Mbunge wa Jimbo la Mbinga Magharibi,Kapteni John Komba akifungua Zahanati ya Tumbi, wa kwanza kulia ni Katibu wa CCM Wilaya ya Mbinga Anastia Amasy
Na Stephano Mango,Nyasa
KILA Kiongozi katika jamii anayo majukumu yake ya msingi ambayo anapaswa kuyatekeleza katika jamii husika kwa muda muafaka ambapo kwa upande wa vyama vya siasa wapo wale wa nyadhifa za uwakilishi ambao ni Madiwani, Wabunge, na Rais ambapo uwepo wao hutokana na Wananchi kuwachagua kupitia masanduku ya kura
Wawakilishi hao wana majukumu mengi ambayo kimsingi yameainishwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na ilani za uchaguzi za vyama vyao ambapo wakati wa kampeni walizinadi ilani hizo kwa nguvu kubwa.
Ambazo kimsingi zinapaswa kutekelezwa kwa viwango vilivyoahidiwa wakati wa kuomba ridhaa ya uwakilishi dhidi ya wananchi kwenye vyombo vya maamuzi.
Kwa sababu dhamana ya viongozi katika nchi mbalimbali duniani ni kuharakisha maendeleo katika jamii kwa kushirikiana na wananchi husika kwa lengo la kutatua kero zao kwa wakati ili kufikia malengo yanayokusudiwa na jamii husika.
Ni dhahiri kuwa ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kuna baadhi ya Wabunge wamefanya na wanaendelea kufanya juhudi kubwa ya kuhakikisha na wengine wamekuwa wakijikita na shughuli zao katika miji mikubwa na kusahau wapiga kura wao.
Wapo wabunge wengine wanafuatilia, na kusimamia utekelezaji wa ilani ya chama chao ambayo wao waliinadi kikamilifu kwa wapiga kura wakati wa Kampeni Mwaka 2010 lakini wengine toka wamepata ridhaa ya uwakilishi wamekuwa bize na mambo yao
Miongoni mwa Majimbo ya uchaguzi Nchini ambayo wapiga kura walipewa ahadi nyingi za kuletewa ustawi katika sekta za barabara, afya, elimu, mawasiliano, na uwezeshwaji kiuchumi ni Jimbo la Mbinga Magharibi ambalo ni miongoni mwa Majimbo saba ya Uchaguzi yaliyopo Mkoani Ruvuma.
Jimbo hilo ambalo limetangazwa hivi karibuni kuwa Wilaya ya Nyasa linawakilishwa na Mbunge Kapteni Mstaafu John Damian Komba ambaye wapiga kura wake wanamuita Mbunge wa Muyaya.
Hivi karibuni niliambatana na Mbunge Kapteni John Komba kutembelea Jimbo hilo ambalo kwa sasa lina jumla ya kata 15 ambazo ni Lundo, Luhangarasi, Liundi, Liparamba, Mtipwili, Lipingo, Lituhi, Mbambabay, Kilosa, Liuli, Kingilikiti, Chiwanda, Ngumbo, Tingi na Kihagara.
Ziara hiyo ya Kapteni Komba ilianzia kwenye Kata ya Lituhi ambapo alifungua Mashindano ya soka kombe la Kapteni Komba, mashindano ambayo yamefadhiriwa nay eye mwenyewe kwa gharama ya shilingi milioni 5
Ambazo zimegawanyika katika manunuzi ya jezi za timu 11 ambazo zinashiriki mashindano hayo, jezi seti tatu za waamuzi, mipira 2 ya mashindano, miamba ya chuma kwa ajili ya magoli, gharama za kutengeneza kombe
Katika mashindano hayo ambayo mshindi wa kwanza atapata zawadi ya shilingi 150,000/= na kombe, wa pili shilingi 100,000/=, wa tatu shilingi 50,000/= ambapo kwa timu 7 zilizobaki watapata kifuta jasho cha shilingi 20,000/= kwa kila timu
Pia alitembelea kata ya Ngumbo na kutoa msaada wa vitanda, mito, shuka, chandarua na magodoro wenye thamani ya shilingi 3 milioni kwenye kituo cha Afya Mkili na Zahanati ya Kijiji cha Mbuli ili kuondokana na tatizo la wagonjwa kulala chini kwa kutumia mikeka
Akitoa misaada hiyo kwenye viwanja vya Kituo cha Afya Mkili Komba alisema kuwa kwa muda mrefu nilikuwa nafahamu kero ya wananchi wa maeneo hayo kuwa ni afya, maji, barabara, elimu na mawasiliano lakini kwa miaka mitano iliyopita nilichagua kushughulikia suala la elimu ,mawasiliano na barabara ambapo kwa sasa nashughulikia afya na maji
“Natambua matatizo yaliyopo kwenye sekta ya afya katika Jimbo la Mbinga Maghalibi hivyo kwa kuanzia natoa msaada wa shuka 24, magodoro 14, vyandarua 14, mito 14, vitanda 14 kwa ajili ya kituo cha afya cha Mkili na pia Vitanda 6, shuka 12, magodoro 6, Vyandalua 6, mito 6, na mzani wa kupimia watoto na wajawazito 1 kwenye Zahanati ya Kijiji cha Mbuli”alisema Komba
Komba alisema kuwa vituo vya afya na Zahanati karibu zote katika Wilaya hiyo hazina wataalamu,Vifaa Tiba na usafiri wa wagonjwa lakini tatizo hilo limeanza kushughulikiwa kwa kasi kubwa na nguvu zaidi kwa kuanzia kutoa vitu hivyo
Alisema kuwa natambua kuwa wananchi wamelalamikia kwa muda mrefu matatizo hayo hasa ya ukosefu wa vitanda na shuka kwani wanapotakiwa kulazwa hulazimika kutafuta mikeka na vitenge kwa ajili ya kujifunika wakati wa kulala huku wakipata mwanga wa vibatali kutokana na kukosa umeme
Kwa upande wake Diwani wa Kata hiyo Emmanuel Nchimbi akipokea msaada huo alisema kuwa kwa muda mrefu kituo hicho kilikuwa kinakabiliwa na matatizo hayo hivyo kwa msaada huo wananchi wanaopata huduma za matibabu watakuwa wameondokana na matatizo yaliyokuwa sugu katika kituo hicho
Naye Mganga wa Kituo hicho cha Afya Thomas Magulilo alieleza kuwa kituo chake cha afya kwa sasa kinakabiliwa na tatizo la watumishi wa kada ya afya,usafiri kwa wagonjwa na ukosefu wa maji kwani wagonjwa wamekuwa wakichota maji Ziwa nyasa na kuyatumia kwa kunywa,kuoga na shughuli zingine na kusababisha kuongezeka kwa magonjwa ya matumbo
Magulilo alisema kuwa kituo hicho kinahudumia wagonjwa kutoka Vijiji vya Yola,Luhundi,Ndonga na Mkili na wengine kutoka maeneo jilani hivyo kituo kimekuwa kikitoa huduma kwa wagonjwa wengi kuliko uwezo wake kwani vifaa tiba vipo vichache,wataalamu wa kada ya afya wapo wachache na kusababisha huduma inayotolewa kuwa duni
Alisema kuwa magonjwa sugu yanayosumbua wananchi wa maeneo hayo kuwa ni Malaria,upungufu wa damu,Minyoo,magonjwa yatokanayo na hali ya hewa, kuhala na kutapika pamoja na ugonjwa hatari wa ukimwi
Akiwa Kata ya Mbaha Mbunge huyo aliwapa pole wahanga wa kimbunga kwa kuwapa msaada wa bati 500 zenye thamani ya shilingi 7.5 milioni kwa waathirika 30 wa kata ya Mbaha ambao nyumba zao ziliezuliwa na mvua iliyoambatana na upepo mkali mwanzoni mwa mwezi Februari mwaka huu na kusababisha harasa mbalimbali za mali
Diwani wa Kata ya Mbaha Stewat Nombo alimshukuru Mbunge huyo kwa msaada wake alio utoa kwa wananchi walio athirika na mvua hizo na kusema pia waathirika walipokea msaada wa maguni ya mahindi kutoka serikali ya wilaya ya mbinga. mbazo wanataka Mbunge wao kupitia serikali na wahisani wazitafutie ufumbuzi ili nao waweze kujivunia maendeleo yao.
Nombo amewaomba watu wengine wenye mapenzi mema kuwa tayari katika kuwasaidia watu mbalimbali wanao patwa na matatizo au majanga pindi yanapo jitokeza kwa kuwa kuna baadhi ya kaya hukosa chakula na makazi ya kuishi
Wakazi wa Jimbo hilo kama walivyo wapiga kura wa majimbo mengine nchini, wanamatumaini ya utatuzi wa kero zao kutoka kwa Mbunge wao kufuatia kuwepo kwa baadhi ya mafanikio kwenye sekta mbalimbali kutokana na juhudi anazozifanya.
Licha ya matumaini waliyonayo na maendeleo yaliyokwisha patikana baaadhi ya wananchi wamepaza sauti zao kuhusu baadhi ya kero zinazowasumbua a
Mkazi wa Kata ya Lituhi Chogo Wachogo anasema kuwa maji yapo ya kutosha kwenye kata yao ila tatizo linalowasumbua ni miundo mbinu ya kusambazia mtandao wa maji hayo.
Wachogo alisema pia barabara zinapitika vizuri kwa wakati wote tofauti na miaka ya nyuma, hata hivyo amemwomba Mbunge wao ashughulikie suala Usafiri wa uhakika ili wanunuzi wa Samaki na dagaa kutoka Ziwa Nyasa waweze kupata usafiri wa uhakika wa bidhaa zao kuelekea katika masoko.
Kwa upande wa mawasiliano Katibu wa CCM Wilaya ya Mbinga Anastasia Amasy anasema katika kata nyingi za Jimbo hilo kuna mawasiliano ya simu ila katika kata za Chiwanda, Ngumbo ambazo zipo kwenye mchakato wa kujenga minara katika maeneo hayo na ujenzi unaendelea ili wananchi wapate mawasiliano ya uhakika.
Amasy anasema kupatikana kwa wilaya mpya ya Nyasa kutatatua kero nyingi za wananchi katika sekta zote na kusema kuwa wananchi hao wanapaswa kufanya kazi zao kwa bidii kwa lengo la kuijenga wilaya hiyo mpya katika nyanja zote muhimu
Wakati wakilalamikia kero hizo kwa upande wao, wakazi wa Jimbo hilo wamepongeza juhudi zinazofanywa na Mbunge huyo za kupambana kwa dhati dhidi ya masuala yanayoonekana kuwa ni kikwazo kwao na kuelezea jinsi sekta za Barabara, Afya, Maji, Elimu, Mawasiliano zilivyopiga hatua kwa kiwango kikubwa.
Kwa nyakati tofauti walisema kuwa toka Dunia iumbwe hawajawahai kumpata Mbunge anayewajali na kuwathamini kwa kusaidiana naye kuleta maendeleo kwa wananchi ambaye kwa muda wote anakuwa jimboni na wananchi wake ama kweli Kapteni Komba anapaswa kuwa "Mbunge wa Muyaya" yaani Mbunge wa milele
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Kanali Mstaafu Edmund Mjengwa alisema Kapteni Komba amejitahidi sana kutatua kero za wananchi wake hivyo anapaswa kupongezwa sana kwa juhudi zake alizozionyesha katika kipindi cha uwakilishi wake wa miaka sita hii
Mjengwa alisema katika kipindi hicho Kapteni komba amefanikiwa kuwaletea wilaya mpya ya Nyasa ambayo ndio itakayokuwa nguzo muhimu katika kuimarisha sekta za uchumi, mawasiliano, barabara, elimu, afya na maisha bora kwa wananchi wa wilaya hiyo ambao shughuli zao kubwa ni kilimo cha kahawa, mihogo, mahindi, ulezi na uvuzi wa samaki na dagaa kutoka ziwa nyasa
Mkuu huyo wa Wilaya amewataka wananchi wa jimbo hilo la Mbinga Magharibi waipokee kwa shangwe wilaya hiyo mpya ambayo inafaida kubwa sana kwao na kuwataka waongeze bidii katika kilimo,uvuvi na kutenga maeneo ya uwekezaji na uzalishaji mali ili waweze kufaidi matunda ya wilaya yao mpya
Hata hivyo akijibu kero zilizoainishwa na wapiga kura wake kwenye Mkutano wa Kata ya Kilosa, Mbunge wa jimbo hilo Kapteni Komba amesema katika kipindi cha miaka mitano ya uwakilishi wake nimejitahidi kutekeleza ahadi muhimu nilizowaahidi ambazo zilikuwa kikwazo kikubwa kwa maendeleo na kero kubwa kwa wakazi wa Jimbo hilo.
Anasema wananchi wa jimbo hilo walimchagua na kumpa dhamana ya kutatua kero mbalimbali zinazowakabili wakijua kuwa yalipo maji ya uzima napajua, hivyo pamoja na kuwaletea huduma muhimu kama Maji, Barabara, Afya, Elimu, Kufufua mazao ya biashara kama Kahawa, Korosho na kuwatafutia masoko ya uhakika,nilijitahidi kutekeleza ahadi zangu kwa 90% kwa kipindi changu cha miaka mitano iliyopita 2005/2010
Kwa upande wa mawasiliano ya simu na miundombinu ya maji barabara kwa baadhi ya maeneo amewaomba wapiga kura wake wavute subira kwani tayari utekelezaji wake upo kwenye mchakato ingawa amesema upatikanaji wa Wilaya mpya ya Nyasa ambayo imetangazwa rasmi utachochea kasi ya maendeleo katika jimbo lake
Komba anasema amejitahidi sana kutatua kero za wananchi wake katika kipicha cha uwakilishi wake na anaishukuru serikali ya awamu ya nne kwa kusikiliza kilio chake cha kupatiwa wilaya hiyo mpya kwani sasa maendeleo ya wanambinga magharibi yatakuwa makubwa kwani nao watafaidika na bajeti ya Serikali kama wilaya zingine
Aidha amewaomba wapiga kura wake wawe na ushirikiano stahiki katika kutatua kero zilizopo ili kuweza kufikia lengo la maisha bora kwa kila mtanzania ingawa amewata kuipokea Wilaya yao Mpya ya Nyasa ambayo makao makuu wanatarajiwa yawe Mbambabay.
“Naomba wapiga kura wangu watambue kuwa kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita nguvu nyingi nilielekeza kwenye ujenzi wa shule za msingi na sekondari, pamoja na miundo mbinu ya barabara, maji na mawasiliano na mwaka huu namalizia ahadi zangu muhimu katika sekta ya afya ili niweze kufanya tathimini ya miaka saba ya uwakilishi wangu” alisema Komba.
Hata hivyo anasema mafanikio ya mwanasiasa yoyote yule ni kutekeleza ahadi alizo ziahidi kwa wananchi wake kwa wakati stahiki, hivyo ahadi zote alizozitoa ametekeleza kwa ukamilifu kwa sababu yeye sie Mbunge wa uwongo bali wa kweli kwa hiyo hapendi wananchi wake walalamike kwa sababu yeye hakuomba ubunge wa malalamiko bali ni wa utekelezaji kwa yale aliyoyaahidi na kwasababu yalipo maji ya uzima napajua mie kazi yangu nikuyashusha kwa wapiga kura wangu ili waweze kufaidi matunda ya uhuru wa Tanganyika
Mwandishi wa Makala haya
Anapatikana 0755 33 5051
No comments:
Post a Comment