About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Thursday, July 26, 2012

URAIS WAMTESA ZITTO KABWE

<>
<>
<><>
<>
<>
Asema ana uwezo,uadilifu kuwa Amiri Jeshi Mkuu
Na Edson Kamukara
HARAKATI za kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwaka 2015 umeanza kuwatesa viongozi wa vyama vya siasa ambapo safari hii, Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA (Bara), Zitto Kabwe, amesema kama akiandikiwa kuwa rais hakuna wa kumzuia.
Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini alijitapa kuwa kama urais upo, utakuja tu, kwani ana uwezo, uadilifu na uzalendo wa kuwa Amiri Jeshi Mkuu.
Zitto ameibuka na kuzungumzia sakata la urais ikiwa ni siku moja tu imepita baada ya wabunge wenzake kulalamika na kukanusha taarifa za kumpigia debe kwa ajili ya urais mwaka 2015.
Wabunge hao, Halima Mdee (Kawe) na Joshua Nassari (Arumeru Mashariki), waliandika barua za kulalamikia habari iliyochapishwa na gazeti moja la kila siku (si Tanzania Daima), wakidai liliwalisha maneno kuwa walimpigia debe Zitto wakiwa mkoani Kigoma kwamba anapaswa kuwa rais mwaka 2015.
Akichangia mjadala wa hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya Wizara ya Mawasilaino, Sayansi na Teknolojia jana mjini hapa, Zitto alitumia muda mfupi kufafanua sakata hilo lililozagaa kwenye vyombo kadhaa vya habari na kwenye mitandao ya kijamii.
“Tamasha letu la wasanii la Kigoma limeleta maneno maneno…lakini napenda kusema kuwa urais kama upo utakuja tu. Sina mashaka hata kidogo kwamba uwezo, uadilifu na uzalendo wa kuwa Amiri Jeshi Mkuu ninao,” alisema Zitto na kushangiliwa na wabunge wenzake.
Mjadala huo ulichukua sura mpya kwenye mitandao ya kijamii juzi ambapo baadhi ya watu walionekana kumlaumu Zitto, wakimhusisha na habari hiyo kuwa aliitengeneza mwenyewe kama sehemu ya kujiandalia mazingira hayo.
Zitto ambaye amekuwa akiandamwa mara kadhaa na wanasiasa ndani na nje ya chama chake, baadhi wakimtuhumu kuwa mamluki na wengine wakimwelezea kuwa ni mwanasiasa mwenye malengo makubwa hapo baadaye, alifafanua zaidi suala hilo kwenye taarifa yake kwa kusema:
“Katika gazeti la Mwananchi la tarehe 23 Julai 2012, kulikuwa na habari yenye kusomeka: ‘Wabunge wamsafishia Zitto njia ya urais 2015?. Habari hii imeleta mjadala mara baada ya kutoka na kusomwa. Mjadala umekuzwa zaidi baada ya wabunge, Halima Mdee na Joshua Nassari kukanusha maneno waliyonukuliwa kusema. Napenda kusema masuala yafuatayo:
“Moja, waheshimiwa wabunge Halima Mdee, Joshua Nassari, Kangi Lugola, Esther Bulaya, Deo Filikunjombe, Raya Ibrahim, Amina Mwidau na David Kafulila walihudhuria tamasha la vijana wa Kigoma All Stars kwa kualikwa na Mratibu wa kundi hilo, Mwasiti Almasi.
“Wabunge wengine walialikwa lakini hawakutokea wakiwamo Joseph Mbilinyi, David Silinde, Amos Makala, Vicky Kamata na Peter Serukamba. Wabunge hawa hawakualikwa na mimi na wala sikufanya mazungumzo nao yoyote ya awali au kuwaambia au kukubaliana nini cha kuzungumza au hapana. Tamasha lilikuwa la muziki na halikuhusika kabisa na siasa.
“Waheshimiwa wote walipewa nafasi ya kusalimia na wote walizungumza. Wabunge waliozungumza kwa muda mrefu kidogo ni ndugu Halima Mdee, Joshua Nassari, Deo Filikunjombe na Kangi Lugola.
“Hotuba za wabunge wote zilirekodiwa kwenye video neno kwa neno na video hizo zitawekwa wazi kwenye blogu yangu kama sehemu ya documentary ya tamasha lile la kihistoria.
“Pili, sikuhusika kwa namna yoyote ile na kuandikwa kwa habari hii iliyozusha mjadala. Wala sikujua kama habari hii ingeandikwa, maana katika ziara ile sikuita mwandishi hata mmoja, maana nilitaka liwe tukio la Kigoma tu.
“Kama mwandishi kaandika mambo ambayo wabunge hawa hawakuyasema basi itaonekana kwenye video hizo. Wabunge wenyewe wanajua kwenye nafsi zao nini walichosema Kigoma na kipi kiliwasukuma kusema waliyoyasema. Nisingependa kuhusishwa kwa njia yoyote ile na matamshi yao, habari iliyowanukuu na hata makanusho yao. Maana mwisho wa siku ukweli ndio utasimama.
“Suala la urais lisitupotezee muda kwani kuna mambo mengi sana ya kujadili kuhusu nchi yetu. Taharuki ambazo watu wanazipata masuala ya urais yanapotajwa zinashangaza sana.
“Chama changu bado hakijatangaza rasmi mchakato wa kupata mgombea urais. Hivi sasa chama hakina mgombea urais mpaka hapo mchakato utakapotangazwa, ambapo wanachama wataruhusiwa kuomba kupeperusha bendera ya chama. Mwanachama wa chama chetu atakaye kubalika na jamii na wajumbe wa mkutano wa uteuzi ndiye atakuwa mgombea wetu. Kwa sasa hayupo na hivyo tusipoteze muda kujadili jambo hili.
“Mzee Thabiti Kombo alituachia usia tunapokuwa tunazungumza. Alisema ‘weka akiba’ si akiba ya fedha, bali ya akiba ya maneno. Tuweke akiba ya maneno. Tusimalize yote.”
Hata hivyo akizungumza na gazeti hili mjini hapa jana mara baada ya Bunge kuahirishwa kwa ajili ya mapumziko ya mchana, Zitto alikanusha tuhuma hizo zinazomhusisha kuandaa habari hiyo akisema ni matusi kwa tasnia ya habari, hivyo kuvitaka vyombo vya habari kutowaendekeza wanasiasa wanaotukana waandishi na vyombo vyao.
“Ni upuuzi kudhani kwamba mimi naweza kuandaa habari kwenye gazeti hilo…nimeshangaa na wewe unaweza kuniuliza jambo hili…unaliamini?” alihoji Zitto.
Kuhusu habari hiyo inayolalamikiwa na wabunge wenzake kuwa ilipotoshwa, alisema kwamba haoni ubaya kwenye habari husika akidai hata hivyo mengi yaliachwa kuliko kuongezwa chumvi. “Hakuna aliyenukuliwa kwa ambalo hakusema. Tamasha zima limerekodiwa kwenye video”.
Kwa muda sasa kumekuwepo na mjadala juu za Zitto kuhusu kauli yake kwamba anautaka urais, jambo liliotafsiriwa kuwa ni mikakati ya kutaka kukivuruga chama chake kwa kikigawa kimakundi lakini Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, amekuwa akisema kila wakati kuwa ajenda yao kwa wakati huu si kujadili nani anafaa kugombea urais 2015 badala yake wanajikita kutatua kero za wananchi.

Chanzo Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment