Kamati hiyo ikikagua ujenzi wa vyoo vya Wasichana Shule ya Sekondari Msamala vilivyogharimu sh 9,610,000.00 |
Jengo la Ofisi ya Kata ya Mletele ambalo kumalizia ukarabati wake umegharimu sh,5,600,000.00 |
Hapa sasa ni ukaguzi wa ujenzi wa vyoo vya Zahanati ya Mletele vilivyogharimu sh 9,314,663.00 |
Ukaguzi wa ujenzi wa kudhibiti kasi ya maji yanayoingia kwenye Intake ya Ruhila |
Na Mwandishi Wetu,Songea
KAMATI ya Siasa ya Halmashauri kuu ya Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Songea Mjini imekagua miradi iliyotekelezwa na Halmashauri ya Manispaa ya Songea katika kipindi cha Januari hadi juni ili kujionea hali halisi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa wananchi wa Wilaya hiyo
Akizungumza na Waandishi wa Habari ofisini kwake jana Katibu wa Chama cha Mapinduzi (Ccm) Wilaya ya Songea Mjini Alfonce Siwale alisema kuwa miradi 20 iliyotembelea na kamati hiyo ni pamoja na ujenzi wa choo katika Shule ya Sekondari Msamala,kitengo cha ufundi Shule ya msingi mfaranyaki, upimaji wa viwanja 347 eneo la Namanyigu, upimaji wa viwanja eneo la Mkuzo, Sekondari ya Mkuzo
Siwale alisema kuwa miradi mingine ni ya ukamilishaji wa Ofisi ya Kata ya Mletele,ujenzi wa vyoo Zahanati ya Mletele,ukarabati wa Zahanati ya Liumbu pamoja na ujenzi wa Tanuri la kuchomea takataka,ujenzi wa vyanzo vya maji Luhila,ujenzi wa vyoo vya Walimu,Utengenezaji wa viti na meza za Wanafunzi shule ya Sekondari Mazoezi na mradi wa ng’ombe katika shule hiyo
Miradi mingine ni ya ujenzi wa Zahanati Mateka’A’,Barabara ya Ruvuma –Kipera,Barabara ya Ruvuma-Mbulani,Barabara ya Mbulani-Shule ya Msingi Misufini,kivuko cha Matarawe-Mfaranyaki,Barabara ya Mwembechai-Kadogoo,ujenzi wa vyoo Shule ya Msingi Ukombozi,ujenzi wa Zahanati ya Nambarapi na ujenzi wa jingo la utawala Subira Sekondari
Siwale alifafanua kuwa Ccm katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana iliingia mkataba wa kuwatumikia wananchi kwa miaka mitano hivyo ukaguzi wa miradi hiyo inayotekelezwa na Halmashauri ya Manispaa ya Songea ni jambo jema kwani chama kinajiridhisha na utekelezaji wa ilani yake ili kufuta malalamiko ya wananchi wanyonge kuhusu chama chao kufumbia macho vitendo viovu vinavyofanywa na Serikali
Alieleza kuwa katika miradi hiyo iliyotembelewa na Kamati hiyo kuna mapungufu mengi yamebainika ambayo yasiporekebishwa huenda ukamilikaji wake usiwe wa kuridhisha pamoja na fedha nyingi kutumika kat ika miradi hiyo
Alisema kuwa mapungufu yaliyoonekana yatawasilishwa kwenye mkutano mkuu wa Halmashauri kuu wa chama ili kuweza kuwapa fursa wajumbe kujadili kwa kina na kisha mapendekezo yatakayotolewa kwenye mkutano huo yatawasilishwa kwa Mkuu wa Wilaya ya Songea Thomas Oley Sabaya na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea Charles Mhagama kwa utekelezaji zaidi kwani wao ni wawakilishi wa chama Serikalini
Mwisho
No comments:
Post a Comment