Watanzania wenzangu,
Tumeshashughudia utekwaji wa watu kadhaa mara kwa mara. Tumeshashuhudia matukio mbalimbali ya ajabu, ambayo hata hivyo yalifanywa kwa namna ya kuwasingizia majambazi.
Leo, tunamwona tena Mwanahabari mahiri, Absalom Kibanda, akipelekwa Afrika Kusini kwa matibabu, si ya ugonjwa, bali ya kipigo kutoka kwa watu wasiofahamika, watu waitwao majambazi.
Hili linatokea muda wa miezi takribani minne baada ya Mnaku Mbani, Mhariri wa gazeti la Business Times kupigwa risasi mdomoni na kupoteza meno matatu.
Hili linakuja baada ya Mwandishi mwingine wa Tanzania Daima, Shaaban Mtutu kupigwa risasi na Polisi eti akidhaniwa ni jambazi. Huyu alipigwa risasi akiwa nyumbani kwake mnamo tarehe 4 Disemba, 2012, eti polisi walimdhania ni jambazi, AKIWA NYUMBANI KWAKE.
Tukio la Kibanda, linatokea ikiwa ni miezi michache tangu Mwangosi Daudi, mwandishi wa Channel Ten kuuawa na jeshi la polisi tarehe 2 Septemba 2012.
Hili linakuja miaka michache baada ya mapema mwaka 2008 Saed Kubenea, Mkurugenzi wa kampuni ichapayo gazeti la Mwanahalisi (ambalo nalo limefungiwa), kumwagiwa tindikali machoni pamoja na Mhariri Mshauri wa gazeti hilo Ndimara Tegambwage kucharangwa kwa mapanga.
Linatokea miezi michache baada ya Dk. Ulimboka kutekwa na kupigwa nusu kifo, na kutupiwa msitu wa Mabwepande. Haya yote yanatokea Tanzania, na asilimia kubwa ya haya yote yamehusishwa na ujambazi.
Huwa najiuliza, ujambazi ni nini? Kwa nini hao majambazi hawaibi chochote zaidi ya kuwajeruhi na kunuia kuwaua hawa makamanda? Kwa nini wawavamie tu watu wenye kuikosoa serikali?
Hao majambazi kwa nini hawapatikani? Ikiwa juzi tu ameuawa kwa risasi Padre kule Zanzibar, na serikali imewaleta FBI kwa ajili ya uchunguzi wa tukio hilo, kwa nini serikali isione haja ya kuwatumia FBI na taasisi nyingine za ukachero kutoka mataifa yaliyoendelea ili tuwapate hawa wahalifu wawavamiao wanahabari na wanaharakati wetu? Watanzania, tutanyamaza hadi lini ikiwa sauti zetu zinanyamazishwa?
Bwana Kibanda, hadi sasa, ana kesi mahakamani. Kesi ya uchochezi baada ya gazeti la Tanzania Daima (Wakati Kibanda akiwa Mhariri) kuchapa makala iliyoandikwa na Mwandishi na Mwanaharakati Samson Mwigamba. Kesi hii ingali ikisikilizwa, leo tunasikia kuwa amevamiwa na majambazi! Kweli? Latuingia akilini kweli? Latushawishi hili kweli?
Tanzania, serikali imetengeneza mtandao wa Kimafia (kama alivyoeleza Mh. Joseph Mbilinyi Bungeni Mwaka jana). Kumekuwa na mtandao wa kimafia unaowawinda makamanda, wanaharakati.
Habari/tetesi zilishawekwa wazi kuwa kuna kundi la watu limeundwa, linalojishughulisha na utekaji, utesaji, na uuaji wa watu wenye ushawishi katika jamii, wanaoikosoa serikali kwa uwazi. Yamkini kundi hili ndilo lililoripotiwa kuwafuatilia Mh. John Myinka, Mh. Godbless Lema, na Mh. Dk. Wilbroad Slaa.
Yamkini hilo ndilo kundi lililomwekea sumu Mwanaharakati mwingine Dk. Harryson Mwakyembe. Hili ndilo kundi lililoripotiwa kufuatilia maisha ya Mh. Samwel Sitta. Hili ndilo kundi, ndilo hasa!
Kundi hili la kimafia limeamua kuwanyamazisha Watanzania, na kuiacha serikali iendelee kutuibia, kutunyonya na kutufanya mafukara.
Kundi hili limenuia kuifanya serikali iendelee kutawala na kujinawirisha. Vigogo wa serikali na watoto wao waendelee kufurahia nchi, kwa kodi zetu wananchi.
Kundi hili limenuia kuhakikisha viongozi waovu na wabadhirifu wa mali za umma wanaendelea kututawala kwa mabavu, kwa matisho na kwa dhuluma.
Kwa mtindo huu, lazima tuhoji waziwazi kuwa kwa nini watu hawa hawakamatwi na kutiwa nguvuni, iwapo kweli serikali haina uhusiano nao?
Si ndio hawa wafanyao kazi kama Ramadhani Ighondu? Hapa tusidanganyane, serikali inawafahamu watu wote wa kundi hili... Serikali inafahamu A hadi Z ya kundi hili, na yamkini serikali ndiyo iliyowapa kazi hii maalum.
Kufunika kombe ili mwanaharamu apite, tunaiona serikali ikienda kuwajulia hali wahanga wa uonevu huu. Serikali inamtuma Makamu wa Rais kwenda kumtazama Kibanda hospitalini, Rais Kikwete pia alikwenda kumjulia hali Saed Kubenea... Yote haya ni kujaribu kutudanganya (elude) kuwa hawajui kiendeleacho..
Serikali inafahamu kundi lake hili la kimafia. Kundi la uovu, inalifahamu vyema..
Sasa, kwa nini serikali ifanye hivi? Kwa nini wanaharakati wateswe, wakamatwe, wauawe? Ukweli wenyewe ndio huu:
Lengo kuu la serikali, ni kunyamazisha sauti zote zinazoikosoa bila kujali sauti hizo zinatokea wapi. Serikali inahitaji kunyamazisha sauti za watu binafsi, inahitaji kunyamazisha sauti za vikundi, vyama au jumuiya zinazoikosoa.
Sasa kwa sababu tasnia ya habari huwafikia wengi, na kwa sababu watu wengi huamini habari za vyombo vya habari, serikali imenuia kuinyamazisha kabisa tasnia ya habari kwa kushughulika na wakosoaji wakubwa katika vyombo vya habari.
Ndio maana hata waandishi wa makala kama hizi wanatafutiwa visa hata vya kufungwa gerezani. Mfano mzuri wa hili ni kesi ambayo inaendelea mahakamani dhidi ya Kibanda mwenyewe, na Samson Mwigamba, eti kwa sababu ya makala iliyochapwa kwenye gazeti la Tanzania Daima.
Pengine wengi wetu mnamkumbuka Sam Shollei. Huyu alikuwa ni Mkurugenzi Mtendaji wa gazeti la Mwananchi, kabla ya Tido Mhando wa sasa.
Huyu si Mtanzania bali ni Mkenya. Shollei aliibadilisha taswira ya gaeti la Mwananchi na kulifikisha katika taswira lililokuwa nayo sasa.
Alifanya kazi kubwa sana. Lakini, mwisho wake alinyimwa kibali cha kuendelea kufanya kazi nchini Tanzania baada ya kibali chake cha awali kwisha muda.
Serikali, kupitia uhamiaji, ilimnyima Shollei kibali bila kuweka bayana sababu za kufanya hivyo. Zitto Kabwe alipiga kelele kidogo kuikosoa serikali kwa swala hilo lakini kelele zake hazikufua dafu.
Shollei, aliyelipa gazeti la Mwananchi umaarufu mkubwa na maendeleo makubwa akalazimika kuacha kazi.
Baada ya Shollei kulazimika kuondoka Tanzania, nafasi yake ikachukuliwa na Tido Mhando. Hapa tukumbuke kuwa, Tido Mhando alifuatwa na Rais Kikwete London mwaka 2007, akiwa Mkurugenzi wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC, na Kikwete akamwomba aje aiongoze TBC.
Hata hivyo naye alipoiongoza TBC na kuwa chombo cha uwazi na ukweli, na pale aliporuhusu kuonyeshwa kwa mikutano ya kampezi ya vyama vyote vya siasa katika uchaguzi Mkuu wa 2010, bila upendeleo, Tido alinyimwa mkataba mpya mwaka 2011.
Tido, akiwa amebadilisha taswira ya Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC), akanyimwa mkataba wa kuendelea kuiongoza. Sasa ni nani asiyejua kuwa TBC imeshapoteza ule umahiri wake ambao Tido aliisaidia kuwa nao? TBC sasa imerejea ilipotoka, imeanza kulichungulia kaburi tena...
Baada ya Tido kunyimwa mkataba na serikali, licha ya kwamba watu wengi walilaumu sana, Tido akachukuliwa na Mwananchi, kuziba nafasi ya Shollei.
Sasa, pengine kwa weledi wa Absalom Kibanda, kwa kazi ambayo ameifanya tangu akiwa Mhariri Mtendaji wa Tanzania Daima, naye ameanza kutafutwa roho yake na hao wanaoitwa "majambazi". Majambazi wasioiba chochote, majambazi watafutao roho za wanahabari mahiri na wanaharakati.
Nirudie tena, lengo la serikali ni kuifunga mdomo tasnia ya habari Tanzania. Lengo lake ni kuwa na vyombo vya habari kama Radio Uhuru na Gazeti la Mzalendo ambayo kazi yao ni kuitukuza serikali ya CCM hata pale pasipostahili.
Lengo la serikali, ni kuwanyamazisha makamanda wote waonekanao kuikosoa serikali kwa uwazi. Na hili linaonekana kufanikiwa kwa kiasi fulani.. Kwani gazeti la Mwanahalisi liko wapi leo? Mwangosi yuko wapi? Kubenea anasikika tena? Je ulimboka mmemsikia tena? Wote hawa wameshanyamazishwa kwa kiasi fualani, sauti zao zimefifia.
Watanzania wenzangu, Tanzania ya sasa si mahala salama kwa Wanahabari makini, na wanaharakati. Nawaomba na kuwasihi tuwe macho na tuamke tuungane na wenzetu hawa waliojitoa mhanga.
Tusimameni imara kuitetea nchi yetu, haijalishi watuue sote. Kwa hakika, tusiposimama imara, nchi hii tutaitumbukiza korongoni.
Tupazeni sauti zetu pale tuwapo na nafasi. Kwa wale tusioweza kuchapa makala kwenye magazeti mbalimbali, mitandao ya kijamii ndio silaha yetu iliyosalia.
Tusiandike jumbe za mapenzi kwenye kuta zetu za Facebook, Tiwitter, blogu zetu. Tuandikeni jumbe za kutafuta haki na usawa nchini.
Tuandikeni jumbe za kuikosoa serikali na kuilalamikia kila uchwao uchao. Tusiishie hapo; tuwaamsheni Watanzia wenzetu; tuwaamsheni waliolala... Tuwaelezeni kumepambazuka.... Tusipofanya hivyo, tutakapoacha kazi hii mikononi mwa wenzetu wachache, kwa hakika tutashiriki kiliangamiza taifa letu. Mwisho tutalia na kusaga meno.
No comments:
Post a Comment