Na Gideon Mwakanosya, Songea
JESHI la Polisi Mkoani Ruvuma linawashikilia watu watano wakikabiliwa na tuhuma za kukutwa na puri 54 za bangi ambayo ilikuwa ikiuzwa kwenye eneo la Mshangano katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma Michael Kamuhanda amesema kuwa tukio hilo lilitokea jana majira ya saa tatu asubuhi huko katika eneo la Mshangano Manispaa ya Songea ambako askari wakiwa doria walifanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao wakiuza wengine wakinunua bangi.
Amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Kessy Mwegela (28) na Jordan Juma (19) wote wakazi wa bombambili,wengine ni John Kanjoroka (26) na Joseph Moyo wote wakazi wa eneo la Mshangano Manispaa ya Songea.
Amesema kuwa watuhumiwa hao baada ya kuona askari Polisi wakiwa wamewazunguka walitafuta njia ya kutaka kukimbia lakini Polisi walifanikiwa kuwatia mbaroni wakiwa na puri 54 kwenye mfuko wa Rambo na nyingine zilikuwa kwenye mifuko yao ya suruali walizokuwa wamevaa.
Amefafanua kuwa watuhumiwa hao kati yao ni wauzaji maarufu wa bangi katika Manispaa ya Songea na wengine ni wavutaji ambao walikuwa wamefika kwenye eneo hilo kwaajili ya kununua bangi.
Kamanda kamuhanda amesema kuwa polisi bado inaendelea kufanya upelelezi zaidi wa tukio hilo na kwamba utakapokamilika watuhumiwa watafikishwa Mahakamani kujibu mashtaka yanayowakabili.
No comments:
Post a Comment