About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Thursday, December 1, 2011

KAPTENI LOWASSA UNAKUMBUKA SWALI LA KIJANA ARON SHERA

 
                                                        Edward Lowassa(Mb)
Na,Stephano Mango,songea
NIMEAMUA leo kuandika makala haya ili kuweka kumbukumbu sawa dhidi ya kauli tata zinazotolewa na Mbunge wa Monduli Kapteni Edward Lowassa mara kadhaa anapopata fursa ya kuzungumza jambo
 
Nimemsikia mara nyingi kiongozi huyu akitamka na kuwataadharisha viongozi wenzake hatari inayokaribia kutokea endapo vijana wataendelea kuachwa nguvu yao ikipotea bure bila kupewa ajila itakayoweza kuleta mabadiliko chanya kwa taifa letu
 
Hakuna ubishi kuwa taifa lolote duniani  haliweza kukua  na kuwa imara kiuchumi na kijamii bila makundi yote ya jamii kushirikishwa kikamilifu katika mapambano dhidi ya umasikini, ujinga na maradhi na hasa kundi kubwa la vijana.
   
Kwani katika ulimwengu huu wa sasa asilimia kubwa ni vijana, na ndio viongozi wa leo na kesho, na nguvu kazi yao inategemewa sana katika kuendeleza jamii zetu licha ya ukweli huo kufahamika, jambo hili linapuuzwa na kuwafanya vijana kukosa thamani kutokana na mambo  mengi yanayo wazunguka ambayo hupelekea kupoteza heshima, utu na nafasi yao katika jamii na Taifa kiujumla
 
Leo anapotokea kiongozi ambaye kimsindi ndio sehemu ya kuasisijambo hilo kwa vijana kupoteza heshima yao na kutoa kauli tata kuhusu ajira kwa vijana,natafakari kwa umakini ili kuweza kuona agenda iliyopo nyuma ya panzia na anayezungumzia hoja hiyo na kubaini usafi wake
 
Na kwasasa nimeamua kuanza na tendo  lililotokea mwishoni mwa mwezi septemba 2007 wakati aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Ngoyai Lowassa alipoenda mkoani Mwanza  kwa ziara ya kikazi
 
Ziara hiyo ilikuwa ni muendelezo wa kile kilicho tafsiriwa na watu wengi kuwa ni kwenda kuifafanua na kutangaza uzuri wa bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha wa 2007 na 2008 kwa wananchi.
 
Katika ziara hiyo,Lowassa kamwe hatasahau alipo kumbwa na vituko ikiwemo kushuhudia  majibu ya uongo kutoka kwa aliyekuwa Waziri wa Miundo Mbinu Andrwe Chenge kuhusu kivuko kibovu kilichopo kisiwa cha Ukelewe.
 
Bila aibu wala uwoga Chenge alilazimika kuanzisha malumbano na wananchi waliokuwa wakipinga kauli yake mbele ya  Mbunge wa jimbo hilo wakati huo Getrude Mongela,huku Chenge akiendelea kutetea jibu lake la uongo kwa madai kuwa kivuko kina fanya kazi vizuri
 
Jambo ambalo dhahiri lilikuwa ni utovu wa nidhamu mbele ya Waziri Mkuu,ndipo mbunge wa jimbo husika Getrude Mongella alipo lazimika kuweka mambo sawa kwa kupinga kauli ya Chenge waziwazi na kuacha siasa za kulindana huku akiwaunga mkono wapiga kura wake kwa kusema ukweli.
Hali hiyo ilimfanya Kapteni Lowassa aende eneo husika akajionee hali halisi,akiwa kivukoni almanusula azame pale mashine(Ingine) ya kivuko ilipozima ghafla mbele yake ndipo alipo amuru kivuko hicho kifanyiwe matengenezo ya haraka.
 
Akiwa katika kisiwa hicho cha Ukelewe Kapteni Lowassa aliulizwa swali na kijana Aron Wambura Shera,mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika shule ya sekondari ya Pius Msekwa ambapo kijana Aron alimuuliza Lowassa  akiwa Waziri Mkuu wakati huo,ninanukuu”Mheshimiwa Waziri Mkuu tumekuwa tukikusikia kupitia vyombo vya habari,wewe pamoja na wasaidizi wako mkituhimizi tusome kwa bidii na maarifa ili kusudi tuje kuwa viongozi wa taifa la kesho, lakini mbona hatuoni hayo katika matendo yenu?
 
Alihoji uhalali wa viongozi wengi kupewa nyadhifa zaidi ya moja wakati kuna wasomi wengi vijana ambao wangeweza kushika nyadhifa hizo huku vijana wengi wakiwa wameachwa wakizubaa mitaani.
 
Aron akijithibitishia kauli yake alitoa mfano wa aliyekuwa Mkuu wa mkoa wa Mwanza Alex Mselekela ambaye pia ni mbunge wa Tabora kaskazini na kuhoji mtu huyo anawezaje kufanya kazi zote mbili kikamilifu?
 
Kapteni Lowassa  hakujibu swali hilo bila sababu za msingi ila alisema atarudi kujibu swali hilo siku nyingine bila kuitaja  siku husika ambapo staili aliyoitumia Kapteni Lowassa kukwepa swali lenye mantiki liliwashangaza wanafunzi wengi waliokuwepo katika eneo hilo,
 
Toka siku hiyo vijana walikatishwa tamaa na Kapteni Lowassa kwa kuwa walitegemea watapewa majibu mazuri,hii ni kutokana na uwezo wa Kapteni Lowassa kujibu maswali kwa umahiri mkubwa wakati huo akiwa Waziri Mkuu
 
Hadi leo tumetimiza miaka minne Kapteni Lowassa ameshindwa kujibu swali la kijana Aron ambalo liliulizwa kwa niaba ya vijana wa Tanzania kwani swali hilo linaeleza hisia halisi za vijana wa Tanzania na uwepo wa mashaka yao lukuki dhidi ya watawala wao
 
Swali lilikuwa wazi kabisa, kwanza linatoa ujumbe kwa watawala wetu kuwa hawatendi sawa na wanachokisema ni uthibitisho kuwa watawala wanaamini wasichokijua na kudharau wanachokijua .
 
Pili inaonyesha kuwa viongozi hawafanani na kile wanachodai kuwa wanatutumikia ingawa ukweli utabaki palepale kuwa viongozi wengi hutumikia matumbo yao huku wakitulaghai kwa maneno ya kinafiki kama vile uchumi unapaa huku umasikini ukionekana dhahiri kukithiri kwa watanzania wengi.
 
Tatu huo ni uthibitisho wa kukua  kwa kasi kwa fikra za kimapinduzi miongoni mwa vijana ambao Lowassa aliwakatisha tama toka mwaka 2007 ambapo leo tunashangaa anawazungumzia hadharani bila kukumbuka swali aliloulizwa na kijana Aron
 
Ni wazi sasa vijana wanathubutu kuhoji,kueleza mawazo yao na kuwabana viongozi kuhusu matendo yao machafu wayafanyayo wakiwa madarakani,ambayo kimsingi yana haribu mustakabali wa kizazi kilichopo na kijacho.
 
Vijana wamechoshwa na mtazamo wa kuwaona wao kuwa ni viongozi wa taifa la kesho huku leo wakikosa malezi stahiki na maandalizi mazuri katika kuchukua majukumu yao leo na hiyo kesho.
 
Kutokana na viongozi wengi kuwa na  fikra za ulafi wa mali za umma huku watanzania wengi wakiteseka na kushuhudiwa na vijana ambao ndio kundi muhimu na ni nguvu kazi ya taifa lolote lile duniani vijana wameamua kuchukua hatua wao wenyewe
 
Vijana wameamua kupaza sauti zao hasa pale nafasi inapojitokeza kwani wamekandamizwa kwa muda mrefu ambapo kumewafanya waweza kuthubutu  kutoa maoni yao waziwazi bila hofu kutokana na uhalisia na ugumu wa maisha wanaouona kwa wazazi wao na hivyo kujiandaa katika kuonyesha njia stahiki itakayo wasaidia kupata maisha yenye neema huko mbele
 
 Hivyo wanajua fika kuwa hali ngumu ya maisha inasababishwa na viongozi walafi ambao wanakula bila kunawa kwa kuingia mikataba mibovu ,kufanya ufisadi na ubadhilifu wa mali za umma bila huruma na kutuacha tukiwa masikini huku  wakifirisi nchi na kwenda kuwekeza nje ya nchi sambamba na kujirundikia vyeo lukuki ili kulinda maslahi yao
 
Vijana wakiwa katika fikra za mapambazuko na kutafuta mwanga stahiki katika maisha yao wanathubutu kuhoji uhalali wa viongozi kujirundikia vyeo kwa mara moja na wanapiga hatua kwa kutaka mafisadi na wabadhilifu wachukuliwe hatua na sio kuchukua nafasi ya kuwatetea
 
Hebu rejea maandamano ya wanafunzi yaliofanyika Agosti mosi mwaka 2007 yenye lengo la kupinga ongezeko jipya la nauli ya sh 50  na kuwa sh 100  kwa usafiri wa mabasi maarufu kama daladala kwa wanafunzi jijini Dar Es Salaam
 
Katika hali ya kimapinduzi na ukakamavu vijana walithubutu kubeba mabango yenye ujumbe mbalimbali wenye maana pana sana,bango moja lilisomeka “Mh JK utawala umekushinda?tulipe sh 100 kwa kipi mlichoboresha? Kiama chenu 2010, bango hilo halikuishia hapo liliendelea kusomeka”wafilisiwe chege ,lowaza , mkaapa kalamaagi na yona”na tuletewe  mabasi ya shule.
 
Kauli ya vijana ni ishara ya uwepo wa kiu kali miongoni mwa vijana wenyewe dhidi ya kusambaratisha mtandao wa viongozi mafisadi nchini ambao kimsingi ndio chanzo ulafi wa madaraka na kurundikiana vyeo ili kulindana katika maslahi ya kifisadi, ambapo watu wengi huishi katika maisha magumu na yanayozidi kuwavujisha jasho watanzania wengi.
  
Ni wazi kuwa hiki ni kizazi ambacho kimeanza kutambua wajibu wake kwa jamii,ni kizazi kinachoandaliwa katika mazingira ya hasira dhidi ya serikali hii kutokana na kudharauliwa pale wanapodai haki zao.
 
Kamwe vijana wasipuuzwe kupewa haki zao, hakika sio busara kuomba haki,hivyo haki inapaswa kudaiwa waziwazi na yoyote anayefinyanga haki za watu ni adui mkubwa,ni wazi kuwa maneno yaliyo andikwa kwenye mabango yaliyobebwa  na wanafunzi hao yasipuuzwe kwani ujumbe wao umefika ingawa leo vijana tunamshangaa Kapteni Lowassa baada ya kuachia ngazi ya Uwaziri Mkuu anajitokeza kuwatetea vijana
 
Vijana wanajifunza kufikiri kisayansi na kujenga hoja zenye mantiki na zenye ushawishi mkubwa kwa jamii,hivyo majibu sahihi yanahitajika katika kukidhi hamu na matakwa yao kwa manufaa ya nchi yetu.
 
Wanapothubutu kuwahoji watawala wana haki ya kupewa majibu yenye mantiki kwa wakati husika kwani kutokutoa majibu stahiki ni kujiaibisha mbele ya macho ya jamii na kutengeneza mshangao hasa wakati huu ambapo utetezi wa vijana unapotolewa na mtu aliyeshindwa kuandaa mfumo mzuri wa maisha ya vijana nchini alipokuwa kwenye madaraka makubwa kama ya Uwaziri Mkuu
  
 Hivyo Kapteni Lowassa hakuwa na sababu ya kukwepa swali aliloulizwa na kijana Aron Shera kwani swali hilo ni la msingi sana kwa mustakabali wa maisha ya vijana ambao leo kwa unafiki mkubwa anajidai kuwatetea katika suala la ajira
 
Lowassa wakati huo alipaswa kutoa majibu ya kina bila kumung’unya maneno kwani swali hilo halikuhitaji takwimu wala utafiti katika kujibu,sasa ilikuwaje Kapteni Lowassa ashindwe kuwa na jibu hadi aseme angerudi kujibu swali hilo kwa wakati mwingine.
 
Vijana hatutaki kuzubaishwa kwa majibu yenye utata kwa kuwa Kapteni Lowassa alishindwa kutupa jibu hadi alipojiudhuru ambapo bila kificho alijifedhehesha mwenyewe mbele ya vijana kwa kutotimiza wajibu na ahadi yake.
 
Akiwa madarakani Kapteni Lowassa alikumbushwa kulijibu swali la kijana Aron na wanaharakati mbalimbali wa masuala ya vijana nikiwemo mimi lakini aliupuuza ushauri wetu na kutuona tuliokuwa tunamkumbusha tumepungukiwa akili
 
Leo bila kificho tunamtaka ajibu swali aliloulizwa,baada ya hapo atuambie kwanini alishindwa kuweka mikakati stahiki na inayotekelezeka ya kutoa ajira kwa vijana wengi katika sekta binafsi na za umma alipokuwa Waziri kwa mara ya kwanza hadi pale alipokuwa Waziri Mkuu
 
Kwanini leo anajitokeza hadharani kuzungumzia suala la ajira kwa vijana akiwa kwenye madaraka ya Ubunge na katika hali ya uchafu anaodaiwa kuwa nao baada ya kubainishwa kashfa kadhaa ambazo anahusika nazo
 
Vijana tunajitambua kamwe hatuko tayari kuwa muhuri wa watenda dhambi kwani tulipothubutu kueleza mawazo yetu tulipuuzwa na kuendelea kushushwa heshima katika jamii na viongozi wetu leo tunapata tabuu kweli kuamini kuwa wanachokisema ndicho wanachomaanisha ikiwezekana watupishe nasi tushike hatamu katika kuwavusha miaka mingine hamsini baada ya uhuru
 
Mwandishi wa Makala haya
Anapatikana simu 0755-335051
 
 

No comments:

Post a Comment