Na Gideon Mwakanosya, Songea
WATU wanne wa Vijiji vya Litolongi na Minango vilivyopo Kata ya Kigonsera Wilayani Mbinga na Mkaya kilichopo Kata ya Lituhi Wilayani Nyasa Mkoa wa Ruvuma wamekufa katika Matukio matatu tofauti yakiwemo ya kupigwa na radi wakati mvua zikiwa zinaendelea kunyesha.
Wametajwa waliokufa kwa kupigwa na radi kuwa ni Manfred Komba (18) na Pascar Ndomba (33) wote wakazi wa Kijiji cha Minango Kata ya Kigonsera na mwingine ni Maria Kinunda (18) Mkazi wa Kijiji cha Litolongi Kata ya Kigonsera Wilayani humo na Martias Charle (52) Mkazi wa Kijiji cha Mkaya Kilichopo Kata ya Lituhi Wilaya mpya ya Nyasa ambaye alikutwa Porini akiwa amekufa.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma Michael Kamuhanda alisema kuwa tukio la kwanza lilitokea January 27 Mwaka huu majira ya Saa 11 Jioni huko katika Kijiji cha Minango kilichopo Kata ya Kigonsera ambako Komba na Ndomba kabla ya kukutwa na mauti walikuwa shambani wakilima.
Alieleza zaidi kuwa wakiwa wanaendelea kulima Majira ya Saa 11 Jioni ghafla manyunyu ya mvua yalianza na baadaye Mvua kubwa iliongezeka huku ikiwa imeambatana na radi ndipo walipoamua kuacha kuendelea kulima kasha wakaanza kukimbilia kwenye kibanda kwa ajili ya kujificha mvua lakini kabla hawajafika kwenye kibanda hicho walipigwa na radi na kufa papohapo.
Kamuhanda alisema kuwa tukio jingine lilitokea January 27 mwaka huu Majira ya saa 12 Jioni huko katika Kijiji cha Litolongo Kata ya Kigonsera wilayani humo Maria alipigwa na radi na kufa papohapo wakati akikimbilia ndani ya Nyumba yake kujificha Mvua.
Alifafanua kuwa Maria mapema inadaiwa kuwa alikuwa akifanya shughuli zake nje ya nyumba yake na baadaye Mvua zilipoanza kunyesha ambazo ziliambatana na radi ndizo zilizosababisha kukatisha Maisha yake kwa kupigwa na radi na kufariki papo hapo.
Wakati huo huo Matias Charle (52) Mkazi wa Kijiji cha Mkaya kilichopo Kata ya Lituhi Wilayani Nyasa ambaye anadaiwa kuwa alikuwa mgonjwa wa akili na ni mlemavu wa mikono na miguu alikutwa porini akiwa amekufa.
Alieleza zaidi kuwa Charle anadaiwa kuwa wakati wa uhai wake Oktoba mwaka jana alitoweka nyumbani kwake na kutokomea kusikojulikana na jitihada za kumtafuta zilifanywa bila kuwepo mafanikio na Juzi majira ya saa 9 alasiri alikutwa porini akiwa amekufa.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment