Wanafunzi wa darasa la awali katika shule ya Msingi Zimanimoto iliyopo kwenye Kata ya Mfaranyaki Halmashauri ya Manispaa ya Songea wakiwa wamekalia madawati yaliyotolewa na Diwani wa Chadema Rhoda Komba
Wazazi wa wanafunzi wa darasa la awali wakiwa kwenye viwanja vya shule ya msingi Zimanimoto kwa ajili ya kusherehekea mahafali ya watoto wao na kupokea msaada wa madawati kutoka kwa Diwani wa Chadema Rhoda Komba
Diwani Rhoda Komba akimtunuku cheti cha kuhitimu darasa la awali Juma Abasi
Na Stephano Mango,Songea
DIWANI wa Viti Maalum kupitia chama cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema) katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma Rhoda Komba amekabidhi msaada wa madawati 10 yenye thamani ya TSh 450,000 kwa ajili ya darasa la awali katika Shule ya Msingi Zimanimoto
Komba akizungumza wakati wa hafla fupi ya mahafali ya awali katika viwanja vya shule hiyo jana alisema kuwa kuna siku alipita kandokando ya shule hiyo na kuwaona wanafunzi wa darasa la awali wakiwa wamerundikana kwenye darasa moja na kugombania madawati
“Hali ile ilinihudhunisha sana nikaamua kutafuta fedha kwa ajili ya kutengeneza madawati ili nije niwakabidhi kwa lengo la kupunguza idadi ya wanafunzi wanaokaa chini na kukuza malezi ya watoto hao kwa kuwapatia elimu bora”
Alisema kuwa elimu bora kwa mtoto ni nguzo muhimu sana kwa maendeleo ya taifa letu na endapo atalelewa vizuri katika darasa la awali atakuwa amejengeka vyema kitabia na kielimu na kumsababisha kuwa na uwezo anapoingia darasa la kwanza
Aidha Diwani huyo pia ameahidi kumsomesha mtoto aliyehitimu darasa la awali katika mahafari hayo Immakulata Gomela mwenye ulemavu wa ngozi kwa kumpatia sare za shule,madaftari,michango ya shule,viatu na huduma ya afya kuanzia darasa la kwanza hadi darasa la saba
Akizungumza kwenye hafla hiyo Mwalimu wa darasa la awali Joha Tambulu alisema kuwa darasa la awali lina wanafunzi 90 ambao wanakalia madawati tisa na kusababisha adha kubwa ya ufundishaji kwani dawati moja linapaswa likaliwe na wanafunzi watatu lakini wanakaa wanafunzi saba na wengine wanakalia matofali
Tambuli alisema kuwa kwa msaada huu wa madawati 10 kunafanya darasa la awali kuwa na madawati 19 ambayo kwa kiasi kikubwa kumepunguza mlundikana wa wanafunzi kwenye dawati moja na kufanya wanafunzi wengi kushindwa kuandika vizuri na kupelekea kuwa na mwandiko mbaya
MWISHO
No comments:
Post a Comment