Na, Augustino Chindiye Tunduru
WANAFUNZI wawili wa Shule ya Msingi Majala wamelazwa katika hospitali ya Wilaya ya Tunduru baada ya kujeruhiwa vibaya na radi huku kukiwa na taarifa kuwa wakazi wa familia 23 kukosa sehemu za makazi baada ya nyumba zao kubomolewa na Mvua.
Akizungumzia tukio lilo Mwenyekiti wa Kamati ya Maafa ya Wilaya ya Tunduru, Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Juma Madaha aliwataja Watoto hao kuwa ni Subira Mohamed anayesoma darasa la Tatu na Stamili Mohamedi anayesoma Darasa la sita wote wakiwa ni Watoto wa familia moja.
Kuhusu tukio la Nyumba 23 kubomolewa na mvua hizo Dc, Madaha alisema kuwa hivi sasa wananchi hao wanahifadhiwa katika nyumba za majirani zao wakati serikali ya Wilaya hiyo ikifanya tathimini ya athari zake.
Alisema kufuatia matukio hayo wananchi wanapaswa kujikinga kwa kuimarisha miundombinu ya nyumba zao pamoja na kuachana na tabia za kujificha katika miti wakati mvua zikiendelea kunyesha ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza.
Akifafanua taarifa ya tukio la radi Kaka wa majeruhi hao Wada Said alisema kuwa mkasa huo ulitokea wakati Watoto hao wakiwa wamejificha katika kibanda cha jiko la kupikia ambapo mvua kubwa iliyo ambatana na upepo ikinyesha kwa muda mrefu huku radi zikipigwa na kusababisha kuwajeruhi ndugu hao
Akizungumzia hali za majeruhi hao mganga mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya hiyo Dkt. George Chiwangu alisema kuwa hali za majeruhi hao bado siyo mzuri na wanahitaji kuwa chini ya maafisa tabibu kwa muda mrefu ili kuokoa maisha yao .
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma Michael Kamuhanda amethibisha kuwepo kwa matukio hayo na kueleza kuwa majeruhi wa tukio la radi waliumizwa vibaya sehemu mbalimbali za miili yao kufutia tukio hilo .
Mwisho.
No comments:
Post a Comment