Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma Michael Kamhanda
Na Gideon Mwakanosya,Songea
BAKARI Hassani ( 30) Maarufu kwa jina la Namopwe Mkazi wa Kitongoji cha Moponi mashambani kilichopo katika Kijiji cha Nakapanya Wilayani Tunduru Mkoani Ruvuma amekutwa akiwa amekufa huku akiwa amening’inia kwenye tawi la mti mrefu baada ya kujinyonga kwa kutumia kamba ya katani.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma Michael Kamuhanda amesema kuwa tukio hilo lilitokea novemba 5 mwaka huu majira ya saa 7 mchana huko katika Kitongoji cha Moponi mashambani kilichopo katika Kijiji cha Nakapanya.
Amesema kuwa inadaiwa siku hiyo ya tukio majira ya saa za mchana Wananchi waliokuwa wakipita kwenye eneo la tukio walishtuka kuona mtu akining’inia kwenye mti mrefu ambao upo kandokando ya barabara na baadaye wananchi hao walipiga kelele kwa ishara ya kuomba msaada na muda mfupi tu watu walifika kwenye eneo hilo ukiwemo uongozi wa Serikali ya Kijiji cha Nakapanya .
Ameeleza zaidi kuwa baadaye uongozi wa Serikali ya Kijiji hicho ulitoa taarifa ya tukio hilo katika Kituo cha polisi mjini Tunduru na askari walipokwenda kwenye eneo la tukio nao waliukuta mwili wa Bakari ukiwa unaning’inia juu ya mti mrefu.
Alisema kuwa askari hao ambao waliongozana na mganga toka hospitali ya Serikali ya Wilaya ya Tunduru walibaini kuwa Bakari alikuwa amejinyonga kwa kutumia kamba ya katani ambayo alijifunga shingoni kisha kujining’iniza kwenye mti mrefu.
Amebainisha zaidi kuwa uchunguzi wa awali wa polisi kwenye kitongoji hicho umebaini kuwa Bakari kabla hajafikia uamuzi wa kujinyonga alikuwa akilalamika kwa muda mrefu kuwa amekata tamaa ya kuishi duniani kutokana na kuugua kwa muda mrefu maradhi hayakuweza kutajwa.
No comments:
Post a Comment