Katibu wa Chama Cha Walimu (CWT)Mkoa wa Ruvuma Luya Ngonyani
Na, Augustino Chindiye Tunduru
WATU watano wanashikiriwa na jeshi la Polisi Wilayani Tunduru Mkoani Ruvuma kwa tuhuma za kufanya majaribio ya kutaka kuwaua Walimu wawili wa Shule ya Msingi Ruanda iliyopo katika Tarafa ya Nakapanya Wilayani humo.
Taarifa za tukio hilo zinaeleza kuwa Walimu walionusulika katika tukio hilo ni Mwl. Ezakieli Ngaleka na Mwl.Emmanuel Hyao wanaodaiwa kuwa na urafiki wa kimapenzi na mke wa mtu.
Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Ruvuma Michael Kamuhanda amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Ally Brashi (19) ambaye pamoja na mambo mengine amekiri kuhusika katika tukio hilo akidai kuwa alitekeleza tukio hilo kwa nia ya kutaka kumuua Mwl. Naleka akiwa anamtuhumu kuwa na mahusiano ya kimapenzi na Mkewe.
Wangine wanaoshikiriwa kutokana na tukio hilo ni pamoja na Mustafa Mariki (19), Mahamudu Juao (21), James Mathayo (20) na Hamisi Athuman (19) wote wakiwa ni wakazi wa kijiji hicho.
Akizungumzia tukio hilo Kaimu afisa elimu wa shule za Msingi wa Wilaya ya Tunduru Mwl.Fravia Nchimbi alisema kuwa kufuatia tukio hilo idara yake imeamua kuwabadirishia vituo vya kazi ili kuwahakikishia usalama wa maisha yao.
Nae Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru Mwl. Rashid Mandoa alipotakiwa kuzungumzia tukio hilo alisema kuwa ofisi yake imewaagiza viongozi wa serikali ya kijiji hicho kufanya mazungumzo na wananchi wao ili waachane na matukio ya aina hiyo.
Kuhusu nyumba iliyoteketea na moto huo alisema kuwa siyo mali ya Halmashauri hiyo bali ilikuwa ikimirikiwa na mkazi wa kijiji hicho Fikirini Brashi ambaye alikuwa na mkataba wa kuwapangisha walimu hao na kwamba baada ya tukio hilo kamati ya shule na uongozi wa kijiji ndio utakaowajibika kumjengea nyumba nyingine.
Wakiongea kwa nyakati tofauti walimu hao walimshukuru mungu kwa kuwaokoa na tukio hilo pamoja na uongozi wa halmashauri hiyo ambao umekubali kuwagharamia kwa kuwanunulia vifaa na kuwafidia mali zilizo teketea katika tukio hilo zinazo kadiliwa kuwa na thamani ya zaidi ya shilingi milioni moja.
Mwisho
No comments:
Post a Comment