Fratel John Kassembo
Na Stephano Mango,Songea
WATANZANIA tunapaswa kufahamu umuhimu wa Makumbusho ili tujenge utamaduni wa kuyatembelea mara kwa mara tuone na kujifunza mambo ya kale ili kuona jamii zao zilivyokuwa zinaishi kwa muingiliano wenye kujenga jamii imara
Makumbusho ni sehemu ambayo watu wanaweza kujifunza namna ya uhifadhi bora wa mazingira kwa kuangalia watu wa kale walivyoweza kunufaika na mazingira yaliyowazunguka na mali asili zilizokuwepo kwa kupata dawa za miti shamba,chakula na vitoweo
Kupitia Makumbusho wananchi wanaweza kujifunza wajibu wao kwa nchi yao na jamii nzima inayowazunguka kwa kuangalia Mashujaa wa kale waliojitoa kwa moyo kupigana kwa ajili ya uhuru wan chi,ulinzi na usalama wa mali zao
Uwepo wa Makumbusho ni jambo la kujivunia kwani yanaweza kutumika kujenga amani katika jamii ya watu wanaoishi kama ndugu na marafiki kwa kuangalia maisha ya watu wa kale walivyoishi kwa kushirikiana katika mambo yaliyokuwa yanawahusu wao na jamaa zao
Pia ni sehemu ambayo huwakutanisha watu wa mataifa mbalimbali wanaokuja kuzitembelea na kujifunza historian a tamaduni zetu hivyo kuifanya dunia kuwa mahali padogo kwani vitu wanavyojifunza hupelekwa nchi za mbali na kujulikana kwa watu wa mataifa mbalimbali
Nakufanya kuwa kiungo cha mabadiliko na maendeleo ya Taifa kwani kupitia Makumbusho watu wanaweza kujifunza umuhimu wa mabadiliko na umuhimu wa kila mmoja kujiletea maendeleo kwa kuangalia namna mwanadamu alivyopitia hatua mbalimbali za mabadiliko mpaka kufikia hatua tuliyopo hivi sasa
Kukuza amani na kuchangia kwa ufanisi zaidi katika kujenga amani Dunia, Makumbusho yanaweza kuandaa midahalo, kuonesha filamu, jitihada za utafiti, matembezi, mikutano ya amani na maonyesho ya utalii
Ni sehemu ambayo huvuta watalii,hukuza sayansi,hushangaza/kustaajabisha,kuelimisha,kuburudisha na hutia chachu ya uwajibikaji kwani ndani yake yana kumbukumbu zilizohifadhiwa hivyo makumbusho ni historia inayoishi
Akizungumzia umuhimu wa Makumbusho ,Mwezeshaji na mtoa mada wa mambo ya uongozi, dini, vijana, falsafa, ujasiriamali na amali za maisha John Kasembo alisema kuwa kumbukumbu ni wasaa wa kutafakari sisi wenyewe maisha yetu hivyo tunapaswa kuweka juhudi za kutunza makumbusho zetu
Kasembo alisema kuwa suala la kutunza Makumbusho ni tete kulibinafsisha kwani linabeba utamaduni na utambulisho wa Taifa au jamii husika, hivyo zinawezwa kutunzwa na mtu binafsi kwa maendeleo yake, taasisi au Taifa
Alisema kuwa mchango wa Tanzania kwenye tamaduni za nchi za Ulaya haupo na haujulikani , ingawa kila siku tunaendelea kutothamini utamaduni wetu kwa kuendelea kuiga tamaduni za nje bila sababu za msingi
Alieleza kuwa utamaduni wa Tanzania unastahili kukuzwa,kutangazwa na kusimamia ili nasi tuweze kuchangia utamaduni wetu kwenye mataifa mengine na ustaarabu wa ulimwengu, hivyo utambulisho binafsi na wa pamoja, kati ya kumbukumbu na historia
Alieleza zaidi kuwa Makumbusho ni benki ya kumbukumbu licha ya kuwa sehemu ya kuelimisha na kuburudisha, pia makumbusho ni kumbukumbu ya fikra, kazi,maisha,mtazamo wa matukio na watu
“Waafrika wengi hatuna utamaduni na hatujalelewa, uvivu, malezi, elimu, ndio gharama za kutunza kumbukumbu binafsi na ndilo hata tatizo linaloikumba Taifa, jambo ambalo linapaswa kurekebishwa”alisema Kasembo
Alieleza kuwa wadau wa utamaduni na wataalamu wa makumbusho wanahitajika kukutana na watu ili kuweza kuelezea maana na kutetea nafasi ya makumbusho kwasababu makumbusho zipo kwenye moyo wa mfumo, taasisi zinazohudumia na kuendeleza jamii
Alieleza kuwa ni njia muhimu ya kubadilishana utamaduni,kutajirishana tamaduni, kustaajabia tamaduni na maendeleo ya maelewano ya pamoja, ushirikiano na amani kati ya watu kwani yana kumbukumbu muhimu kwa jamii na zaidi ni chachu ya maendeleo ya jamii
Alifafanua kuwa akumbusho yanakusanya vitu vyenye umuhimu wa kisayansi,kijamii na kihistoria ili kutunza, kusoma, kutafsiri mambo mbalimbali ili kizazi kijacho kiweze kutukumbuka kwa kulinganisha yaliyopita nay a wakati huo
Ni ukweli uliodhahiri kuwa kumbukumbu ni muhimu isivyodhanika kwa maendeleo na ustawi wa utunzaji wa taifa, taasisi au mtu binafsi, hivyo zinapaswa zitunzwe,zikuzwe,zistawishwe,zielezwe na ziandikiwe maelezo
Uaminifu katika utunzaji ni muhimu kwani kuna hatari kubwa ya kuweka kumbukumbu ambazo zimebeba uongo ndani yake na nje zimevishwa sura ya ukweli kwasababu tunaandaa siku mbaya kwa kizazi chetu kijacho
Historia ni mwalimu mzuri kwa sababu ili uweze kutafsiri na kuyaelewa yanayotokea sasa na kuyaelewa yatakayotokea kesho, tuna lazima ya kuangalia na kutafsiri kilichotokea jana
Watanzania tunayo fursa nzuri ya kuutafakari na kuutathimini utamaduni wetu na hivyo kujitahidi kuutunza, kuulinda, kuuboresha, kuukuza na kuusambaza kwasababu nchi isiyo kuwa na utamaduni ina kosa mizizi ya kusimamia
Utamaduni ni roho ya Taifa na tunu yetu tuutunze ili tuweze kujivunia na kuchangia kwenye ustaarabu wa ulimwengu katika muunganiko wa tamaduni na ustaarabu wa dunia
Hatuwezi kuukimbia udhaifu wetu, lakini tunaweza kupigana nao na tukidhamiria vya kutosha tunaweza kushinda ambapo wakati stahiki ni sasa hapa tulipo kwa sababu uimara wa utamaduni wa kizazi cha sasa na kijacho upo mikononi mwetu
Leo, sisi ni vyombo vya uamuzi wa kutengeneza Taifa lenye afya njema kiutamaduni,mira na desturi kwa kutunza yale yafaayo na kuyarekebisha au kuyaondoa yale yasiyofaa kwa faida yetu nay a vizazi vijavyo
Mtazamo wangu na wako ndio unaotengeneza uhai wa utamaduni na taifa letu, hivyo tuamue kuwa chombo cha mabadiliko kwa kuwaelimisha na kuwahamasisha umuhimu wa utamaduni na makumbusho kwani utambulisho una uwezo mkubwa wa kuakisi maendeleo kusudiwa
Mwandishi wa Makala
Anapatikana 0715-335051
No comments:
Post a Comment