MENEJA WA TANESCO MKOA WA RUVUMA MONICA KEBARA
Na Stephano Mango,Songea
KUFUATIA kuendelea kuwepo kwa tatizo la umeme la kukatika mara kwa mara katika halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma baadhi ya wananchi wameendelea kuelekeza kilio chao kwa uongozi wa shirika la umeme Tanzania(TANESCO) mkoa wa Ruvuma kwa kushindwa hata kutoa taarifa kwa wateja kuhusu katizo hilo ambalo limeonekana kukithiri.
Uchunguzi uliofanywa na www.stephanomango.blogspot.com kwa zaidi ya mwezi mmoja umebaini kuwa baadhi ya maeneo ya mji wa Songea yamekuwa yakipata huduma hiyo kwa kiasi kidogo ikiambatana na mgawo usioweza kuelezwa kwa sababu baadhi wamekuwa wakipata huduma hiyo usiku wa manane na alfajiri umeme unakatwa jambo ambalo limesababisha malalamiko mengi ya wateja dhidi ya shirika hilo mkoani Ruvuma.
Uchunguzi huo pia umebaini kuwa katika taasisi za afya ikiwemo hospitali ya Serikali ya mkoa na kituo cha afya cha Mjimwema zimelazimika kutafuta namna nyingine ya kupata nishati ambayo inapaswa kutolewa na shirika la umeme mkoani humu namna hiyo mbadala ya kukabiliana na changamoto iliyofanywa uongozi wa taasisi hizo za tiba kuwa na jenereta kwa ajili ya kuwezesha kuendelea kujitoa huduma wakati shirika la umeme likiwa limekata huduma hiyo.
Baadhi ya mashine za kusaga nafaka ambazo zipo katika baadhi ya maeneo ya Manispaa hiyo zimeshindwa kutoa huduma kwa muda muafaka na kusababisha wananchi walio wengi kulazimika kutembea umbali mrefu kufuata huduma nje ya Manispaa yakiwemo maeneo ya Lilambo,Shule ya Tanga na Mletele ambako kuna mashine za kusaga nafaka zinazotumia mafuta ya Dizeli na kusababisha bei ya huduma hiyo kupanda mara mbili ikilinganishwa na awali.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wamiliki wa mashine za kusaga na kukoboa nafaka wamesema kuwa kitendo cha shirika la umeme mkoani humu kushindwa kutoa huduma hiyo kwa wakati mbali ya kusababisha usumbufu kwao lakini kimekuwa kikiwakosesha mapato ambayo wanayatumia kulipa kodi kwenye mamlaka ya mapato Tanzania(TRA) ambao wanatekeleza wajibu wao wa kukusanya mapato kwa mujibu wa kanuni.
Akizungumza Julius Mlawa(Mtazamo) kuhusiana na hali hiyo alisema huenda akalazimika kusitisha kwa muda kutoa huduma ya usagaji na ukoboaji wa nafaka kama hali hiyo ya ukosefu wa umeme wa uhakika haitafanyiwa kazi na shirika hilo la umeme mkoani humu kwa sababu mbali ya kukosa mapato lakini imekuwa ni usumbufu kwa wananchi ambao wanahitaji huduma hiyo.
Mmoja wa wamiliki wa mashine za kusaga nafaka katika nafaka katika eneo la Manzese ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema kitendo cha shirika hilo kutotoa taarifa ya kuwepo kwa mgawo au katizo la umeme na badala yake limekuwa likikata umeme hovyo na kusababisha uharibifu wa mitambo yao.
Akizungumza kuhusiana na hali hiyo mganga wa mkoa Dkt.Daniel Malekela amesema kuwa wamelazimika kutafuta jenereta kubwa kwa ajili ya kuendelea huduma hiyo muhimu katika hospitali ya mkoa wa Ruvuma iliyopo mjini Songea kwa sababu huduma za upasuaji na maabara zinahitaji nishati ya umeme muda wote lakini shirika halifanyi hivyo na halitoi taarifa ya katizo kwa muda muafaka.
Naye mkurugenzi wa Manispaa ya Songea Nachowa Zakaria alisema kuwa halmashauri hiyo iliangalia uwezekano wa kutatua tatizo hilo kwenye kituo cha afya cha Mjimwema mjini hapa kwa kununua jenereta ambalo linasaidia kwa kiasi kutoa huduma hiyo kwa wananchi walio jirani na kituo hicho cha afya.
Kwa upande wake Meneja wa shirika la umeme mkoa wa Ruvuma Mhandisi Monika Kebara alikiri kuwepo kwa tatizo hilo na alisema hivi sasa huduma hiyo ya umeme inatolewa kwa mgawo kwa sababu uwezo wa ufuaji wa umeme umepungua sana kutokana na kuharibika kwa mitambo ya kuzalisha umeme iliyopo Kibulang,oma mjini hapa.
Alisema kituo hicho kina mashine saba za kuzalisha umeme lakini kwa hivi sasa ni mashine tatu ndizo zinazofanya kazi hiyo kwa kutoa Megawati 2.6 wakati mahitaji ni Megawati 5 hasa ikizingatiwa kuwa katika mji wa Songea shirika hilo lina wateja elfu kumi na mbili.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment