SIKU moja baada ya gazeti la Mtanzania kuandika habari likidai kuwa siri ya
kumuua Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA) imefichuka, kiongozi
huyo amejitokeza akisema ni uzushi.
Habari hiyo ilidai kuwa ilipangwa Zitto anyweshwe sumu hotelini na kumtaja
Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa kuwa ndiye alimtuma kijana Ben
Saanane kutimiza mkakati huo.
Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wa kisiasa walisema habari hiyo inayodai
tukio hilo lilitokea Mei mwaka jana jijini Dar es Salaam, ilikuwa ni propaganda
ya kuhamisha mjadala wa sakata la kuteswa na kuumizwa kwa
Mwenyekiti wa Jukwaa
la Wahariri nchini (TEF), Absalom Kibanda.
Kibanda alitendewa unyama huo Machi 6 mwaka huu, lakini hadi leo vyombo vya
dola vimeshindwa kuwakamata wahusika na badala yake yamekuwa yakiibuliwa matukio
mbalimbali ili kupoteza ajenda hiyo inayoonesha udhaifu wa kiutendaji wa vyombo
hivyo.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Zitto alisema habari hiyo
imemletea usumbufu mkubwa kwani ndugu, jamaa, marafiki na wapiga kura wake
wamejawa na wasiwasi kwamba anaweza kuuawa.
“Moja, sijawahi katika maisha yangu yote kukutana na mtu anayeitwa Ben
Saanane na hivyo hicho kikao ambacho inasemekana nilikuwa naye na akajaribu
kunipa sumu hakijawahi kutokea. Imetajwa Hoteli ya Lunch Time ambayo sio tu
sijawahi kufika, pia hata siijui ipo wapi,” alisema.
Alifafanua kuwa haijawahi kutokea yeye kufanya kikao cha pamoja na Ben
Saanane, Juliana Shonza na Mtela Mwampamba. Hivyo habari iliyoandikwa ni ya
kufikirika.
“Pili, siamini kamwe kuwa Katibu Mkuu wa chama changu (Dk. Slaa) anaweza
kupanga kuniua maana hana sababu ya kufanya hivyo. Napenda kurudia kusema kwamba
mimi ninaamini kuwa kila nafsi itaonja mauti.
“Kila mtu atakufa. Kama nitakufa kwa kuuawa na mtu mwingine ndiyo itakuwa
nimeandikiwa hivyo na Mungu. Ndiyo maana hata siku moja silalamiki kuhusu
vitisho vya kuuawa. Kama kuna mtu anafikiria kuwa kumuua Zitto ndiyo furaha ya
maisha yake atakuwa anajidanganya tu maana Zitto anaweza kufa kimwili, lakini
mawazo, fikra na maono yake yataishi tu,” alisema.
Aliongeza kuwa haogopi kufa maana maisha aliyoyachagua ndiyo haya ambayo
yamejaa vitisho, kwamba muhimu kwake ni kufanya kazi zake kwa bidii, uhodari na
uaminifu.
“Tatu, nawashauri watu ambao wamehama CHADEMA na kuhamia vyama vingine
watumie muda wao kujenga vyama vyao badala ya kila siku kuzungumzia masuala ya
chama ambacho wao sio wanachama tena.
“Kama mtu kaamua kuhama CHADEMA anapoteza haki ya kujadili masuala ya
CHADEMA, maana kama angekuwa anapenda kuyajadili asingehama. Naonya mtu yeyote
ambaye anatumia jina langu ili kufanikisha malengo yake ya kisiasa,” alionya
Zitto.
Zitto ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA (Bara), alisema chama hicho
si pango la watesaji wala wauaji, kwamba kuna mwanachama wa chama kingine cha
siasa anayedhani kuna mtu ndani ya CHADEMA anapanga mipango ovu aende kwenye
vyombo vya sheria kumshtaki.
“Matendo ya mtu mmoja yasifanyiwe propaganda kama ni malengo ya taasisi. Nne,
Nawashauri viongozi wa CHADEMA na hasa wanachama tutumie muda wetu kujenga
mshikamano ndani ya chama. Fitna, majungu, uongo, uzandiki nk kamwe havijengi
chama,” alisema.
Saanane ang’aka
Naye Saanane aliyedaiwa na gezeti hilo kuwa ndiye alikuwa ametumwa kumdhuru
Zitto, alisema amesikitishwa jinsi lilivyoshiriki katika dhamira nzima ya
kumchafua.
Akizungumza katika ofisi za Tanzania Daima jana, Saanane ambaye ni mjumbe wa
Baraza la Vijana wa CHADEMA (BAVICHA) alisema kutokana na habari hiyo ameamua
kukutana na wanasheria wake kuangalia hatua za kuchukua ili ukweli ubainike.
“Nasisitiza sijawahi kupanga kumuua mtu yeyote, sijawahi kutumwa kumuua Zitto
Kabwe. Nimesikitishwa kuona chombo cha habari kikitumika kwa maslahi binafsi ya
kuchafua watu kisiasa,” alisema.
Aliongeza kuwa mara zote alizokutana na Zitto, hawajawahi kufika katika
Hoteli ya Lunch Time wakiwa pamoja kama ilivyoelezwa katika gazeti hilo.
Bashe anena
Alipoulizwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya New Habari (2006) Ltd
wachapishaji wa gazeti hilo, Hussein Bashe juu ya tetesi za kutumiwa kuyeyusha
sakata la kuteswa kwa Kibanda kwenye vyombo vya habari, alisema hawawezi
kutumiwa na taasisi yoyote kuzima suala hilo.
“Hilo la namna habari ilivyotoka mimi si mwandishi wa habari, ninachoweza
kukuambia ni kwamba magazeti ya New Habari hayawezi kutumiwa na mtu yeyote
kuzima au kufifisha suala la Kibanda,” alisisitiza.
Alisema kama kuna watu wanafanya siasa rahisi za kuyahusisha magazeti yao na
mkakati wa kuzima suala la Kibanda watakuwa wamekosea kwa kile alichoeleza
hawezi kuruhusu hali hiyo.
Alipoulizwa atachukua hatua gani kwa mhariri endapo itabainika gazeti hilo
kutumika kwa lengo la kuwatoa watu katika kujadili madhila yaliyompata Kibanda,
alisema hayo ni masuala ya ndani ambayo hayawezi kuwekwa hadharani pasipo
kufuata taratibu.
|
No comments:
Post a Comment