Na Augustino Chindiye,Tunduru
MAPIGANO makali ya kugombea Ardhi ya kulima yamezuka kati ya wakazi wa vijiji vya Semeni Chikomo Wilayani Tunduru Mkoani Ruvuma na kumjeruhi kwa kukata kata kwa Mapanga mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Mohamed Abdalah.
Kufuatia tukio hilo majeruhi huyo amelazwa katika Hospitali ya Missioni ya Mbesa baaya ya kujeruhi vibaya sehemu mbali mbali za mwili wake hali iliyo pelekea zaidi ya watu 50 wakazi wa kijiji cha Chikomo Wilayani humo wanatafutwa na Polisi ili waweze kujibu tuhuma hizo zilizotokaka na wananchi wa vijiji hivyo kuanzisha mapigano hayo.
Wakizungumzia tukio hilo kwa nyakati tofauti mbali na kukiri kutokea kwa ugomvi huo madiwani wa Kata za Mtina Mahamudu Katomondo na Kata ya Mbesa , Mohamedi Mtiko kila mmoja wao alitoa lawama kuwa wananchi wa kijiji jirani ndio chanzo cha mgogoro huo.
Upande wa Diwani wa kata ya mtina Katomondo yeye alidai kuwa wananchi wa kijiji cha Chikomo ndio waliofanya makosa ya kuvamia mipaka ya kijiji chake akidai kuwa mpaka unaotenganisha kijiji cha Semeni na Chikomo iliwekwa eneo la ng’ambo ya Mto Lukumbule.
Wakati diwani huyo akitoa madai hayo Diwani wa Kata ya Mbesa Mtiko yeye alidai kuwa na watu watatu waliohusika wakati wa upimaji wa mipaka hiyo mwaka 1978 na wanayo ramani hiyo inayo onesha mipaka ya vijiji hivyo na kwamba ugomvi uliopo kati ya vijiji hivyo umetokana na wananchi wa kijiji cha Semeni kukaidi kulipa ushuru unaotakiwa kutozwa pindi wakulima wanapovuka mipaka na kwenda kulima kijiji jirani.
Akiongea kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya hiyo,Katibu tawala wa Wilaya ya Tunduru Martini Mulwafu mbali na kukiri kuwepo kwa mgogoro huo alisema kuwa ofisi yake imepanga kufanya mazungumzo kati ya viongozi kutoka katika Tarafa, kata na vijiji vinavyohusika na mgogoro huo ili kutafuta ufumbuzi wa kudumu.
No comments:
Post a Comment