NAIBU MEYA SONGEA CHUPUCHUPU AFUKUZWE KUONGOZA KIKAO
Na Stephano Mango,Songea
MADIWANI wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea walitofautiana kwa muda wa zaidi ya saa moja kwa kutaka kumuondoa Naibu Meya wa Manispaa hiyo Mariam Dizumba kwa madai kuwa muda wake wa uongozi umekwisha
Wakichangia hoja mbalimbali Madiwani hao katika kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika jana kwenye ukumbi wa Saccos ya Walimu wa Manispaa ya Songea ambacho kilikuwa kinaongozwa naye walimtaka Naibu huyo aondoke kwenye kiti chake ili uchaguzi wa Naibu Meya ufanyike
Diwani wa kata ya Ruhuwiko Gerald Ndimbo alisema katika kikao hicho kuwa kabla ya kuendelea na kikao ni vema madiwani tukapata ufafanuzi juu ya kikao kama ni kikao cha kawaida au ni kikao cha mwaka ambapo katibu wa kikao hicho ambaye ni Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Nachoa Zakaria alijibu kuwa ni kikao cha kawaida
Ndipo Diwani wa Kata ya Ruvuma Victor Ngongi alipoingilia kati kwa kutoa ufafanuzi juu ya kanuni za kudumu za mikutano na shughuli za Halmashauri namba 6 ambayo ilifanyiwa marekebisho mwaka 2005
Ngongi alieleza zaidi kuwa kanuni tajwa inasema kuwa kama ni mkutano wa kawaida basi agenda ya ratiba ya vikao mbalimbali vya Halmashauri iondolewe kwani agenda hiyo inaambatana na mambo makuu manne
Alisema kuwa mambo hayo ni pamoja na uchaguzi wa Naibu Meya,kuteua wajumbe wa kamati mbalimbali za kudumu, kujadili taarifa ya utendaji na uwajibikaji kwa mwaka uliopita na ratiba ya vikao
“Kutokana na mabadiliko hayo ya mwaka 2005,vikao vyote vya mwaka vinaishia mwezi juni ambapo mwezi julai tunaanza mwaka mpya wa fedha na uchaguzi wa unaibu meya na kamati zake zinatakiwa ziwe sambamba na mwaka wa fedha”alieleza Ngongi
Ngongi alimtaka Mkurugenzi wa Manispaa hiyo aliombe radhi baraza kwa kukiuka kanuni na kuwasumbua madiwani bila sababu za msingi kuelezwa kabla
Akifunga kikao hicho Naibu Meya Mariam Dizumba alioneka kuwa na hasira na kutamka kuwa kama madiwani wana roho ya kwanini waendelee kusubiri muda wa uchaguzi utakapofika
MWISHO
No comments:
Post a Comment