LUGHA CHAFU,UKOSEFU WA DAWA NI TATIZO KWA WAJAWAZITO NYASA
Na Stephano Mango,Nyasa
SEKTA ya afya ni moja ya eneo nyeti katika maisha ya mwanadamu yoyote yule duniani lakini imekuwa ikilalamikiwa kwa kiasi kikubwa na wadau wa sekta hiyo kutokana na huduma mbovu na zenye kejeli kwa akina mama wajawazito
Uchunguzi uliofanywa na waandishi wa habari kwa ufadhiri wa Mtandao wa Jinsia Tanzania(TGNP)hivi karibuni kwenye Zahanati na vituo vya afya vilivyopo mwambao mwa Ziwa Nyasa umebaini kuwa akina mama hao wamekuwa wakipewa lugha chafu na zilizojaa kejeli pindi wanapofika katika Zahanati na vituo vya afya kabla na baada ya kujifungua
Imebainika kuwa watumishi katika sekta ya afya katika kituo cha afya cha Mbambabay wamekuwa wakiwatolea lugha zilizokosa staha akina mama wajawazito kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kuchelewa kufika kuanza kliniki na nyinginezo
Kutokana na hali hiyo imebainika kuwa akina mama wengi wajawazito wamekuwa wakishindwa kuendelea kuhudhulia kliniki kwa kuhofia lugha chafu zinazotolewa na wahudumu wa sekta ya afya na badala yake wamekuwa wakijifungua kwa wakunga wajadi
Wakizungumza kwa uchungu na hofu ya kukutwa na wahudumu wa afya katika kituo hicho baadhi ya akina mama wajawazito walisema kuwa wanapofika katika kituo cha afya wanakaa muda mrefu bila kusikilizwa na kupatiwa huduma ya afya
Annet Koleka mkazi wa Ndengere akizungumza na gazeti hili alisema kuwa licha ya kuwahi katika kituo cha afya kwa ajili ya kupatiwa matibabu wamekuwa wakikaa kati ya masaa manne hadi saba wakisubiri kupata huduma hiyo
Koleka alisema kuwa wahudumu wa afya katika kituo hicho wamekuwa wakiwadharau sana kwani muda mrefu wamekuwa wakipanga foleni kwa ajili ya kupata huduma na wakati mwingine wanaambiwa kuwa idadi yao inapaswa iongezeke ndipo waweze kutoa huduma kwa madai kuwa hawawezi kuwahudumia watu wachache jambo ambalo linawashangaza sana
Uchunguzi umebaini kuwa akina mama hao wamekuwa wakilipia huduma ya uzazi na mtoto bila mpangilio maalum wa bei kwani imekuwa ikipangwa kilanguzi na wahudumu wa afya na kwamba mara chache tena kwa kubahatisha wamekuwa wakipewa bure dawa za minyoo na wakati mwingine dawa za malaria
Alisema kuwa usafiri umekuwa ni wa tabu sana na kwamba wakati mwingine unapopatika kunakuwa siyo siku ya kliniki kwa wakazi wa eneo fulani na kuendelea kuwa na adha kubwa kwa akina mama hao kuwahi kliniki siku walizopangiwa
Imebainika kuwa kutoka na kero hizo akina mama hao wamekuwa wakilazimika kukodi pikipiki wakiwa wajawazito wawili wenye zamu moja ya kwenda kupima kliniki ili waweze kuhimili kuchangiana gharama za usafiri
Kutokana na adha mbalimbali wanazozipata akina mama hao wamesema kuwa ni vema wakaendelea kujifungulia kwa wakunga wajadi ili kuweza kukwepa kero hizo ingawa wanakili wazi kuwa kujifungulia kwa wakunga hao kunaweza kuhatarisha afya zao
Aidha uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini wazi kuwa wanaume wengi wilayani humo wamekuwa wakiwaacha wake zao ambao wajawazito wakitembea umbali mrefu kwenda kufuata huduma za afya pekee yao bila kuwasindikiza hali ambayo ina hatarisha afya ya mama mjamzito na mtoto aliyetumboni
Agnes Katuli mkazi wa Ngingama alisema kuwa katika kituo cha afya cha Lituhi wanakutana na changamoto ya kufuatana na wenza wao kwenda kliniki ili kupata elimu stahiki ya afya ya uzazi kwani wenza wao wamekuwa wakikaidi wito wa wahudumu wa afya wanapo takiwa kufika katika vituo vy afya
Imebainika kuwa wanaume wengi wa maeneo hayo wameshindwa kushirikiana na wenza wao ili kuhakikisha mama anakuwa na afya njema wakati wa ujauzito wakati wa kujifungua na baada ya kujifungua ili kuweza kukomesha vifo vinavyotokana na uzazi
Wakizungumza na Gazeti hili katika Kituo cha Afya cha Lituhi akina mama wajawazito waliofika kituoni hapo kuhudhuria kliniki walisema kuwa wamekuwa wakitembea umbali mrefu pekee yao bila kuwa na wenza wao hadi kwenye kituo hicho cha afya
Veronika Rohomoja aliliambia gazeti hili kuwa amekuwa akitembea kwa miguu polini zaidi ya kilometa 5 kutoka katika kata ya Ngingama hadi kituoni hapo na kwamba anapokuwa amechoka hupumzika chini ya mti na kisha kuendelea na safari yake
“Hii ni mimba ya uzao wa tatu na inamiezi 8 nimekuwa nikija kituo cha afya pekee yangu ambapo mwenza wangu anakuwa kwenye shughuli za uzalishaji mali na kwamba tumezoea kutembea polini pekee yetu bila kuwa na msaada wa mtu yoyote na wakati mwingine tunakuwa akina mama wajawazito wawili kutoka kwenye eneo moja”alisema Rohomoja
Uchunguzi huo umebaini kuwa wanaume wengi wamekosa elimu ya afya ya uzazi na mtoto na kwamba wamekuwa hawatambui kuwa wao ndio wadau muhimu katika kuhakikisha mama mjamzito anakuwa na afya njema muda wote wakati wa ujauzito,kujifungua na baada ya kujifungua
Akizungumza na gazeti hili Emilia Chawala (38) mkazi wa kijiji cha Mango ambaye anaujauzito wa miezi saba ikiwa ni mzao wake wa nne alisema kuwa wamekuwa wakikutana na changamoto ya dawa na vifaa tiba mara wanapofika katika zahanati na vituo vya afya
Chawala alisema wana kutana na changamoto ya vifaa hivyo ambavyo ni muhimu kwa ajili ya huduma ya kliniki hali ambayo inawalazimu kwenda kununua kwenye maduka ya dawa muhimu kwa bei kubwa
Akizungumza na gazeti hili Daktari Mfawidhi wa Kituo cha Afya cha Lituhi Dkt Martin Ndunguru alisema kuwa wanaume wamekuwa mara nyingi hawataki kuwasindikiza wenza wao kliniki ili waweze kujua matatizo wanayowakabili mama na mtoto kutoka na mazingira magumu ya maisha,mfumo dume na mila na tamaduni za eneo hilo
Ndunguru alisema kuwa licha ya wanaume kuwa na shughuli nyingi za kutafuta ridhiki,wamekuwa wakiendelea kuwaelimisha akina mama mbinu za kuwavuta wenza wao ili waje kupata elimu muhimu ya huduma ya afya ya uzazi na mtoto ili kuweza kunusuru vifo vitokanavyo na masuala ya uzazi
Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya cha Mbambabay Dkt Wenselausy Soky alisema kuwa kituo chake kinahudumia watu wengi kuliko uwezo wake hali inayopelekea wengine kukosa dawa muhimu kwa ajili ya maradhi yao
Dkt Soky alisema kuwa kituo hicho kinahudumia wagonjwa kutoka katika maeneo mengi na wale ambao wamepewa rufaa kutoka katika Zahanati 11 za Mwambao mwa ziwa Nyasa na kwamba wajawazito wamekuwa wakinunua dawa na vifaa tiba katika maduka ya dawa baridi na sio kuwa wahudumu wa afya ndio wamekuwa wakiwauzia akina mama hao kwa bei kubwa
Alisema kuwa wahudumu wa afya katika kituo hicho wanakutana na hangamoto nyingi kutoka kwa wagonjwa ikiwemo ya familia nyingi kuchelewa kutoa maamuzi ya kutafuta huduma kwenye kituo cha afya kutoka na uelewa mdogo wa kufahamu dalili za hatari kwa mama mjamzito
Alieleza kuwa akina mama hao mara wanapofika kuanza kliniki wamekuwa wakiambiwa waje na waume zao ili waweze kupata vipimo vya maambukizi ya magonjwa mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupatiwa elimu ya afya ya uzazi na mtoto hali inayosababisha kutokuelewana na kuhisi kuwa wametukanwa kwa sababu za tamaduni na mila zao
Alileza zaidi kuwa mara nyingi kituo chake kimekuwa kikikosa dawa muhimu na vifaa tiba kwa ajili ya dharura kwa mama mjamzito kwani huduma za msingi kama vile drip,dawa kwa ajili ya kukabiliana na uambukizi,kifafa cha mimba,kumsafisha mama ambaye mimba yake imetoka,kutoa dawa ya kuzuia damu kuendelea kutoka,kufanya vacuum imekuwa duni kutokana na ukosefu wa vifaa tiba na dawa muhimu kwa ajili ya huduma hizo
Mwandishi wa Makala haya
Anapatika kwa 0755-335051
Baruapepe;stephano12mango@yahoo.com
MWISHO
No comments:
Post a Comment