About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Thursday, December 1, 2011

KIJANA TAIFA LA KESHO NI FALSAFA ILIYOPOTOSHWA KWA MAKUSUDI

Vijana wa kundi la sanaa la Wazalendo wakiwa kwenye picha ya pamoja baada ya kumaliza kikao chao cha maandalizi ya uzinduzi wa filamu ya The Challenge(Majaribu) inayotarajiwa kuzinduliwa Disemba 22 mwaka huu

Na Stephano Mango.Songea
 
TAIFA lolote Duniani haliwezi kukua na kuwa imara kiuchumi na kijamii bila makundi yote ya jamii kushirikishwa kikamilifu katika mapambano dhidi ya umasikini,maradhi na ujinga.

Ni wazi kuwa katika ulimwengu huu wa sasa,asilimia kubwa ni vijana ambao kimsingi ndio wanaopaswa kuwa viongozi wa leo na kesho na nguvu yao inahitajika sana katika jamii zetu kutokana na maarifa na mchango wao katika kusukuma gurudumu la maendeleo ulivyo mkubwa.

Hivyo basi, vijana ni kundi kubwa na rasilimali muhimu katika kuleta maendeleo ya taifa lolote lile duniani kutokana na nguvu na fikra za kimapinduzi walizo nazo.

Ukweli wa jambo hilo huwa ni rahisi kudhihirika waziwazi endapo vijana wataandaliwa vyema katika jamii zao kushiriki na kushirikishwa katika kubuni, kupanga na kutekeleza mikakati mbalimbali ya mandeleo.

Viongozi wengi wamekuwa wakisema mara kwa mara hasa wanapowapa nasaha utasikia wakisikika wakisema “Vijana ni Taifa la kesho fanyeni kazi kwa bidii na sio kuzurula ovyo, hampaswi kuishi lelemama na kuzubaa katika vijiwe huku mkipiga soga ambazo hazina umuhimu katika maisha yenu kwa kuwa kuwepo kwa vijiwe husababisha vishawishi vikubwa katika anasa na tamaa za kumiliki mali pasipo kufanya kazi.
 
Kitendo cha kuwafungua vijana masikio na kuyeyusha fikra mgando ambazo zinatawaliwa na uvivu,uchu wa mali na maisha ya anasa kilikuwa ni kizuri na chenye busara katika fikra yakinifu katika kukabiliana na changamoto zao

Ufanyaji wa shughuli za kimaendeleo ambazo zinaleta ukombozi katika jamii zetu ni jambo la kheri na huleta faraja katika maisha na mustakabali wa harakati za vijana wenyewe na jamii zao.
 
Nimekusudia kuandika makala haya kutokana na kushindwa kuivumilia falsafa inayotumika mara nyingi hasa na viongozi wengi ambao wanadhamana mbalimbali katika nchi hii,ujumbe unaotolewa huenda ulikuwa mzuri katika maisha ya vijana lakini kauli ya kusema vijana ni taifa la kesho ndiyo inayoleta ugomvi katika harakati za vijana na hapa ndio hoja yangu.

Ni dhahiri kuwa falsafa ya “vijana Taifa la kesho” imekuwa ikisemwa mara nyingi ambayo ni upotoshwaji mkubwa katika uhalisia wa mambo licha ya kuwa kauli yenyewe sio ngeni katika masikio ya jamii, kwani imekuwa ikijirudia mara kwa mara katika majukwaa mbalimbali.

 Kuna juhudi kadha wa kadha zimefanyika na wanaharakati mbalimbali wa masuala ya vijana katika kuipinga falsafa hiyo na kuonyesha falsafa mbadala katika kuweka mambo sawa na kupunguza malumbano yasiyo ya msingi

Ila kutokana na ugumu wa wanasiasa wengi kukubali mabadiliko chanya na yenye kueleweka katika maisha ya vijana kwa sababu zao binafsi ikiwemo hofu ya kizazi kipya kuchukua nafasi katika nyanja mbalimbali za uongozi,wanaendelea kuleta mikaganyiko katika jamii kwa faida zao za ulafi wa madaraka

Viongozi hao wamebaki kutoa mahubiri hasi ambayo hayana mantiki bali ni nguvu ya kuwavesha vijana kilemba cha ukoka na fikra mgando za kusubiri muda wa kuitumikia nchi yao kwa kutumia hoja hafifu ya kjana Taifa la kesho pasipo kesho kutimia

 Lugha wanayoitumia ni laghai na kimantiki neno kesho huwa halikamiliki katika mfululizo wa siku ingawa kimsingi kesho ni neno ambalo lina uhalisia wake kinadharia zaidi kuliko kivitendo.

 Jambo ambalo linathibitishwa na kamusi ya Kiswahili sanifu iliyotungwa na Taasisi ya uchunguzi wa Kiswahili chuo kikuu cha Dar-es-salaam ambapo inafafanua kuwa kesho ni “siku inayofuata baada ya leo, ni wakati ujao”.

Hiyo ina maana kuwa hakuna siku itimiayo katika mawazo ya kawaida ya binadamu iitwayo kesho kwa kuwa kesho huwa haifiki, ni siku ambayo inapaswa kusubiriwa tu kila kunapokucha.
 
Napata tabu sana katika kufikiri ili nielewe katika tafsiri ya kijana taifa la kesho,sielewi mwanzilishi wa falsafa hiyo alikuwa anamaanisha nini na kwa maslahi ya nani? Endapo yupo basi nahitaji mjadala naye ili kuweka sawa hoja husika

Wengi katika jamii waliisikia falsafa hii kwa mara ya kwanza katika utoto wao na hasa walipokuwa katika madarasa ya watoto kwenye shule za awali au za msingi.

 Ni wazi kuwa walimu walisikika mashuleni wakiitumia falsafa hii ili kutufanya tujifunze kwa maarifa na ujuzi na tuzoee kutenda mema na kujijengea sifa nzuri kwa ahadi kuwa sisi ni viongozi wa baadaye yaani tafsiri nzuri ni “Taifa la kesho”.
 
Je inawezekana kauli hiyo ilikuwa sahihi kipindi cha utoto wetu,sisi ambao kwa sasa ni vijana? naamini kila mmoja kwa kutumia vigezo vyake anaweza kujibu swali hilo hapo juu,

Katika mikataba na sheria mbalimbali za kimataifa zinafafanua kuwa binadamu mwenye umri kuanzia miaka 0-17 ni mtoto na haruhusiwi kufanya maamuzi yeyote mazito kuhusu maisha yake, ingawa kamusi tajwa hapo mwanzo inaleta utata katika vipande viwili vya umri hasa katika maana ya kijana,kamusi inasema kijana ni mwana mdogo,mtoto mwenye umri wa miaka 7 hadi12.

 Lakini katika mtazamo wa kawaida tunaamini kuwa kijana ni binadamu mwenye umri wa
kuanzia miaka 18-40 na wakati mwingine mpaka miaka 45.

 Ukirejea kamusi tajwa hapo juu tafsiri ya Taifa ni jamii ya watu wanaoishi katika Nchi moja na wanaounganika kutokana na matukio ya kihistoria,mfumo wa uchumi na utamaduni chini ya serikali moja.
  
Kauli ya kijana ni taifa la kesho kwa namna yoyote ile imepotoshwa kwa mujibu wa tafsiri ya kamusi kuhusu taifa.Nasema hivyo kwa sababu tunapozungumzia kesho kimantiki ni wakati ambao unasubiriwa,hata ukizungumza juu ya taifa huwezi kukwepa kutaja ardhi,mipaka,watu na serikali yao kama vielelezo vya taifa husika,sasa itakuwaje kijana ambaye yupo useme ni taifa la kesho,rejea tafsiri ya taifa na kesho

Tafsiri ya mtu kama kijenzi kimojawapo katika taifa haitugawi katika makundi ya umri wala kabila,awe mtoto,kijana,mzee,kilema ama vyovyote vile bado mtu atabaki kuwa ni sehemu ya Taifa tena la leo sio kesho

 Pasipo kujali dhana ya wakati uwe uliopita,uliopo au ujao bali kwa kuzingatia kipindi chote ambacho binadamu yupo hai.
  
Naamini huhitaji nguvu nyingi ili uweze kubaini upotoshwaji uliopo katika falsafa ya kijana ni taifa la kesho kwa kuwa inapoteza maana ya kijana na juhudi zake katika kufikiri,kubuni na kuthubutu kutenda.
  
Kimsingi falsafa hii ina walakini katika kuichanganua na kuelewa kusudio la mwanzilishi wa falsafa hii kwa kuwa watu wengi katika mtazamo wao mara wasikiopo neno kijana,humaanisha ni mtu mwenye umri wa miaka 18 hadi 40 sasa mtu huyo atakuwaje taifa la kesho wakati yupo leo

Binadamu siku zote tunapaswa kuwa makini katika fikra zetu na kauli tuzitoazo kwani uzoefu unaonyesha kuwa ndizo zinazozaa matendo yetu.

Lakini ni muhimu zaidi kusoma matendo yetu na kuyaelewa kwani matendo tuyatendayo ndiyo hasa tabia zetu.

Natambua pasipo shaka utofauti uliopo kutoka binadamu mmoja na mwingine katika jamii zetu,juu ya uwezo wa kufikiri na kuchambua mambo kutokana na sababu za kibailojia.
 
Hivyo naamini kuwa wapo watu wenye mtazamo wa kuwaona vijana ni taifa la kesho,binafsi naona mtazamo huo ni potofu,asiye amini kauli na mtazamo wangu basi mlango upo wazi hivyo karibu katika mjadala ili kuweka mambo sawa.

 Kwa kutumia akili ya kawaida haitamuwia vigumu binadamu yeyote yule kuona,kushawishika na kukubali mchango wa vijana katika maendeleo na ustawi wa jamii katika taifa lolote lile.

 Kwa kuwa vijana ndio wajenzi wazuri wa taifa hata hoja kulingana na mazingira stahiki,na wao ndio wanaopaswa kufanya shughuli zote za kimaendeleo ambapoa wazee wanapaswa kuwa washauri na kuwaachia vijana nafasi ili waweze kulitumikia taifa lao
  
Ni wazi kuwa endapo vijana wakipewa nafasi ya kushiriki katika kuunda taifa na kushughulikia mambo ya kimaendeleo kama vile ulinzi na usalama,biashara ndogo ndogo na kubwa,udaktari,ukulima,masuala ya michezo,sheria na mengineyo taifa litapiga hatua zaidi kimaendeleo.

 Kwa misingi hiyo,falsafa ya kumwona kijana ni taifa la kesho itanapaswa kufa iwe yenyewe au kwa kuiua kwani bila shaka falsafa hiyo inapaswa kuwa ni taifa la wakati wa sasa wafanyapo kazi za kujenga taifa lao (Taifa la leo),hivyo itakuwa ni vigumu kuwahadaa vijana kusubiri taifa la kesho wakati wao wanaishi leo

Falsafa ya vijana ni taifa la kesho ina ukakasi sana kwa sababu inawejengea vijana tabia ya kusubiri katika kuchukua hatua juu ya maisha yao.Hivyo inawapa na kuwajengea matumaini ya kuwa wajinga na wanyonge sambamba na kuhimizwa kuwa na subira kwa vitu visivyokuwepo.
 
Ni wazi kuwa muda umefika wa kumwona kijana ni taifa la leo,sasa hii ndio inapaswa kuwa kauli au falsafa mbadala kuliko kuiendekeza falsafa ambayo haieleweki katika akili za watu

Katika karne hii ambapo maendeleo ya sayansi na teknolojia yamesambaa duniani kote vijana wanapaswa kushika madaraka mbalimbali katika taifa lao,ni jambo la aibu kumkuta mzee ambaye kimsingi anapaswa kuwa amestaafu bado yupo kazini,huu ni ubinafsi,uchoyo na ulafi.Inashangaza kuona wazee wakipunguza umri wa kuzaliwa na kuongeza umri wa kustaafu ili waendelee kung’ang’ania madaraka
  
Vijana tuamke tuseme ukweli dhidi ya wazee wetu,wang’atuke na watupishe ili nasi tutimize wajibu wetu,hakuna ulazima wowote wa wao kuendelea kuzeekea katika madaraka ili hali wana watoto ambao kimsingi wana elimu ,hali kufikiri,kubuni na kuumba vitu anuai,wazee pumzikeni kwani wajibu wenu tayari mmeutimiza ulio baki ni wetu vijana
  
     
        0755 33 50 51 au 0715 33 50 51 au 0784 33 50 51
 

No comments:

Post a Comment