About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Wednesday, May 23, 2012

AZIMIO LA ARUSHA, MWAROBAINI PEKEE ULIOBAKI


 
Paschally Mayega
RAIS wangu Kikwete, nalilia Azimio la Arusha sasa kuliko wakati mwingine wowote! Kuachwa kwa baadhi ya mawaziri kumeibua mambo ya kuogofya ambayo yanaweza yakatupeleka kwenye mwisho wa aibu kubwa!

Baadhi ya wananchi wa Jimbo la Moshi Vijijini wanasema mbunge wao hakutendewa haki kuachwa katika baraza la mawaziri.

Raymond Assenga, mmoja wa wananchi hao alisema, “Mwaka 2010 Chami alituunganisha, tukachanga zaidi ya milioni 50 kusaidia kampeni za Rais”.

Hili ndilo neno linalotakiwa litolewe ufafanuzi. Zilichangwa milioni 50 kama bei ya kuununua uwaziri? Uwaziri 2010 ulikuwa unauzwa? Hii ikithibitika, itakuwa ni kashfa kubwa!

Kama hivyo ndivyo, je, wale mawaziri wawili ambao nao walituhumiwa kama mbunge wao Cyril Chami lakini wao wamo watakuwa walichangia shilingi ngapi? Ukiifikiria sana hali hii damu inaweza ikakusimama mwilini, hebu tuifikirie kwa kibonzo hiki.

Uongozi wa Kampuni moja tajiri sana duniani, mabingwa wa kutengeza chapati walitaka kuweka tangazo la chapati zake katika sehemu litakakosikika dunia nzima.

Wakakusanya masanduku mengi yaliyojaa fedha nyingi wakampelekea Baba Mtakatifu, Papa, wakimwomba awaamuru Wakristu wote duniani, wanaposali sala ya Baba yetu uliye mbinguni, badala ya ile sentensi wanayosema, ‘utupatie leo mkate wetu wa kila siku’, waseme, ‘utupatie leo chapati yetu ya kila siku’.

Baba Mtakatifu alipozikataa hela nyingi kiasi kile, Jamaa walizimia. Eti walishindwa kuelewa ni kiasi gani cha fedha kampuni ya kutengeneza mikate ilimpatia Baba Mtakatifu mpaka akakubali mkate utangazwe katika sala ya Baba yetu.

Rais wangu sasa inanijia akilini, wakati Jumanne Maghembe akiwa waziri wa Elimu, wadau wa elimu walifanya kila waliloweza kumwambia kuwa mtindo wa kitabu kimoja cha kiada pamoja na kwamba ni kuua elimu nchini lakini huko ni kuchochea rushwa kubwa kabisa!

Alikuwa mbogo mtu huyu sijapata kuona mfano wake. Lakini ni kweli kulikuwa na minong’ono mitaani kuwa waziri aliagizwa kuandaa mazingira ya uchaguzi mkuu 2010.

Kama naye alichangia, atakuwa alichangia kiasi gani mpaka abakishwe? Natamani hii isiwe kweli! Inapofikia watu wanauza mpaka elimu ya nchi nzima, ni kipi wanakuwa wamebakisha cha kuutambulisha utu wao? Mavazi tu!

Kama watu walilipia uwaziri nani atakuwa na ubavu wa kuwaamuru mawaziri hao? Utajikuta unalazimika kuunda baraza la mawaziri kubwa kuliko mahitaji halisi ya nchi. Hili tumeliona mara zote! Kulipa fadhila!

Hawa ni mawaziri. Kuna wakuu wa mikoa na wilaya. Au ndiyo sababu uteuzi wa wakuu wa wilaya imechukua miaka miwili? Yawezekana pia ikawa ni sehemu ya sababu ya kuongeza mikoa na wilaya? Tuendako, siko!

Mwenyekiti wa chama cha wananchi (CUF) Profesa Ibrahim Haruna Lipumba alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam, Aprili 24 mwaka huu alisema, “Tatizo la ubadhirifu haliwezi kwisha katika serikali ya awamu ya nne maana tatizo siyo watendaji wala mawaziri, ni Rais Kikwete mwenyewe…amekuwa ni mtu asiyekuwa na uamuzi.”

Alisema, “Haishangazi kuona mawaziri katika wizara moja hawaelewani. Kuna mawaziri wana nia njema na wanasimamia haki, lakini hata wakitoa mapendekezo yao yanapuuzwa.

Na wapo wanaotumia nafasi zao vibaya huku rais akiendelea kuwachekea.” Nadhani ufunuo wa hapo juu ulikuwa haujamfikia. Utamfanya nini mtu aliyejilipia?

Naye Katibu Mkuu wa CHADEMA Dk. Willibrod Slaa akihutubia mkutano mkubwa wa hadhara katika viwanja vya Sahara Aprili 22 mwaka huu jijini Mwanza alisema, ”Uozo uliofanywa na mawaziri umekuwa ukipata baraka zake, kama

Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri na amekuwa na kawaida ya kulinda ubovu wa mawaziri wake kutokana na udhaifu wake mwenyewe wa kiuongozi.” Maskini Mwalimu Nyerere hakujua kama Ikulu kuna biashara. Nyumba ya baba yangu itageuzwa pango la walanguzi!

Dk. Slaa aliendelea kusema, “Kikwete ndiye chanzo cha udhaifu wote serikalini unaosababisha matatizo makubwa kwa taifa na kwa wananchi”. Huenda rais wetu si dhaifu kiivyo ila ikawa ndiyo hitaji ya mazingira ya biashara iliyofanyika.

Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa hivi karibuni alikaririwa akisema, “Muundo na imani ya chama cha mapinduzi ni mzuri. Tatizo ni uongozi katika utendaji. Ni dhaifu mno katika kufanya maamuzi.

Mara nyingine yamefanyika maamuzi yasiyo sahihi na wakati mwingine maamuzi yakifanyika yanafanyika yakiwa yamechelewa mno kiasi cha kuyafanya yaonekane ni maamuzi yasiyo na maana yoyote”.

Kama hawataki kukosolewa, watatakaje kujirekebisha? Mtu huyu alishiriki kikamilifu kuwaletea Watanzania uongozi wa awamu ya nne, inawezekana vipi asiujue udhaifu wa waliokuwa washirika wake?

 Lakini Edward Lowassa, kama alivyo Abdulrahman Kinana lazima wajue kuwa wana deni kubwa kwa Watanzania kutokana na maisha magumu waliyonayo sasa ambayo ni matokeo ya uongozi walioupigania.

Ndugu Rais wakati wa kuja mwaka 2005 ulikuja na Edward, ilibidi wakati wa kuondoka uondoke na Edward vinginevyo wananchi wataamini maneno ya Dk. Slaa kuwa, “Ni kiongozi anayekwepa lawama na kubebeshwa mzigo wa uzembe wake kwa watu wengine”.

Mlianza vema kwa maagizo mfululizo yaliyokuwa yanatoka Dar es Salaam kwenda mikoani, wilayani hadi vijijini. Hakukuwa na mzaha. Hali hii ilipelekea pia mateso fulani kwa baadhi ya wananchi na hasa pale viongozi wa vijijini walipojaribu kukabiliana na kasi ya maagizo katika shughuli za maendeleo hasa ujenzi wa shule za kata. Watu walinyang’anywa mifugo yao na madhila mengine mengi.

Msingeweza kuepuka kufanya makosa kwa sababu nyinyi nanyi ni wanadamu, lakini mlijijengea heshima kwa wananchi kwasababu kila tulipoandika kukosoa utendaji wenu mlifuatilia na kuchunguza na ilipobidi mkasahihisha bila kusubiri mateso kwa watu wenu kuzidi.

Tofauti na sasa ambapo huwezi kuthibitisha kama wanasikia au hawasikii. Kama hawasomi haya tuandikayo ni kwa hasara yao wenyewe kwasababu wananchi wanasoma.

Richmond ni matokeo ya viongozi kutaka kufanya biashara. Haya ndiyo makatazo yaliyomo katika Azimio la Arusha. Baba waambie watu wako, ‘mnahofia nini’ na Edward Lowassa kuhusu Richmond?

Tofautianeni lakini tambueni kuwa siku ya hukumu wananchi watawahukumu pamoja!
Kutokana na mparaganyiko wenu wahuni wachache wametumia fedha na raslimali nyingi za nchi kwa kisingizio cha kupinga ufisadi na gamba!

Aliyeileta Richmond alitenda dhambi kubwa. Waliowabebesha watu wengine dhambi ya Richmond walitenda dhambi kubwa zaidi na ndiyo maana hawana amani katika vifua vyao siku zote.
Wasipotubu, itawawewesesha usiku na mchana mpaka siku yao ya hukumu itakapowafika!

CHADEMA wamesema watazingatia Ibara ya 8 ya katiba waende kwa wananchi ili ipigwe kura ya kutokuwa na imani na Rais. Nchi imekwama. Tutatokaje hapa tulipokwama? Baba hakuna tulichoachiwa hapa cha kuchagua.

Kuiepusha nchi isiingie katika vurugu tulirejelee Azimio la Arusha ili tuanze upya! Nchi imevurugwa kupita maelezo.

Rais wangu nchi iko katika mchakato wa kuandika katiba mpya. Hili ni jambo jema sana. Lakini tunataka katiba mpya, ili iweje? Katiba mpya haiwezi kutuletea chakula wala maisha bora.

Katiba mpya itashusha bei ya vyakula? Bila uongozi makini, imara katiba mpya itafaa vipi? Swali hapa ni je, tunaye msimamizi imara wa kusimamia hiyo katiba mpya?

Katiba tuliyonayo ndiyo ileile aliyokuwa akiitumia Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wakati wa urais wake.

Ni katiba ileile aliyokuwa anaitumia Rais wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi na Benjamin William Mkapa, Rais wa awamu ya tatu ukiacha marekebisho madogo madogo ya hapa na pale.

Imewezekanaje imekuwa mbovu kupindukia ghafla tu katika awamu ya nne?
Katiba hii hii na ubovu wake huu huu usingekuwa kero kubwa kwa nchi kama inavyoonekana sasa, kama Azimio la Arusha lingekuwapo.

Maadili na miiko ya uongozi viliyokuwa vimezingatiwa ndani ya Azimio ya Arusha visingeruhusu hali hii kufikia hapa.

Rais wangu ni mengi yamesemwa na kuandikwa juu ya Azimio la Arusha. Hata wakati fulani Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alisikika akisema, “Kila ninapotembea mfukoni mwangu ninakuwa na vitabu viwili. Biblia Takatifu na Kijitabu cha Azimio la Arusha”.

Mwalimu Nyerere alilienzi Azimo la Arusha kama sala. Wakati akiwa madarakani Nyerere hakuchoka kulihubiri Azimio la Arusha kwa watu wake. Alifanana na mitume na manabii waliohubiri habari njema kwa mataifa.

 Nchi ilitulia. Upendo na mshikamano kati yetu vilistawi kiasi cha kutufanya tushindwe kutambua tofauti zetu.

Ndani ya Azimio la Arusha wote tulikuwa ndugu na tuliitana ndugu toka mkuu wa nchi mpaka mponda kokoto! Tukajivunia amani ya kweli ilikuwa imetamalaki nchi nzima hadi vifuani mwetu! Nje ya Azimio la Arusha tuna waheshimu wezi na mafisadi. Mungu atawalaani wote!

Nyerere alipong’atuka manyang’au wakalihujumu hata wakalifuta. Yeyote aliyeshiriki kuliua Azimio adhimu la Arusha, Jua la Mwenyezi Mungu limwakie na siku yake ya mwisho ikifika raha ya milele hataipata wala mwanga wa milele hautamwangazia!

Mwalimu alilia! Akiwa amesimama mbele ya mkungu uliokuwapo mbele ya nyumba yake alimtazama katibu mkuu ofisi ya rais, akageuza uso wake na kumwangalia kwa muda Waziri wa Nyumba na Maendeleo Mijini, Edward Lowassa, kisha akasema, “….na nyinyi wengine, mkilivunja Azimio la Arusha kabisa kabisa, mtakuja kupata taabu sana baadaye.”

Wakati huu ndiyo naelewa ni uchungu kiasi gani Mwalimu alikuwa nao moyoni mwake wakati akitamka maneno hayo! Aliiona Tanzania ya bila Azimio la Arusha! Aliwaona viongozi wetu wa bila Azimio la Arusha, kisha akaiona dhiki kuu itakayowashukia watu wake kwa kukosekana Azimio la Arusha! Akasema, “Mtakuja kupata taabu sana baadaye!”

Naye akisha kuyasema hayo aliondoka katika eneo la mkungu tulilokuwapo, akaingia ndani katika kiofisi chake cha pale nyumbani kwake, Msasani. Alikuwa mtu mzima lakini unamwona anaingia ndani akiwa amechoka kabisa si kwa uzee bali kwa kuwahurumia watu wake maskini ambao sasa nadhani aliwaona wamebaki yatima.

Baadhi ya watu waliitwa ndani wakaongee faragha na Mwalimu. Nami pia niliitwa. Mwalimu hakuwa na mengi ya kusema zaidi ya kulalamika tu, kitu ambacho kilinifanya nijue kuwa alikuwa anaumizwa sana na jinsi viongozi wa serikali walivyokuwa wakiongoza.

Naikumbuka siku ile kama vile ilikuwa jana. Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere akitumia mkono wake wa kulia alimshika Edward Lowassa mkono wa kushoto maana walikuwa wamekaa sambamba, akamtamkia maneno mazito usoni mwake katika sentensi tatu! Maneno yale kutoka katika kinywa cha Mwalimu yaliniingia na kuninyong’oneza kabisa, utadhani nilikuwa naambiwa mimi!

Aliyoendelea kusema Mwalimu nilibaki nasikia tu lakini nilikuwa sielewi kitu tena mpaka tulipoondoka!

Ndugu Rais, acha mimi leo nilililie Azimio la Arusha! Siku nyingine Mwenyezi Mungu akipenda nitakwambia maneno ambayo Baba wa Taifa aliyomtamkia Edward Lowassa usoni pake!

Nayakumbuka maneno yale, nukta kwa mkato! Edward alimjibu Mwalimu kwa unyenyekevu mkubwa.

Nyakati zimepita na sasa zimetimia. Siku za majaribu zinawasonga Watanzania, wakumlilia hawamwoni.

Viongozi wetu ndio hawa wa kununua na kuuza uongozi. Mwalimu Nyerere aliwatabiria dhiki kuu watu wake baada ya yeye kuuondoka ulimwengu huu wa mateso!

Leo Watanzania wanaporwa kila kitu! Wamebaki kuchechemea kwa ugumu wa maisha huku viongozi wao na familia zao wakiwa katika ukwasi wa kutisha!

Wananchi wamefanywa kama kuku wa kienyeji. Wanaachwa wajilishe wenyewe, jioni warudi. Mpaka siku wanapotakiwa kuchinjwa ndipo wanatupiwa mtama kidogo! Kapelo, fulana, kanga na buku mpaka uchaguzi ujao!

Aliposikia viongozi wa Tanzania wanapokewa kwa shangwe duniani kwa uhodari wao wa kuuza ardhi, Mwanamwema Anney Anney alinitumia ujumbe uliosomeka: “Nilikaa Segerea miezi 5. Nikaendesha kesi mwaka mzima, nikashinda! Kisa nilisema Jakaya Mrisho Kikwete anauza ardhi yetu pamoja na utu wetu kwa Wazungu na Wahindi.

Leo (18-5-2012) BBC asubuhi wametangaza, Tanzania inaongoza kwa kasi ya kutisha kuuza ardhi kwa wageni katika ukanda wa Afrika Mashariki. Ni Mayega tu aliyenisemea nikiwa jela! Kosa langu lilikuwa ni nini?”

Mwanamwema Anney Anney endeleeni kuomboleza. Kilio cha wenye haki Mungu anasikia! Alisikia kilio chako ukiwa gerezani! Akasikia na sauti yetu tuliyomlilia, leo uko huru nao watesi wako wameandaliwa anguko la aibu!

Siku zimekaribia ambapo milango ya Magereza itafunguka na wote walioko nje bila kuwa na haki wataingia humo, nao wenye haki waliokuwa ndani watatoka, kwa maana mtetezi wetu yu hai!

Rais wangu, warudishie Watanzania Azimio lao la Arusha upate heri na miaka mingi hapa duniani. Nanyi wana wa nchi hii yawapasa kufahamu kuwa wakuwakomboa hakuna.

 Yawalazimu mjikomboe nyinyi wenyewe. Yeyote anayekuja kwetu kutaka kutuongoza aje na ahadi ya Azimio la Arusha.

Bila hivyo naye hatufai! Nchi yetu kwanza! Vyama vyote vya siasa na uzuri wa viongozi wake baadaye! Kuendelea kulialia tu na kulalamikalalamika bila

Azimio la Arusha katika nchi hii, ni sawa na kung’ang’ana kunyoosha kivuli cha mti uliopinda! Azimio la Arusha, ndiyo mwarobaini pekee uliobaki! Mwenyezi Mungu awabariki nyinyi wote!
 

No comments:

Post a Comment