamii za watu walioishi katika kuenea waliyoyachukua kuja tawala kwa nguvu,kushiriki katika uanzishaji wa mashamaba  ya mazao waliyoyahitaji katika viwanda vyao huko ulaya.

Vita vilipoanza katika vilima vya matumbi,kaskazini magharibi mwa kilwa julai  1905 na sababu kubwa ilikuwa ni wananchi kupinga vitendo viovu hasa vya kulazimisha kulima mazao ya biashara,kulipa kodi na unyanyasaji mwingine waliofanyiwa na mfumo wa utawala wa wajerumani.

Kwa muda wa miaka miwili wajerumani walishuhudia waafrika wakiwadhihirishia kwamba  dhana waliyokuwa nayo ya kuona Afrika ni bara la giza haikuwa sahihi hata kidogo.

Walilazimishwa kujua kwamba Afrika ina watu wenye dhamira,utashi na uwezo wa kutetea utu, uhuru na heshima yao,jambo lililowalazimisha wajerumani kuongeza wapiganaji kabla ya ushindi ili kukabiliana na mashambulizi ya mashujaa wa Afrika wa kusini  mashariki mwa Tanzania bara.

Wajerumani kwa juhudi kubwa na kwa kutumia bunduki na mbinu nyingine nyingi ikiwemo kuchoma moto mashamba na  maghala ya kuhifadhia chakula ya waafrika ili kudhoofisha uwezo wa kushambuliwa

Baada ya vita kusambaa askari na viongozi 67 walioshiriki vita walikamatwa na kufungwa jela na kuhukumiwa kunyongwa hadi kufa Februari 27 mwaka 1906.

Tarehe hiyo ilikuwa ni siku ya masikitiko makubwa kwa watu wa Ruvuma na Taifa kiujumla kwani watu 67 walinyongwa na kuzikwa katika kabuli moja lililochimbwa na wao wenyewe walipokuwa wafungwa bila kujua kuwa ndilo litatumika kuwazika wenyewe isipokuwa kiongozi wao Nduna Songea Mbano ndiye aliyezikwa kwenye kaburi la peke yake.

Mashujaa 66 walinyongwa na kuzikwa kwenye kaburi moja akiwemo chifu Mputa Gama na wasaidizi wake (nduna) kumi na mbili (12)  akiwemo nduna Songea mbano  ambaye alikuwa maarufu kuliko chifu mputa Gama alinyongwa na kuzikwa katika kaburi lake.

Akizungumzia tukio la kunyongwa mashujaa wa vita hivyo Makamu Mwenyekiti wa Baraza la mila na Desturi la Makumbusho ya Taifa ya Majimaji Songea,Ally Songea Mbano ambaye pia ni Mjukuu wa Nduna Songea Mbano aliyepewa heshima ya jina lake litumike katika kuuita mji wa Songea

Anasema kwa masikitiko kuwa unyongaji ulifanyika kwa awamu tatu yaani Februari 27, machi 20 na Aprili 12,1906 katika eneo la Songea Club lililopo kata ya Mjini Manispaa ya Songea na kwamba siku ya kunyongwa watu wengi walikusanywa na walisimamishwa mahali ambapo waliweza kuwaona wanyongaji na waliokuwa wakinyongwa

Anasema  kuwa ilifanya vile ili kujenga hofu miongoni mwa jamii za waafrika ili kuwa vunja moyo wa ushupavu na ujeuli hasa pale watakapokuwa wanapewa amri mbalimbali za wakoloni wa kijerumani.

Katika eneo ambalo mnara unatarajiwa kujengwa kuna nguzo kubwa mbili zilizosimikwa pande mbili ambazo kwa mujibu wa Mbano,nguzo hizo zilishikilia mnyororo uliofungwa vitanzi vinne na kwamba chini ya nguzo hizo kulikuwa na ubao uliowekwa juu ya nguzo fupi nne.

“Basi waliwafunga wafungwa wa nne toka kwenye mnyororo ule mkubwa na wakasimamishwa juu ya ule ubao uliotegeshwa wakawapachika zile kamba zilizoning’inia kila mmoja na kamba yake huku wakiwa wamefungwa kamba mikono yote miwili ili wasiweze kujimudu kujitikisa na nyuso zao zilikuwa zimefungwa vitambaa nyekundu ili wasiweze kuona” anasema Mbano.

Anasema kuwa walisitiliwa maumbile yao kwa vitambaa vidogo kwenye sehemu zao za siri kabla ya askari kufyatua ubao na ndipo miili ya Mashujaa hao ikabaki ikining’inia kwenye vitanzi mpaka  walipokata roho

Baada ya Mashujaa kukata roho katika mateso makali, wauaji hao waliondoa miili hiyo na kuweka kando kwani walikuwa wakiwanyonga  wanne kwa wakati mmoja ambapo kwa siku ya kwanza Februari 27 walinyongwa watu 40 na  machi 20 walinyongwa watu 26 na Aprili 12 . 1906 alinyongwa Jemedari Nduna Songea Mbano.

Anabainisha kuwa maiti za Mashujaa walionyongwa kwa siku moja zililazwa katika kaburi hilo kubwa kiubavu bila sanda na kufukiwa kidogo ili kutoa nafasi kwa maiti wengine wa siku nyingine kuzikwa na kwamba walioongezeka kunyongwa walilazwa juu ya wale wa kwanza na kufukiwa katika kaburi hilo moja kubwa na kuongeza kuwa kati ya Mashujaa hao kulikuwa na wa imani tofauti  kwani walikuwepo wapagani,wakristo na waislamu.

Anasema kuwa Aprili 12 .1906 Nduna Songea  Mbano alidai na yeye anyongwe kama ndugu zake na wajerumani walimnyonga na kumzika kwenye kaburi la pekee yake ambalo lipo kwenye eneo la Makumbusho ya Taifa ya  majimaji Songea katika eneo la  Mahenge,Manispaa ya Songea.

Anasema hiyo ilitokea kwa sababu Nduna Songea Mbano alikuwa ndiye jemedali mkuu wa jeshi la wangoni na alikuwa hodari asiyeogopa  lolote kwa hiyo wajerumani walitaka abakie ili wamtumie kwa malengo yao jambo ambalo hawakufanikiwa.

Mzee Mbano anasema kuwa Mashujaa walionyongwa  vitanzini walikuwa 67, waliokufa gerezani kabla ya kunyongwa walikuwa wawili na waliopigwa risasi ili kuonyesha nguvu ya risasi walikuwa watano na kufanya jumla ya mashujaa 74 waliouwawa kikatili.

Ingawa inakadiliwa kuwa watu 75,000 walipoteza maisha yao ukanda wa kusini mwa Tanznaia baada ya vita ambapo katika eneo la Ruvuma inakadiriwa kuwa zaidi ya watu 1000 walipoteza maisha yao.

Ni wazi kuwa vita vya Majimaji vilikuwa na madhara makubwa ya kiuchumi na kijamii kwa watu wa mikoa ya kusini mashariki mwa Tanzania bara kwani kulitokea vifo vilivyosababishwa na  mapigano,upungufu wa chakula, watu kushindwa kufanya kazi kutokana na kukimbia makazi yao, ulimwaji wa mashamba na maghala ya kuhifadhia chakula uliofanywa na wajerumani ili kudhoofisha uwezo wa kushambuliwa wajerumani nao walipata madhala  kwani wapiganaji wao waliuawa na wapiganaji wazalendo na walilazimika kuongeza wapiganaji kukabiliana na mashambulizi kabla ya ushindi.

Vita vya Majimaji ni kumbukumbu muhimu katika historia ya Tanzania na kwamba Mashujaa wa vita hivyo wanastahili kuheshimika kwa kuwa walitetea utu, heshima na haki za binadamu na kielelezo halisi cha watanzania kukataa kutawaliwa na wakoloni kwani machifu na wapiganaji wengine wa vita hivyo Nduna songea mbano na wenzake wanastahili kukumbukwa.

Pamoja na jamii nyingine zilizopambana na wakoloni wakiongozwa na  machifu kama vile Mkwawa wa wahehe, Mangi sina wa Moshi, Abushiri na Bwana heri wa Pangani na viongozi waliongoza harakati za kudai uhuru kutoka kwa  waingereza

Mashujaa wa harakati za kudai uhuru  ni wale wote walioshiriki bila kuyumbishwa na hila za wakoloni kuhamamisha wananchi kuondoa utawala wa kigeni mpaka Taifa letu lilipopata uhuru mwaka 1961 Tanzania bara,na mapinduzi ya Zanzibar yaliyoondoa utawala wa kisultani Tanzanaia visiwani  mwaka 1964.

Orodha ya Mashujaa wa vita vya Majimaji ni kubwa ambapo baadhi ya majina yao yamehifadhiwa katika orodha ya walionyongwa baada ya kukamatwa na kufungwa na wajerumani.

Miaka zaidi ya mia moja  baada ya vita vya Majimaji watanzania wamejifunza mengi na kujenga upendo miongoni mwao na mahusiano mazuri na mataifa mengine ingawa ni wazi kuwa machungu ya vita hivyo bado hayajasahaulika

Lakini utamaduni mpya umejengeka miongoni mwa watanzania wa kushirikiana na kuheshimiana bila kujali kabila,rangi na asili ya mtu anakotoka huu ni ukomavu mkubwa uliojengwa na Mashujaa wetu hivyo ujenzi wa mnara wa Mashujaa hao ni muhimu kwa kizazi kilichopo na kijacho kwani ni kielelezo muhimu cha kuwaenzi, kuwaheshimu na kuwathamini wazee hao

Mwandishi wa Makala haya
Anapatikana simu 0755-335051
Barua pepe;stephano12mango@yahoo.com.

No comments:

Post a Comment