About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Tuesday, July 3, 2012

RAIS TUEPUSHE NA LAANA HII

 
KAMA kuna neno zito lenye hekima na busara lililotolewa na Rais Jakaya Kikwete, ni kauli yake ya kuwaomba madaktari waliogoma warudi kazini ili kuwahudumia wagonjwa.
Rais alipolihutubia taifa juzi, alisema inatia majonzi makubwa pale watu wanaposhuhudia miili ya wapendwa wao ikipelekwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti kwa sababu madaktari wamegoma.
Tunaungana na Rais kwa kauli yake hiyo ya kuwasikitikia wananchi huku tukihoji ni kwa nini mgogoro baina ya madaktari na serikali unaendelea kama kuna dhamira ya dhati ya kuwahurumia watu?
Tunasema hivyo tukiamini kuwa ni fedheha kwa serikali inayojifanya kuwa na huruma kuendelea kuvutana, kutambiana na kutoa kauli za ubabe na vitisho kwa madaktari ambazo mwisho wake ni unyama kwa wananchi maskini.
Rais kama mkuu wa nchi na amiri jeshi mkuu wa vyombo vya ulinzi na usalama alikuwa na kila sababu ya kuhakikisha anapata taarifa sahihi kuhusu madai ya madaktari na kisha kupanua mjadala nao ili kuepusha mgomo.
Ni dhahiri kuwa hatuungi mkono madaktari kugoma wakati wananchi wanapoteza maisha, lakini hoja yetu ni kwamba ufafanuzi wa Rais Kikwete na msimamo wake juzi kwa taifa, alipaswa kuutoa na mapema kabla mgomo haujaanza.
Katika vuta nikuvute hii, tunashangazwa na ukimya wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (TUGHE) chenye dhamana ya kuitisha mgomo kwa sekta hiyo badala yake tumeachwa kwenye ombwe la danadana baina ya Chama cha Madaktari (MAT) na Jumuiya ya Madaktari.
Tumeona migogoro kadhaa iliyofukuta huko nyuma iliyowahusu wafanyakazi wa Kampuni ya Mawasiliano (TTCL) ilishughulikiwa na TEWUTA na NBC kina TUICO walionekana sana katika kutatua mgogoro na kufikia hatua nzuri.
Tumeona jinsi mgogoro ya kimaslahi baina ya Wafanyakazi wa Reli na Serikali, chombo chao cha wafanyakazi (TRAWU) hakikukaa pembeni ndio maana tunajaribu kuangalia kwa kina hawa kina TUGHE hawana uhusiano wowote na madaktari?
TUGHE walipaswa kutoa msimamo kwa umma kueleza ama wanaunga au hawaungi mkono mgomo wa madaktari kwa kuwa umeanzia ndani ya umoja wao wa kitaaluma na kwamba wamekiuka au wamefuata ipasavyo sheria za kazi.
Tunasema hivyo kutokana na ukweli kwamba wananchi hawahitaji kujua nani anapaswa kuitisha mgomo baina ya jumiya na MAT, isipokuwa wanataka kupata huduma bora za afya.
Hivyo mwenye dhamana ya kusimamia hilo la huduma bora za afya ni serikali. Na ndiyo maana tunaiona kauli ya Rais Kikwete kwa madaktari kuwataka wasioweza kupokea mishahara ya serikali waache kazi, imechelewa.
Kwa maana hiyo Rais angefanya kila mbinu ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha TUGHE ili kumaliza mivutano baina ya serikali na madaktari.

Chanzo Tanzania daima

No comments:

Post a Comment