Na Joseph Mwambije,Songea
KAIMU Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Nyanda za juu kusini Susan Magani amewataka wahitimu wa kozi ya CBET kutokuwa na muda wa mchezo kwenye kazi yao ya Ualimu wa Ufundi kwa kuwa inamjengea mtu ujuzi katika maisha yake
Aliitoa kauli hiyo hivi karibuni wakati akifunga kozi ya kufundisha kwa kutumia mfumo mpya wa Compitance based education and training(CBET) iliyofanyika Peramiho na kushirikisha walimu 36 wa vyuo vya ufundi toka Mikoa ya Ruvuma na Iringa.
Magani alisema kuwa kazi hiyo ni kazi nzito na muhimu kama zilivyo kazi nyingine hivyo ni vyema walimu wanaofundisha vyuo vya ufundi wakatambua jukumu lao la kuwajengea watu ujuzi wa kwenda kujitegemea.
‘Walimu mnaofundisha vyuo vya ufundi mnapaswa kujijua kuwa nyinyi ni watu muhimu mnaohusika katika kumjengea mtu ujuzi wa kujitafutia maisha hivyo mnapaswa kujiendeleza kielimu kwa kuwa kuna mabadiliko ya kiuchumi’alisema Magani.
Pia aliwataka walimu wa vyuo vya ufundi kuwa wajasiriamali ili waweze kupambana na makali ya maisha ya sasa ambayo yanaendelea kupanda kila siku na kuwa wajasiriamali wa vitendo na kwamba kwa hali hiyo hata wanafunzi wao wanaweza kuiga ujasiriamali toka kwao.
Alisema kuwa walimu hao waliohitimu mafunzo ya kufundisha kwa kutumia mfumo huo mpya watakuwa na nafasi nzuri ya kuwaeleza wanafunzi watakaokuja kusoma kwenye vyuo vyao.
Akijibu risala ya wahitimu hao ilyotaka walimu wa ufundi toka taasisi za dini na binafsi kuongezewa mishahara,walimu kupata mafuzo ya kopyuta na kiingereza na kufungua maduka ya vitabu vya ufundi alisema maombi yao yatafanyiwa kazi.
Kaimu Mkurugenzi huyo wa VETA alisema suala la upatikanaji wa vitabu wataliingiza kwenye mpango kazi wa miaka mitano na maoni yao yatapelekwa kwenye ngazi za juu kwa ajili ya hatua zaidi
MWISHO
No comments:
Post a Comment