UTASHI WA KISIASA UNAHITAJIKA KUBORESHA AFYA YA UZAZI NYASA
Na Stephano Mango,Nyasa
SEKTA ya afya katika nchi yoyote duniani ina umuhimu mkubwa sana katika kuleta ustawi wa jamii na kwamba ili jamii iweze kujitegemea kielimu,kisiasa,kiuchumi ni lazima iwe na afya bora itakayowezesha nchi kupiga hatua kusudiwa
Kwa kutambua hilo hivi karibuni nilikuwa katika ziara kwenye wilaya mpya ya Nyasa Mkoani Ruvuma katika shughuli za kiuandishi kufuatilia hali ya huduma ya afya ya uzazi kwa wakazi wa wilaya hiyo iliyopo mwambao mwa Ziwa Nyasa
Nilibahatika kufika huko kwa ufadhiri wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP)na kuweza kufanikiwa kutembelea kata sita za Lituhi,Mbaha,Kihagara,Mbambabay,Chiwanda na Kilosa katika wilaya hiyo
Katika shughuli zangu za uandishi nilibaini mambo kadhaa yanayowakumba akina mama wajawazito kabla na baada ya kujifungua wakati wa kwenda katika vituo vya afya na Zahanati kupata huduma ya afya ya uzazi na mtoto
Miongoni mwa mambo hayo ni umbali mrefu kutoka kwenye makazi hadi kufika katika vituo vya afya ili kuweza kupata huduma ya kliniki kwani akina mama wengi wajawazito wamekuwa wakitembea umbali mrefu pekee yao bila hata kusindikizwa na wenza wao
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kutoka katika vijiji vya
Chimate,Mtupale,Chinula,Ndengele na N’gombo umebaini kuwa akina mama wengi wajawazito wamekuwa wakikumbana na kero kubwa ya usafiri wa kutoka kwenye vijiji wanavyoishi hadi kwenye vituo vya afya kufuata huduma za kliniki ya mama na mtoto
Imebainika kuwa akina mama hao wajawazito wamekuwa wakichelewa kufika katika vituo vya afya na wakati mwingine kukosa kabisa huduma muhimu ya afya ya mama na mtoto kutokana na adha kubwa ya usafiri jambo linalopelekea kudhoofika kwa afya zao kabla na baada ya kujifungua
Baadhi yao kutoka katika Vijiji vya Mtupale,Mtipwili,Chiulu,Kwambe,Mbaha na Kingirikiti wakizungumza na gazeti hili walisema kuwa kutokana na umbali mrefu uliopo toka wanakoishi hadi kwenye vituo vya afya wamekuwa wakishindwa kuhudhulia kliniki kabla na baada ya kujifungua kwani wakina mama hao wamekuwa wakilazimika kujifungulia majumbani kwa sababu ya kukosa nauli na wakati mwingine usafiri wa kuwafikisha katika vituo hivyo
Walisema kuwa hali hiyo licha ya kuwa ni hatari kwa afya zao lakini wamekuwa wakilazimika kufanya hivyo kutokana na mazingira magumu waliyonayo katika maeneo wanayoishi na kwamba Zahanati nyingi zilizopo kwenye maeneo jilani wanayoishi zimekuwa zikikosa dawa,wataalamu pamoja na vifaa tiba
Uchunguzi huo umebaini kuwa Wilaya mpya ya Nyasa ina vituo vya Afya Vitatu ambavyo ni Lituhi kinachomilikiwa na Kanisa Katoliki Jimbo la Mbinga,Liparamba na Mbambabay pamoja na Hospitali ya Liuli ambayo inamilikiwa na kanisa la Anglikana Dayosisi ya Ruvuma pamoja na Zahanati nyingi ambazo huduma yake ni duni
Imebainika kuwa wakina mama wajawazito kutoka kijiji cha Mango hadi kituo cha afya cha Mbambabay wamekuwa wakitembea kwa miguu umbali wa kilometa 43 na wakati mwingine wamekuwa wakitumia usafiri wa Yeboyebo(pikipiki) kwa nauli ya shilingi elfu 9,500 ambako kwa gari ni shilingi elfu 3000
Aidha imebainika kuwa gharama za matibabu ni kikwazo kwa akinamama hao kwani wamekuwa wakichangia huduma za kliniki na matibabu kati ya shilingi 2000 na shilingi 6000 kila wanapohitaji kupata huduma kinyume na sera ya taifa ya matibabu bure kwa wajawazito na watoto chini ya miaka mitano
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili katika kata ya Lundo akina mama hao walisema kuwa Serikali imekuwa ikisema akina mama wajawazito na watoto chini ya miaka mitano wanatakiwa kupata huduma ya afya bila kuchangia malipo lakini wao wamekuwa wakichangia fedha nyingi
Kutokana na kuchangia gharama hizo ambazo kwao zimekuwa kero kubwa wamekuwa wakilazimika kwenda kliniki wanapokaribia kujifungua tu ili kuweza kukwepa gharama zinazotozwa mara wanapofika katika Zahanati na vituo hivyo kutokana na ugumu wa maisha
Walisema kuwa katika kata hiyo kuna Zahanati ya Lundo ambayo mara nyingi imekuwa ikikosa dawa muhimu za wajawazito na wahudumu wake wamekuwa na lugha chafu kwa wagonjwa hali inayopelekea akina mama wengi kutohudhulia Kliniki kwa kuhofiwa kutukanwa na kupoteza muda wa kufanya kazi zao za kujitafutia ridhiki
Mary Haule mkazi wa kata hiyo ambaye anaujauzito wa miezi saba alisema kuwa kutokana na hali hiyo amekuwa akienda kupata matibabu katika Kituo cha Afya cha Mbambabay kwa kuhofia usalama wake wakati wa kujifungua
Haule alisema kuwa wajawazito wengi wamekuwa wakinyanyaswa sana pindi wanapofika katika Zahanati kwa ajili ya kupata huduma za matibabu jambo ambalo linaonyesha uzalilishaji wa hali ya juu kwa wanawake
Uchunguzi uliofanya na Gazeti hili umebaini kuwa Zahanati nyingi za Mwambao mwa Ziwa Nyasa zimekuwa zikikosa dawa muhimu kwa ajili ya wajawazito na watoto chini ya miaka mitano kutokana na mgawanyo usio wa uwiano unaotolewa na Bohari ya Madawa Nchini(MSD)
Aidha kutokana na ukosefu huo wa dawa uchunguzi umebaini kuwa wahudumu wa Zahanati hizo wamekuwa wakiwauzia dawa na vifaa tiba wajawazito kwa bei kubwa hali inayopelekea unyanyasaji mkubwa kwa akina mama hao ambao wanatoka umbali mrefu kwa ajili ya kupata matibabu stahiki
Gazeti hili lilishuhudia baadhi ya wajawazito 3 katika Kituo cha Afya cha Mbambabay wakitokea Kata ya Tumbi umbali wa kilometa 43 ambapo wamekuwa wakitembea kwa miguu na wakati mwingine kwa pikipiki kwa kutozwa nauli kubwa kwenda kuhudhulia Kliniki
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Chiwanda Oldo Mwisho aliliambia gazeti hili kuwa kufuatia adha wanazopata wakina mama wajawazito alisema kuwa Halmashauri yake inazitambua adha hizo na kwamba sera ya afya ya Serikali imetamka wazi kuwa kila kata ni lazima ijenge kituo cha afya ili kukabiliana na adha hizo na kila kijiji ijenge Zahanati
Mwisho alisema kuwa kutokana na hali wananchi wamekuwa wakihimizwa ujenzi wa vituo vya afya kwenye kata zao ambapo changamoto kubwa inayoikabili Serikali ni ubovu wa miundombinu, upungufu wa wataalamu wa afya,dawa na vifaa tiba
Akizungumza na gazeti hili Mbunge wa Jimbo la Mbinga Magharibi Kapteini John Komba alisema kuwa Wilaya ya Mbinga ina eneo kubwa la kiutawala hivyo ilikuwa imezidiwa uwezo wake wa kutoa huduma kwa jamii kwani ilikuwa ina hudumia wakazi wa majimbo mawili ya uchaguzi la Mbinga Magharibi na Mbinga Mashariki
Komba alisema kuwa Serikali kuu kwa kutambua ukubwa wa eneo hilo imeamua kuyagawa majimbo hayo katika Wilaya na kupata Wilaya ya Mbinga na Wilaya mpya ya Nyasa ambayo inaanza rasmi katika kipindi hiki cha bajeti ya mwaka wa 2011/2012 hivyo mara itakapoanza itapunguza adha hizo za wajawazito kwa kiasi kikubwa
Alisema kuwa mara nyingi amekuwa akipigania ustawi wa afya za akina mama wajawazito anapopata wasaa wa kuchangia bungeni akiwa mwanasiasa aliyepewa dhamana na wananchi katika kushirikiana nao kujiletea maendeleo kusudiwa katika jimbo hilo
Mwandishi wa makala
Anapatikana kwa 0755-335051
Barua pepe;stephano12mango@yahoo.com
No comments:
Post a Comment