Na Thomas Lipuka,Songea.
MKUU wa mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu amewaagiza waandishi wa habari ambao hawajajiunga na chama cha waandishi wa habari mkoani humo RPC kujiunga mara moja ili kuwa na jukwaa la kuzungumzia matatizo yanayowakabili na kukuza taaluma yao.
Akifungua mkutano wa wadau wa habari uliyoandaliwa na RPC na kufanyika hivi karibuni kwenye ukumbi wa Chama Cha Walimu Tanzania CWT mkoa wa Ruvuma
Mwambungu alisisitiza kuwa mwandishi wa habari ambaye hajajiunga na chama cha waandishi wa habari katika mkoa husika anajichelewesha katika kujenga umoja wa taaluma na ameshindwa kujitendea haki yeye mwenyewe.
Mwambungu alifafanua kuwa kazi ya uandishi wa habari ni ya kitaaluma kama zilivyo taaluma nyingine hivyo suala la maadili kwa wanahabari sharti lizingatiwe wakati wote mwandishi anapofanya kazi yake.
“Maadili ya habari ndiyo yanayoongoza ,taaluma ya habari,maadili pia yanaongoza taaluma nyingine ,kwa mfano daktari hawezi kutoa siri ya mgonjwa kwa kusema mgonjwa wako atakufa leo au kesho’’,alisisitiza
Amewaasa waandishi wa habari kuacha tabia ya kuhatamia au kuficha habari ambazo wananchi wangezipata,na kwamba habari hiyo inaweza kutafuta mkondo mwingine wa kuwafikia wananchi.
Mwambungu aliwaagiza viongozi wa RPC kuweka vigezo vya kutambua nani aitwe mwandishi wa habari pamoja na sifa zake zikiwemo kiwango cha taaluma au elimu ya weledi huo.
Mwisho
No comments:
Post a Comment