Na Augustino Chindiye ,Tunduru
JUMLA ya Tani 7000 za Korosho kutoka kwa Wakulima wa Wilayani Tunduru zimepangwa kununuliwa na Chama kikuu cha Ushirika cha wakulima wa Wilaya hiyo (TAMCU) katika msimu wa Mwaka 2011/2012.
Hayo yamesemwa na Meneja Mkuu wa chama hicho Imani Kalembo na kuongeza kuwa ununuzi huo utaanza kufanyika Novemba 10 mwaka huu baada ya kukamirika kwa taratibu za mkopo wa Shilingi Bilioni 5.986 kutoka Benki ya CRDB.
Kalembo aliendelea kufafanua kuwa katika msimu huu ambao chama hicho kinaendelea kununua kupitia mfumo wa Stakabadhi Gharani mkulima atalipawa mkononi Shilingi 850/= kwa kila kilo atakayoiuza na baada ya Korosho hizo kuuzwa na chama hicho mkulima atapatiwa fedha zake zilizo bakia ambazo ni Tsh.350/= na kufanya jumla ya Tsh.1200/= ambayo ndiyo bei ya soko kwa kila kilo moja ya zao hilo katika msimu huu.
Kalembo aliendelea kueleza kuwa kufuatia hali hiyo kwa kuanzia Chama hicho kimekwisha leta Shehena ya magunia 72,300 zenye thamani ya zaidi ya Shilingi Milioni 300 zenye uwezo wa kununulia wastani wa Tani 6000.
Alisema katika kuhakikisha kuwa mpango huo unafanikiwa na kuhakikisha kuwa korosho zote zinauzwa ndani ya Wilaya hiyo na kuiwezesha halmashauri yao kukusanya Ushuru wake TAMCU imeandaa mitego na mikakati mbalimbali ya kuwanasa walanguzi ambao hununua Korosho hizo kwa kutumia vipimo visivyo kuwa halali maalufu kwa jina la Kangomba.
Meneja huyo alibainisha baadhi ya mikakati hiyo kuwa ni pamoja na kuunda vikosi kazi vinavyo shirikiana na viongozi na waandishi wa Vyama vya Msingi (AMCOs LTD) pamoja na kupeleka fedha na kuanza kununulia Korosho zilizopo katika vyama vya msingi vya Namitili na Mtetesi mpakani mwa Wilaya za Tunduru Mkoani Ruvuma na Wilaya ya Nanyumbu Mkoani Mtwara zikiwa ni mbinu za kuwadhibiti walanguzi hao na kwamba atakaye kwepa katika maeneo hayo na kukamatwa wakati wa mauzo ya Korosho hizo atanyang`anywa korosho zote bila malipo.
Nae Mwenyekiti wa Chama hicho Wilaya ya Tunduru Mahamudu Katomondo akizungumzia ucheleweshwaji wa zoezi la kuanza kununua Korosho hizo kutoka kwa wakulima ikiwa ni zaidi ya mwezi mmoja toka Bodi ya Korosho Tanzania itangaze kufunguliwa kwa msimu kuanzia Oktoba 1 mwaka huu alisema kuwa hali hiyo ilitokana na kuchelewa kuiva kwa Korosho za wakulima wa Wilaya hiyo.
Mwisho
No comments:
Post a Comment