WAJAWAZITO WALIA NA UMBALI MREFU KWENDA VITUO VYA AFYA
Na Stephano Mango,Songea
WANAWAKE wajawazito wa Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma wanakabiliwa na umbali mrefu kutoka katika maeneo wanayoishi kwenda katika Vituo vya Afya Mbambabay,Liparamba na Lituhi kwa ajili ya kupata huduma za afya kabla na baada ya kujifungua
Uchunguzi uliofanya na gazeti hili kutoka katika vijiji vya
Chimate,Mtupale,Chinula,Ndengele na N’gombo umebaini kuwa akina mama wengi wajawazito wamekuwa wakikumbana na kero kubwa ya usafiri wa kutoka kwenye vijiji wanavyoishi hadi kwenye vituo vya afya kufuata huduma za kliniki ya mama na mtoto
Imebainika kuwa akina mama hao wajawazito wamekuwa wakichelewa kufika katika vituo vya afya na wakati mwingine kukosa kabisa huduma muhimu ya afya ya mama na mtoto kutokana na adha kubwa ya usafiri jambo linalopelekea kudhoofika kwa afya zao kabla na baada ya kujifungua
Baadhi ya wakina mama wajawazito kutoka katika Vijiji vya Mtupale,Mtipwili,Chiulu,Kwambe,Mbaha na Kingirikiti wakizungumza na gazeti hili walisema kuwa kutokana na umbali mrefu uliopo toka wanakoishi hadi kwenye vituo vya afya wamekuwa wakishindwa kuhudhulia kliniki kabla na baada ya kujifungua kwani wakina mama hao wamekuwa wakilazimika kujifungulia majumbani kwa sababu ya kukoasa nauli na wakati mwingine usafiri wa kuwafikisha katika vituo hivyo
Walisema kuwa hali hiyo licha ya kuwa ni hatari kwa afya zao lakini wamekuwa wakilazimika kufanya hivyo kutokana na mazingira magumu waliyonayo katika maeneo wanayoishi na kwamba Zahanati nyingi zilizopo kwenye maeneo jilani wanayoishi zimekuwa zikikosa dawa,wataalamu pamoja na vifaa tiba
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa Wilaya mpya ya Nyasa ina vituo vya Afya Vitatu ambavyo ni Lituhi kinachomilikiwa na Kanisa Katoliki Jimbo la Mbinga,Liparamba na Mbambabay pamoja na Hospitali Liuli ambayo inamilikiwa na kanisa la Anglikana Dayosisi ya Ruvuma pamoja na Zahanati nyingi ambazo huduma yake ni duni
Imebainika kuwa wakina mama wajawazito kutoka kijiji cha Mango hadi kituo cha afya cha Mbambabay wamekuwa wakitembea kwa miguu umbali wa kilometa 43 na wakati mwingine wamekuwa wakitumia usafiri wa Yeboyebo(pikipiki) kwa nauli ya shilingi elfu 9,500 ambako kwa gari ni shilingi elfu 3000
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Chiwanda Oldo Mwisho aliliambia gazeti hili kuwa kufuatia adha wanazopata wakina mama wajawazito alisema kuwa sera ya afya ya Serikali imetamka wazi kuwa kila kata ni lazima kijengwe kituo cha afya ili kukabiliana na adha hizo na kila kijiji iwepo Zahanati
Mwisho alisema kuwa kutokana na hali wananchi wamekuwa wakihimizwa ujenzi wa vituo vya afya kwenye kata zao ambapo changamoto kubwa inayoikabili Serikali ni ubovu wa miundombinu, upungufu wa wataalamu wa afya,dawa na vifaa tiba
Akizungumza na gazeti hili Mbunge wa Jimbo la Mbinga Magharibi Kapteini John Komba alisema kuwa Wilaya ya Mbinga ina eneo kubwa la kiutawala hivyo ilikuwa imezidiwa uwezo wake wa kutoa huduma kwa jamii kwani ilikuwa ina hudumia wakazi wa majimbo mawili ya uchaguzi la Mbinga Magharibi na Mbinga Mashariki
Komba alisema kuwa Serikali kuu kwa kutambua ukubwa wa eneo hilo imeamua kuyagawa majimbo hayo katika Wilaya na kupata Wilaya ya Mbinga na Wilaya mpya ya Nyasa ambayo inaanza rasmi katika kipindi hiki cha bajeti ya mwaka wa 2011/2012 hivyo mara itakapoanza itapunguza adha hizo za wajawazito kwa kiasi kikubwa
MWISHO
No comments:
Post a Comment