About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Sunday, November 10, 2013

UBAYA ALETA UBAYA CHUO CHA UALIMU SONGEA





Ni jengo la Utawala ambalo ni Ofisi ya Ubaya Suleiman Salum ambaye ndiye Mkuu wa Chuo Cha Ualimu Songea

HALI TETE CHUO CHA UALIMU SONGEA, WIZARA YA ELIMU YAMBEBA MKUU WA CHUO.

Na, Stephano Mango, Songea

Ni takribani miezi nane sasa tangu nianze kufuatilia  uendeshaji wa chuo cha Ualimu Songea kama kinaweza kuendana na kauli mbiu ya sasa ya Serikali ya Big Result Now (Matokeo Makubwa Sasa)

Nimelazimika kukifuatilia Chuo hicho kutokana na mgogoro mkubwa uliopo kati ya wafanyakazi (wakufunzi) na mkuu wao wa chuo Ubaya Suleiman.

Mgogoro huo umetokana na uongozi mbovu usiozingatia misingi ya uongozi na Demokrasia katika vyuo vya ualimu Tanzania kwani Mkuu huyo wa chuo amekuwa na lugha za matusi,vitisho kwa wafanyakazi na wanachuo, kutopokea ushauri kwa washauri wake, mbinafsi, kutowaamini watendaji wake kwa nafasi alizowateua, kufanya kazi kwa kutumia vyanzo visivyo rasmi, Matumizi mabaya ya fedha za Serikali na vyombo vya usafiri

Pamoja na hayo mkuu huyo wa chuo amediriki kuwapeleka baadhi ya wafanyakazi wake kwenye vyombo vya dola (polisi) (kuwatishia) akiwatuhumu kuwa wanataka kumuua. Baada ya mgogoro huo kutopata suluhu kupitia vikao vya ndani, Jitihada zifuatazo zilifanyika na wafanyakazi wa chuo hicho ili kuleta hali ya amani na utulivu wa chuo;

Tarehe 27/04/2013 walifanya kikao na mkuu wa wilaya ya Songea Joseph Mkirikiti, tarehe 15/05/2013 na tarehe 01/06/2013 walifanya kikao na Bodi ya ushauri ya Chuo, hata hivyo suluhu ya mgogoro huo haikupatikana. 

Kutokana na hali hiyo Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Profesa Sifuni Mchome aliunda tume ya watu watano ikiongozwa na Mkaguzi Mkuu wa shule na vyuo wa nyanda za juu kusini ambaye alifahamika kwa jina moja la Lyapambile, kuja kufanya utafiti wa chanzo cha mgogoro, lakini mpaka sasa tume hiyo haijatoa majibu ya uchunguzi wa jambo hilo 

Tume hiyo haikuishia hapo tarehe 13/08/2013 wafanyakazi walifanya kikao na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu, ambaye baada ya kusikiliza mgogoro huo aliahidi kuleta suluhisho la kudumu mapema iwezekanavyo ili kuleta amani na utulivu(peace and Tranquility) chuoni hapo. 

Lakini cha kushangaza hadi sasa yapata miezi mitatu hakuna kilichofanyika hali ambayo imeendelea kuwavunja moyo wafanyakazi wa chuo hicho.

Licha ya jitihada zilizofanywa, Mkuu huyo wa Chuo Ubaya Suleiman anaendelea kuwanyanyasa wafanyakazi wake na kusema pigeni kelele lakini wakuning’oa mimi hapa hayupo na lugha zingine ambazo sio za ustaarabu anazitoa, na kuwafanya wafanyakazi wenzake wahoji nguvu aliyonayo katika utendaji, mfano wa lugha zake mbovu ni “kwani mizizi yangu ni mirefu”. Kitendo hicho kinawafanya wafanyakazi wa chuo na wadau wengine watilie mashaka juu ya sifa za uteuzi wake kushika nafasi kubwa kama hiyo.

Tunamuomba Waziri wa Elimu na mafunzo ya ufundi Shukuru Kawambwa na Naibu wake Philipo Mulugo kumuondoa mkuu huyo wa chuo madarakani na kumtafutia shughuli nyingine ya kufanya kwa ustawi wa chuo cha ualimu songea, taaluma ya ualimu Tanzania na ili kuleta ufanisi wa kauli mbiu ya serikali ya Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (Big Results Now)  

Sababu zinazopelekea hilo ni nyingi ila kwa sasa nitazitaja chache ili kuweka kumbukumbu sawa, ya kwanza Novemba 1, 2013 Mkuu huyo wa chuo bila kuwasiliana na Mtaaluma wake wa Chuo Maiko Luoga, alidiriki kuwaandikia Barua Wakufunzi kuwataka watunge Mtihani wa Moko wa Ualimu viwango vya Baraza la Taifa la Mitihani(NECTA) kwa lugha ya kejeri hali ambayo imesababisha maudhi na utulivu wa akili miongoni mwa wafanyakazi katika kufanikisha utungaji wa mitihani hiyo

Kitendo hicho licha ya kuwa ni kinyume na utawala bora , lakini pia kimekiuka maagizo ya Bodi ya Chuo ambayo yalitolewa tarehe 28/8/2013 (……. mambo yote yanayohusu fedha yaendeshwe kwa uwazi na ushirikishwaji mkubwa miongoni mwa wanaidara / taasisi kwani inaonekana mambo yanaenda kwa usiri mno).

Sababu ya pili amekuwa na vitisho vingi katika utendaji wake na maneno ya kuudhi dhidi ya viongozi wenzake , mfano wa maneno yake ambayo anayatamka huku akigonga meza kuashiria ubabe na kiburi cha madaraka ni kama vile,(…. Ukiingia ndani ya kumi na nane zangu nakumaliza, Angalieni msije mkaumia wengine tunambavu za chuma, Nipo tayari kuua inzi kwenye kioo cha TV hata kama itavunjika potelea mbalimbali raha yangu ni kuhakikisha inzi amekufa, Mkitoboa mtumbwi nitahakikisha kabla sijazama mimi nawazamisha ninyi kwanza, Angalia wengine watakaanga mbuyu na kuwaachia wenye meno watafune, Amekuwa akitishia kung’oa mtu kwa kumwendea (kumpandia)wizarani ndani ya siku mbili na kumchukulia barua ya uhamisho kwenda vyuo vya pembezoni mwa Tanzania, Mimi nafanya haya hata niking’olewa kwa muda mfupi potelea pote nitakuwa nimejenga historia)

Sababu ya tatu ni kutokuwa na uwazi, ukweli na ushirikishwaji kwa njia ya kidemokrasia miongoni mwa idara zake katika chuo hicho na hasa katika fedha ambazo zinakuja kwa ajiri ya manunuzi ya vitu mbalimbali, fedha ya kuendeshea mafunzo ya ualimu kwa vitendo(BTP)

Fedha hiyo licha ya kuchelewesha kuitoa kutokana na ufisadi wake lakini pia hakuitoa yote na wala hakueleza kwa uwazi na ukweli, hali ambayo haikuwezesha wakufunzi  kwenda kufanya kazi stahiki kwenye maeneo kusudiwa ya kuwatahini wanachuo ambao walikwenda kwenye shule mbalimbali kwa ajili ya mazoezi ya kufundisha kwa vitendo.

Sababu ya nne ni uwezo wake wa kiuongozi kwani kumekuwepo na mashaka mengi katika Wasifu wake wa kielimu na kiutendaji, hali inayopelekea kuendesha Chuo katika misingi binafsi bila kuzingatia Kanuni, Sheria na Taratibu za Wizara.

Kutokana na hayo yote Chuo hicho kimejikuta kikiingia kwenye mgogoro wa muda mrefu na mkubwa na kupelekea shughuli zote za kiutendaji chuoni hapo kutofanyika katika viwango vyenye ubora na kwa wakati na hasa pale anaposafiri mambo huwa yanasimama, kwani mara nyingi utendaji wote anaufanya yeye mwenyewe na wakati mwingine huwa anajiita Chief Accountant na kumuona Makamu wake kuwa hana uwezo wala mamlaka ya kutoa maamuzi kwa mustakabali wa chuo

Ni mengi ambayo nimeyabaini na ushaidi upo wazi kuwa Mkuu huyo wa Chuo hafai kuendelea kuongoza Chuo hicho kwani Wakufunzi, Wafanyakazi na Wanachuo hawana imani nae, na wanafanya mambo mengi bila morari ya utendaji kutokana na mazingira mabovu ya utendaji kazi katika chuo hicho

Nimefanya jitihada za kukutana na baadhi ya Wakuu wa Idara Chuoni hapo na kupata majibu ambayo yanaonyesha ukataji wa tamaa kutokana na mazingira mabovu ya kiutawala ambayo yanaonyeshwa na Mkuu wa Chuo hicho katika kufanikisha mpango mkakati wa matokeo makubwa sasa,

Pia nimebahatika kuwauliza viongozi wa Bodi akiwemu Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo ambaye amejitambulisha kwa jina la H,Lugome naye pia ameonyesha masikitiko makubwa sana juu ya utendaji wa Mkuu wa Chuo hicho

Lakini pia Mkuu wa Wilaya ya Songea Joseph Mkirikiti ambaye pia ameshiriki kusuluhisha mgogoro huo katika kikao chake cha April 27, 2013 lakini ameshindwa na kukata rufaa kwa kulipeleka swala hilo kwa Mkuu wa Mkoa ili aweze kuliingilia kati

Naye Naibu Waziri wa Wizara ya Elimu Philipo Mulugo alipo tafutwa kupitia simu yake ye kiganjani yenye namba  hii 0754315922 alijibu kuwa swala hilo bado halijafika mezani kwake na endapo likifika basi atachukua hatua stahiki za kinidhamu na kisheria dhidi ya Mkuu yoyote wa Chuo ambaye atakwamisha malengo na ufanisi wa kazi nchini

Kutokana na hayo na mengine mengi ni dhahiri kuwa utendaji wa kazi katika chuo cha  Ualimu Songea kilichopo eneo la Matogoro Mkoani Ruvuma wilayani Songea ni mgumu miongoni mwa Wafanyakazi na kusababisha hali ya sintofahamu katika Saikolojia zao na mustakabali wa Elimu ya wanachuo

Ni vema sasa mamlaka zinazohusika zikachukua hatua stahiki za kumaliza mgogoro huo ikiwemo na kumuondoa Mkuu huyo wa Chuo ili kurudisha Amani na Utulivu chuoni hapo miongoni mwa wanajumuia wanaokizunguka chuo hicho ili kuweza kufanikisha mikakati mbalimbali iliyopo nchini ya kuhakikisha kuwa elimu bora inafikiwa nchini hapa

Mwandishi wa Makala hii
Anapatika kwa 0755-335051 AU 0715-335051
Barua pepe,stephano12mango@yahoo.com
www.stephanomango.blogspot.com

Saturday, October 26, 2013

DKT NCHIMBI APIGWA MAWE SONGEA NA MSAFARA WAKE


Waziri wa mambo ya Ndani ya Nchi Dkt Emmanuel Nchimbi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini

Na Stephano Mango,Songea

MSAFARA wa Waziri wa mambo ya Ndani ya Nchi Dkt Emmanuel Nchimbi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini Wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma wapigwa mawe na wananchi waliojitokeza kuzungumzia kero ya daraja la Matarawe ambalo linadaiwa kusababisha vifo vya watu zaidi ya watatu katika mwezi huu wa octoba mwaka huu

Wananchi hao wa kata ya Matarawe  Manispaa ya Songea,wakiwemo waendesha  Pikikipiki maarufu kwa jina la Yebo Yebo  walifunga barabara kwa  zaidi ya masaa mawili na kufanya fujo za kung’oa kingo za daraja  pamoja na kuweka  magogo na mawe  katikati ya daraja na kuchoma matairi moto  ili Mbunge huyo asipite mpaka atoe majibu ya kina kuhusu daraja

Hali hiyo ililazimisha Jeshi la polisi kuwatawanya  wananchi hao kwa kuwafyatulia mabomu ya machozi kwa lengo la kuzuia uharibifu zaidi na kuufanya msafara upite wakati ukirudi kutoka kwenye Mkutano wa hadhara wa Matarawe baada ya kuzuiriwa wakati wa kwenda na wakati wa kurudi ambapo hadi sasa watu nane wanashikiliwa na Jeshi hilo kutokana na vurugu hizo.

Tukio hilo limetokea jana kati ya saa kumi  hadi saa kumi na mbili jioni  ambapo wananchi hao wakiwa na hasira walifanya fujo hizo  wakiwa na lengo la kumshinikiza Mbunge wa Jimbo la Songea  mjini ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Dkt.Emmanuel Nchimbi  awasaidie kupanua daraja  la mto Matarawe ambalo ni dogo kwani kwa  muda mrefu limekuwa likisababisha ajalli mara kwa mara katika eneo hilo kutokana na ufinyu wa daraja hilo.

Awali  Mbunge huyo akiwa katika ziara yake ya siku ya pili akitokea  mtaa wa Liumbu kata ya Mletele  kukagua shughuli mbali mbali za maendeleo pamoja na kuzungumza na wananchi akiwa anaelekea kata ya matarawe  kwenye mkutano wa hadhara ndipo alikutana na umati mkubwa wa wananchi wakiwemo  waendesha piki piki  walikuwa wamezuia njia na kusimama njiani ili asikilize kero zao kutokana na watu kufa mara kwa mara ambapo siku moja kabla ya mbunge huyo kufanya ziara kuna kijana aliyetambulika kwa jina la Mashaka Nuhu mkazi wa Matarawe akiwa anaendesha piki piki alitumbukia mtoni na kufariki dunia papo hapo.

Hata hivyo Dkt.Nchimbi alilazimika kusimama na kushuka kwenye gari yake  akiwa ameongozana na viongozi mbali mbali wa  chama na Serikali akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Songea Joseph Joseph Mkirikiti  ambapo Mbunge huyo aliwapa pole kwa ajali zinazotokea na kwa watu ambao wamepoteza ndugu zao alizungumza nao na kuwataka wawe na subira  wakati ombi lao linashugulikiwa, majibu ambayo wanachi hao hawakulizika nayo

“Natoa pole sana kwa msiba na ajali ambazo zimetokea nimewasikia, na ninaahidi  nitawajengea daraja  hili ,kama nimeweza kujenga barabara hii kwa kiwango cha lami bila maandamano wala kufungiwa barabara nitashindwa daraja? hivi ni vitu vinavyozungumzika  hili ni jambo dogo hivyo naomba  twende kwenye mkutano wa hadhara na tutaongea vizuri zaidi , kwani ni kweli daraja ni finyu na linahitaji kufanyiwa maboresho zaidi, ‘alisema Dkt. N chimbi.

Dkt.Nchimbi akiwahutubia Wananchi  kwenye mkutano wa hadhara  uliofanyika kwenye viwanja vya  Shule ya sekondari ya kutwa ya matarawe  amesema,amesikitishwa na tukio hilo kwani tabia hiyo haipendezi ,haikubaliki na haina maadili na aina
tija kama wangekuwa na busara wangefika kwenye mkutano na kutoa kero zao badala ya kufanya fujo ambapo ameliagiza jeshi  la polisi kuwasaka wahusika wa fujo hizo.

Amesema, ni kweli daraja hilo ni dogo ila siyo ustarabu kufunga barabara kwa masaa mawili kwani wamesababisha shughuli mbali mbali za maendeleo kusimama kutokana na barabara hiyo kufungwa  na kwamba tayari ameshamuagiza Mhandisi wa halmashauri ya Manispaa hiyo kufanya tathmini ili kujua gharama zinazohitajika ili liweze kupanuliwa.

Mapema Diwani wa kata ya Matarawe James Makene aliungana na kundi kubwa la wananchi hao na alimweleza Nchimbi kuwa  hiyo ni changamoto ambayo wakazi wa matarawe  wamekuwa wakilia kila mara hivyo wanahitaji msaada wa kupanua daraja hilo ambalo limeonekana kuwa ni kero ya muda mrefu.

Kwa upande wake kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma Deusdedit Msimeki ameeleza kuwa kufatia vurugu hizo tayari watu nane wanashikiliwa na wanaendelea kuhojiwa zaidi ili kuwabaini vinara wengine wa fujo waliowashawishi wananchi kufanya fujo hizo .
MWISHO.

Thursday, October 3, 2013

MASHINE ZA TRA ZAZUA BALAA, WENGINE WASHUSHIANA MKON'GOTO



Na Kenneth Ngelesi

WAFANYABIASHARA mkoani Mbeya wamezua kizaazaa wakigoma kufungua maduka wakipinga agizo la Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) linalowataka kununua mashine za kielektroniki kwa ajili ya kukatia risiti za wateja pindi wanapowauzia bidhaa.

Katika sokomoko hilo lililotokea jana na kusababisha taharuki kwa muda kadhaa, wafanyabiashara hao wanadai kuwa gharama za mashine zitolewe na serikali.

Eneo la Soko la Sido ambalo lina wafanyabiashara wengi na tegemeo katika uchumi wa Jiji la Mbeya, walifunga biashara zao kwa muda usiojulikana.

Kadhia hiyo inakuja siku moja tangu Mkuu wa Mkoa huu, Abbas Kandoro, akutane na viongozi wa wafanyabiashara kutoka Soko la Sido na kuwataka viongozi kuwataarifu wenzao wasitishe mkutano ambao walitaka kuufanya jana katika uwanja wa Shule ya Msingi Ruanda Nzovwe.

Kandoro alifikia uamuzi wa kukutana na viongozi hao baada ya kupata taarifa kupitia gari la matangazo ambalo lilikuwa likipita na kuzunguka katikati ya jiji na kuwataka wafanyabiashara hao kufunga maduka na kufika mkutanoni ili kujadili suala zima la mashine hizo.

Taarifa zinadai kuwa baada ya Kandoro kusikia matanagzo hayo, aliliagiza Jeshi la Polisi kumkamata dereva wa gari hilo pamoja na Mwenyekiti wa Soko la Sido na kuwaweka rumande kwa muda usiojulikana.

Baada ya wawili hao kuwekwa ndani, lilitolewa agizo la kuzunguka tena mitaani kwa kutumia gari hilo ili kuwatangazia wafanyabiashara hao kuwa mkutano huo umesitishwa.

Uamuzi wa kusitisha mkutano huo ulipuuzwa na wafanyabiashara hao ambao jana waliendelea na maandilizi ikiwa ni kukodi gari jingine la matangazo kupita mitaani kuwahimiza wenzao kujitokeza kwa wingi. 

Hatua hiyo iliufanya uongozi wa mkoa kuwasambaza polisi mitaani kuzuia mkutano huo. Mabomu ya machozi na maji ya kuwasha vilitembezwa kwa wafanyabiashara hao ambao walikuwa wamekusanyika huku maduka yao yakiwa yamefungwa.

Mabomu hayo ya polisi yaliwaathiri wanafunzi wa Shule ya Msingi Kagera na kuwafanya wataharuki na kuanza kukimbia hovyo huku wengine wakizirai.

Kufuatia hali hiyo, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Ayoub Kiwanga, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Ilomba, Erasto Mwakaponda na Diwani wa kata hiyo, Dickson Mwakilasa, walikubaliana kuwakabidhi wanafunzi hao kwa wazazi wao waliofika shuleni hapo kuwajulia hali baada ya kupokea taarifa za kupigwa mabomu.

Wakizungumza na Tanzania Daima, wafanyabiashara hao walisema kuwa wanashindwa kuelewa nguvu kubwa ambayo inatumiwa na polisi wakati hakuna vurugu zozote katika eneo hilo.

Alex Oswald, kwa niaba ya wenzake alisema kuwa wao waliamua kufunga maduka kwa hiari yao na kwamba lengo la mkutano lilikuwa kutoa msimamo wa kuiomba serikali itoe mashine hizo bure.

Naye Peter Tweve, alisema kuwa kimsingi wao hawajagoma kutumia mashine hizo bali wanataka wawekewe bure, kwani si kila mfanyabiashara anaweza kuinunua mashine hiyo ambayo kwa sasa inauzwa kwa sh 800,000.

Alipotafutwa Kandoro kuelezea tukio hilo, aligoma akisema kuwa yupo katika kikao, pia Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Diwani Athumani, simu yake iliita bila kupokewa.

Wiki moja iliyopita, Mkurugenzi wa Elimu ya Kodi wa TRA, Richard Kayombo, alitoa taarifa kuwa wafanyabiashara wenye mapato ya zaidi ya sh 45,000 kwa siku wanapewa hadi Oktoba 14, mwaka huu wawe wamenunua mashine hizo.

Friday, September 20, 2013

WAZIRI AMTISHA JK

Na, Betty Kangonga

WAZIRI wa Sheria na Katiba, Mathias Chikawe amemtisha Rais Jakaya Kikwete akisema kuwa endapo hatasaini muswada wa sheria ya marekebisho ya sheria ya mabadiliko ya katiba wa mwaka 2013, atakuwa ameingia kwenye mgogoro na Bunge.

Muswada huo uliopitishwa hivi karibuni na wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja na Augustine Mrema wa TLP (Vunjo), unapingwa vikali na vyama vya upinzani pamoja na makundi mbalimbali ambayo sasa yanamshinikiza rais asiusaini kuwa sheria.

Makundi hayo ambayo yamepata msukumo wa vyama vitatu vya CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi ambavyo wabunge wake walikataa kuujadili muswada huo wakipinga uchakachuaji uliofanyika wa kuongeza vifungu na kutoishirikisha Zanzibar, tayari yametishia kwenda kortini ikiwa watapuuzwa.

Akizungumza jana na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Chikawe alisema kuwa ni vyema makundi mbalimbali yakaacha kumlaghai Rais Kikwete ili asiusaini muswada huo.

Kwa mujibu wa Chikawe, iwapo Rais Kikwete ataliafiki suala hilo la wapinzani na makundi mengine, na kuacha kutia saini muswada huo, atakuwa ametengeneza mgogoro na mhimili wa Bunge kutokana na chombo hicho kukamilisha kazi yake.

Alisema kuwa taratibu zote zilifuatwa kuhusiana na kupitishwa kwa muswada huo, na kudai kushangazwa na baadhi ya makundi yanayopiga kelele.

“Hao wanaolalamikia juu ya jambo hilo hawatendi haki kwani sheria zote zilifuatwa na hayo mapendekezo wanayotoa ya kutaka Rais Kikwete asitie saini sio sahihi hata kidogo, huko ni kutaka ‘kumblack mail’ na kumsababishia mgogoro na Bunge,” alisema.

Waziri Chikawe alisema kuwa ameshangazwa na baadhi ya matamshi yanayotolewa juu ya kuwepo kwa fujo au kumwagika damu na kusema jambo hilo haliwezi kufanikiwa kama halijapangwa.

“Fujo zinapangwa, hivyo wale wanaotaka kumwaga damu ni vyema wakajitaja na kusema kuwa ‘sisi tutamwaga damu’ kwa kuwa naamini damu haiwezi kumwagika yenyewe,” alisema.

Waziri huyo alisema kuwa ni vyema wale wanaotaka kuzunguka kwa wananchi na kufanya udanganyifu juu ya suala hilo, wangekubali kuwasilisha hoja hizo ndani ya Bunge na si mahali kwingine.
Kuhusu Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria kutopeleka muswada huo kwa wananchi wa Zanzibar, 

Chikawe alisema kuwa utaratibu uliotumika ni hisani tu, kwani hakuna sheria inayotaka muswada wa aina yoyote kupelekwa kwa Watanzania.

“Utaratibu wa kupitisha muswada huo sio huo tu, bali zipo njia nyingi ambapo anaweza kuandika anayohitaji na kuwasilisha kwa kamati ya Bunge na wapo waliofanya hivyo,” alisema.
Chikawe aliongeza kuwa inawezekana Kamati ya Katiba na Sheria ikawa na  sababu za kushindwa kuwafikia wananchi wote, lakini kwa upande wao walipokea maoni ya Serikali ya Zanzibar yaliyotolewa Mei 27, mwaka huu.

Alisema kuwa moja ya pendekezo lililotolewa na Serikali ya Zanzibar ni juu ya kuongezwa kwa siku 20 kati ya 70 zinazotakiwa kutumiwa na Bunge Maalumu la Katiba.
Chikawe alisema kuwa ni vyema yale yanayoenda kutolewa kwenye mkutano wa wapinzani kesho katika viwanja vya Jangwani, yangepelekwa bungeni kwa kuwa hata wakitoa katika viwanja hivyo haitasaidia.


ju





Thursday, September 19, 2013

WAANDISHI WAKWIDWA , WANYANYASWA NA KUPOKEA KIPIGO




Na Dixon Busagaga, Moshi

WAKATI watuhumiwa wanne zaidi wakiongezwa katika kesi ya mauaji ya mfanyabiashara wa madini ya tanzanite mkoani Arusha, Erasto Msuya, waandishi wanaoiripoti jana walionja joto ya jiwe kwa kukwidwa na kutaka kunyang’anywa vitendea kazi vyao.

Tafrani hiyo ilitokea katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mjini Moshi saa 5:30 wakati kesi hiyo inayowakabili washtakiwa saba wanaodaiwa kushiriki kupanga na kutekeleza mauaji ya Msuya ilipofikishwa mbele ya mahakama kwa ajili ya kutajwa.

Akizungumzia tukio hilo, mmoja wa waandishi hao, Fadhili Athuman alisema kuwa walipata wakati mgumu walipojaribu kuchukua picha za ndugu wa Msuya.

Athuman alisema kuwa baada ya kupiga picha kadhaa, alikwidwa na wanafamilia hao, wakitaka kumpora kamera huku mwandishi mwenzake akishikwa na kupigwa kibao.

“Baada ya kesi kuahirishwa iliibuka tafrani, walitaka kuninyang’anya kamera ili wafute picha nilizokuwa nimepiga. Mwenzangu yeye alikamatwa na kupigwa vibao kabla askari wa kikosi cha FFU kumuokoa,” alisema.

Kwa mujibu wa mmoja wa watu wa karibu na familia ya Msuya ambaye aliomba kuhifadhiwa jina, wamechukizwa na hatua ya baadhi ya waandishi kutochapisha picha za watuhumiwa, na badala yake zinatolewa za wanafamilia hiyo.

Hali ya taharuki ilianza mapema baada ya chumba kilichozoeleka kuendeshea kesi hiyo kubadilishwa kwenda kwenye chemba kutokana umati wa watu uliohudhuria kuwa mkubwa.

Wakati huo huo, vilio viliendelea kutawala mahakamani hapo baada ya kesi hiyo kuahirishwa. Mama mzazi wa Msuya, Marry Msuya alipoteza fahamu na kukimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC.

Awali mbele ya Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Ruthi Mkisi, mawakili wa serikali, Stella Majaliwa akisaidiwa na Janeth Sipule waliieleza mahakama kuwa washitakiwa wanne wameunganishwa katika kesi hiyo na kufikia saba.

Majaliwa aliwataja waliounganishwa kuwa ni mshitakiwa wa nne hadi saba ambao ni Jalila Zuberi, Karimu Kihundrwa, Sadiki Jabiri (Chusa) na Joseph Mwakipasile ambao wote walifika mahakamani hapo.

Hakimu Mkisi alisema kesi hiyo imeahirishwa kutokana na upelelezi kutokamilika na hivyo kutaka washitakiwa hao kurudi rumande hadi Oktoba 2, mwaka huu.

Agosti 21, mwaka huu, washitakiwa watatu; Sharifu Mohammed, mkazi wa Kimandolu Arusha, Shaibu Mpungi, mkazi wa Kijiji cha Songambele wilayani Mererani na Musa Mangu mkazi wa Shangarai kwa Mrefu Arusha, walifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza.

Washitakiwa wote saba waliondolewa mahakamani hapo chini ya ulinzi mkali wa askari wenye silaha za moto wakiwa ndani ya gari lenye namba za usajili T 743 ADC lenye vioo vyeusi.

Msuya aliuawa Agosti 7 mwaka huu saa 6:30 mchana kwa kupigwa risasi 13 kifuani, kando ya barabara kuu ya Arusha – Moshi katika eneo la Mjohoroni wilayani Hai.

Friday, September 13, 2013





 Mkurugenzi  Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania ( TGNP) U ssu Mallya

Na,Alpius Mchucha—Namtumbo

BAADHI ya wanawake wa wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma,wamesema wangetamani  siku moja kuona katika katiba ijayo kunakuwa na kipengele maalum cha kuwabana wanaume wanaowakashifu wanawake kwa kutaja sehemu za siri za wanawake hao kwani tabia hiyo imekuwa ikiwadhalilisha sana kwa jamii na kuwavunjia heshima na utu wao.

Wakizungumza katika mdahalo wa siku moja jana uliowakutanisha wanawake zaidi ya 50 kutoka katika vijiji mbalimbali  vya wilaya hiyo wanawake hao walisema,wameshachoshwa na matusi yanayotolewa na wanaume ambayo yanataja sehemu za mwili wa mwamke hivyo ni lazima  kutafuta njia ya kukomesha kwakuwa matusi hayo yamewafanya kuonekana kama siyo watu wanaotoa mchango kwa jamii na  nchi.

Mdahalo huo wenye lengo la kujadili,kubadilishana uzoefu, kujifunza masuala ya  kijinsia na elimu ya uraia uliandaliwa kwa pamoja na shirika lisilokuwa la kiserikali la Oxfam na mradi wa kuwawezesha vijana wa Restless Devolopment ulifanyika katika ukumbi wa Parokia mjini Namtumbo.

Mmoja wa wanawake hao Christina Kuhimini alisema, sasa wameshachoshwa na  udhalilishaji dhidi yao  hivyo kuiomba serikali kutokuwa na huruma na watu hao  wasiokuwa na hata  chembe ya aibu ambao kila kukicha wanatafuta maneno mapya ya  kuwakashifu wanawake licha ya kutambua kuwa bila ya  mwanamke  basi hata wanaume hao wasingeweza kutokea hapa Duniani kwa kile alichoeleza kuwa hakuna binadamu anayeweza kuzaliwa na mwaume bila ya kuwa na mwanamke.

“bahati mbaya sana muda wa kutoa maoni kwa ajili ya katiba mpya umekwisha,lakini kupitia vyombo vya habari vilivyopo hapa leo naomba  sana watufikishie ujumbe wetu sisi wanawake wa Namtumbo tumechoshwa sana na matusi yanayotolewa na wanaume kila siku,tena ni mibaba mizima nayo utoa lugha za kuwakashifu wanawake ambao hawana hatia yeyote,ili siyo jambo jema hata kidogo ni baya linalowadhalilisha wanawake”alisema.

Aliongeza kuwa,  tabia hiyo  ya matusi licha ya kutaja maumbile ya ndani ya mwanamke lakini kwa bahati mbaya sana imekuwa ikiwarithisha watoto wadogo wanaohitajki kusikia au kufundishwa matendo  mazuri kutoka kwa watu wazima,lakini cha kushangaza hakuna hatua inayochukuliwa hivyo kuendelea kuota mizizi na kuonekana kama jambo la kawaida.

Kwa upande wake mwenyekiti wa mtandao wa polisi wanawake  na mratibu wa dawati la jinsia mkoani hapa Mrakibu wa jeshi la  polisi Anna Tembo alisema tatizo kubwa lililopo ni  wazazi kushindwa kuwafundisha maadili mema watoto wao tangu wakiwa wadogo hivyo kujikuta wakiiga tabia mbaya za mitaani ambazo hazina misingi bora kwao.

Pia amewataka wanawake kubadilika na kuanza kujitambua kwa kutojihusisha katika matukio yanayowafedhehesha ambayo yanawafanya kuonekana vituko kwa jamii ya kistaarabu na ambayo kwa kiasi Fulani yanawapa kiburi wanaume kufanya watakalo kwa wanawake.

Tembo alieleza kuwa,wanawake wengi wanafanya matukio   ambayo ndiyo yanayowapa hamasa wanaume kufikiria kuwa mwanamke ni chombo cha kutumika vibaya badala ya pambo ndani ya nyumba na kuendelea kuwafanyia unyama wa kila aina akina mama.

Alitaja uvaaji wa nguo fupi,  zinazobana na zinazoonesha maumbile yao,kucheza shoo nyakati za usiku katika sehemu za starehe,kujiuza, na hata ukatili kwa watoto navyo ni sababu kubwa ya kudhalilika kwao.
                 MWISHO