About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Monday, April 29, 2013

LEMA AENDELEA KULA BATA BAADA YA KUPEWA DHAMANA

            Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema



MVUA nyepesi iliyonyesha kuanzia alfajiri, jana haikuwazui mamia ya wafausi wa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, kujitokeza kwa wingi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, wakati mbunge huyo alipofikishwa kusomewa shtaka la uchochezi.


Lema ambaye alikamatwa Ijumaa usiku kwa amri ya Mkuu wa Mkoa, Magesa Mulongo, na kuwekwa rumande kwa siku tatu, alifikishwa mahakamani saa tatu asubuhi akiwa katika gari dogo lenye vioo vyeusi likiwa na namba za usajili T 818 AJD.

Mbunge huyo alisindikizwa na askari wawili waliovaa suti wakiwa na silaha pamoja na Mkuu wa Upelelezi Mkoa (RCO).

Ilipofika saa nne, mbele ya Hakimu Devota Msofe, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Elianenyi Njiro, alidai kuwa kesi hiyo ni mpya na inatajwa mara ya kwanza, angeomba asome mashtaka na ipangiwe tarehe nyingine.

Akisoma mashtaka hayo, alidai kuwa Aprili 24, mwaka huu, katika eneo la Freedom Square Chuo cha Uhasibu, Lema alichochea utendaji makosa na kukiuka kifungu 390 na 35 cha kanuni za dhabu sura ya 16 kama ilivyorekebishwa mwaka 2000.

Alitaja shtaka la Lema ni kutamka maneno: “Mkuu wa mkoa anakwenda kwenye ‘send off’, hajui chuo cha uhasibu mahali kilipo wala mauaji ya mwanafunzi wa chuo hiki. Ameshindwa kuwapa pole kwa kufiwa na kusikiliza shida zenu na anasema hawezi kuongea na wanafunzi wasio na nidhamu.” Alisisitiza kuwa maneno haya ndiyo yaliyosababisha kuvurugika kwa amani.

Baada ya kusoma shtaka hilo, aliongeza kuwa kwa upande wao hawana kipingamizi cha dhamana na hivyo hakimu Msofe alimuuliza wakili wa mshtakiwa, Method Kimomogolo, kama ana la kusema.

Kimomogolo alimueleza hakimu kuwa kwa vile maelezo ya shtaka hayaonyeshi kuelekea kwenye kutenda kosa, anaomba mshtakiwa aruhusiwe kujidhamini mwenyewe kwa kuwa ni mbunge wa Arusha, hivyo hawezitoroka.

Hakimu Devota alitaja masharti ya dhamana kuwa ni mdhamini mmoja mwenye kitambulisho na atakaesaini dhamana ya sh milioni moja ambapo Diwani wa Viti Maalumu (CHADEMA), Sabina Francis, aliitwa na Kimomogolo akamdhamini Lema baada ya kukidhi masharti hayo.

Mara baada ya kukamilika kwa taratibu hizo, hakimu Msofe aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 29 itakapofika kwa ajili ya kutajwa tena.

Hali mahakamani

Lango la kuingilia katika chumba cha mahakama hiyo lilikuwa na askari sita ambapo watatu walivalia mavazi rasmi wakiwa na silaha na wengine wakiwa wanaangalia kila mtu anaekaribia hapo.

Askari wengine waliovalia kiraia walikuwa ndani ya chumba cha mahakama wakiratibu kila mtu aliyekuwemo ndani ambapo wengi waliokuwamo ni madiwani wa CHADEMA na waandishi wa habari.

Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nasari, alikaa na Lema wakibadilishana mawazo juu ya kilichotokea.


Nje ya mahakama ambako wananchi wengi walikuwa wamekusanyika, nako kulikuwa na askari wengi waliokuwa wamevalia kiraia.

Mbali na askari kanzu kujaa mahakamani hapo pia askari waliovalia sare wakiwa na gari tano huku wakisheheni silaha nzito pamoja na mabomu ya machozi walifanya doria mahakamani na maeneo ya barabara zote za kuelekea na kutoka eneo hilo.

Kulikuwa na magari yenye namba za usajili PT 2077, PT 1076, PT 2017 na PT 1844, zote zikiwa na askari wenye silaha kati ya saba na tisa wakizunguka maeneo yote jirani na Mahakama Kuu mjini Arusha wakati katika Kituo Kikuu cha Polisi kuliimarishwa ulinzi ambapo hakuna gari lililokuwa likiruhusiwa kuingia.

 

Lema ahutubia

Baada ya kesi kuahirishwa, wafuasi wa Lema waliandamana naye kutoka katika viwanja vya mahakama na kupitia ofisi ya mkuu wa mkoa wakishangilia hadi ofisi za CHADEMA mkoa.

Kutokana na wingi wa wafuasi hao ililazimu Lema kuzungumza nao katika kiwanja cha Shule ya Msingi Ngarenaro.

Aliwashukuru kwa kujitokeza kumuunga mkono na kuwasihi kuwa kamwe wasiwe waoga katika kutetea haki zao mpaka wahakikishe nchi inakombolewa.

Pia Lema alivishukuru vyombo vya habari kwa kuripoti ukweli halisi wa tukio na kusaidia kuepuka kubambikiwa mashtaka.

Alisema licha ya kuwekwa rumande lakini imemsaidia kujua masahibu mengi wanayoyapata mahabusu wanapokuwa sero, kwamba kuna mahabusu wana siku 26 hadi 40 hawajafikishwa mahakamani.

Alisema ameshangazwa kukuta chumba cha kukaa watu 20 wanalazwa watu 90 kitendo ambacho alidai kinahatarisha usalama wa mahabusu.

Lema alisema kuwa hatokwenda bungeni wiki yote ili apate muda wa kufanya mikutano ya hadhara huku akiwasisitizia wananchi wa Arusha mjini kumzomea mkuu wa mkoa popote atakapokwenda.

“Nasisitiza ilikuwa ni haki yake kuzomewa na wanafunzi wa Chuo cha Uhasibu kutokana na dharau alizozionyesha alipofika chuoni hapo na nawaambia wakazi wa Arusha kuendelea kumzomea popote atakapokwenda jimboni kwangu,’’ alisema.

Nao baadhi ya wananchi waliozungumza na gazeti hili baada ya Lema kuachiwa walimlalamikia mkuu wa mkoa wakisema ametumia madaraka vibaya pamoja na kumpotezea muda Lema wakati shtaka lenyewe halina mashiko.

Walisema kuwa ifike wakati uwekwe utaratibu wa kuwadhibiti viongozi kama hao wanaochezea kodi za wananchi kwa mambo yasiyo na msingi.

Naye Nasari alimuonya Mulongo kuacha tabia ya kuwadharau wabunge wa CHADEMA na kusema hali hiyo itamfanya ashindwe kuongoza mkoa huu.

Katibu wa CHADEMA Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa, mbali na suala hilo la Lema alitoa tamko la chama kuitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi kupitia kwa Mkurugenzi wa Jiji kuiunganisha kata ya Sombetini katika uchaguzi mdogo utakaofanyika Juni 16.

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), Hussein Bashe, amesema kuwa Mulongo alionyesha dharau ya wazi mbele ya wanafunzi wa Chuo cha Uhasibu jijini Arusha na kwamba hali hiyo inapaswa kulaaniwa na kila mmoja.

Bashe alisema kwa dharau hiyo ni dhahiri ameivunjia heshima serikali na kuwafanya wananchi kuongeza chuki zaidi dhidi ya CCCM.

Mjumbe huyo alitoa maoni hayo kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Facebook wakati akijadili suala zima la kukamatwa kwa Lema pamoja na uamuzi wa baraza la madiwani wilayani Nzega mkoani Tabora kujitengea zaidi ya sh milioni 80 kwa ajili ya safari ya mafunzo jijini Arusha na Dodoma.

Alisema watu badala ya kutumia nguvu kubwa kuwatafuta wahalifu waliosababisha kifo cha mwanafunzi wa chuo hicho, wameamua kutengeneza mazingira ya kumkamata Lema.

“Kaka yangu Mulongo katika hili alivyolisimamia na kulitekeleza ameonyesha udhaifu wa hali ya juu na matokeo yake ni kuivunjia heshima serikali ya chama chetu na kuongeza chuki,” alisema.

No comments:

Post a Comment