About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Tuesday, April 23, 2013

TAFAKARI MAANDIKO HAYA KWA AFYA YA AKILI YAKO

Umaarufu au Udhaifu Haulazimishwi, Bali Unajithibitisha Wenyewe!


Ukweli siku zote ni lazima ubakie ukweli, watu wengi mara kwa mara wamejitahidi kurudia uongo na hata wakati mwingine uongo huo ukiandamana na vitendo vya uhalifu wa kupangwa ili mradi tu kuuhalalisha uongo huo! Yote hii ni kujitahidi kuficha ukweli, lakini ukweli siku zote haupotei, unaweza kujificha kwa kipindi kifupi lakini mwishowe ni lazima ujitokeze.

Kuna wanasiasa mchwara ambao wanadhani kutumia magenge ya uhalifu wa kupangwa kwa kuwadhuru waandishi wa habari na wale wote wanaoonekana kuwa wawazi wa kujieleza na kutoa maoni yao juu hali halisi ya kisiasa na kiuchumi hapa nchini, ndiyo watakuwa wamefanikiwa kuuficha udhaifu wao usijulikane mbele ya jamii! Hizi ni fikra dhaifu zisizokuwa na maono ya mbali kwa vile udhaifu au umaarufu wa mtu hudhihirishwa na mtu mwenyewe, na wala haudhihirishwi na mwandishi wa habari, chombo cha habari wala mtu yeyote zaidi ya wewe mwenyewe! Hivyo kuwaandama waandishi au watu wanaoonekana kujua udhaifu wako haina maana kwamba ukimaliza kuwaangamiza ndiyo umeimarisha umaarufu wako, hapana, bali utakuwa umezidi kujidhoofisha!

Tukirudi nyuma kwenye uchaguzi wa mwaka 2005 lile genge la uhalifu wa kupangwa ambalo lina matawi hata huko kwenye nyombo vya habari; lilipomchafua Dr. Salim Ahmed Salim ili aonekane hafai mbele ya jamii kuwania kile kiti cha kula bila kuulizwa unakulaje? Genge hili lilidhani limemdhoofisha Dr. Salim moja kwa moja lakini kiukweli limemuimarisha, na limejikuta ule upande lililokuwa linaushabikia ndiyo umedhoofika tena upo taaban! Hii yote imetokea kwa vile Dr. Salim alijua kwamba umaarufu wa mtu unatengenezwa na mtu mwenyewe, na ndiyo maana hata alipochafuliwa hakutaka kulumbana, bali alikaa kimya akisubiri ukweli ujilete wenyewe ambao wote tunauona!

Watanzania inabidi tuwe makini wa kuweza kutambua wenyewe bila ushawishi watu wenye sifa za kuwa viongozi wa umma bila ya msukumo wowote toka kwenye lile genge ambalo siku zote lipo mustari wa mbele kabisa kutuchagulia viongozi kwa kuwajengea umaarufu wa uongo ili mradi mambo yao yaendelee kuwa mazuri na sisi tukiendelea kuwa masikini zaidi! Sasa hivi genge hili hili lipo katika kampeni chafu za kuwajengea baadhi ya wanasiasa umaarufu wa uongo na baadhi yao hata umri wao bado haujawaruhusu kujipenga makamasi peke yao, ni mpaka wapengwe makamasi na hata nguo bado wanavalishwa, lakini mikakati inafanywa ili hata katiba ibadilishwe watu wao waweze kugombea urais! Watoto wadogo wawe marais wa taifa lipi!? Hao watoto wamefanya miujiza gani mkapa hata tuone kwamba wana umuhimu wa kuliongoza taifa hili!? Au kupiga makelele bungeni ndiyo busara kwa uelewa wa Watanzania!? Au kutumiwa na mitandao kwa kupewa siri za serikali na kuzitoa bungeni ndiyo wameshakuwa mashujaa kiasi ambacho hatuwezi kuishi bila wao kutawala!? Kwani nani hawezi kusimama bungeni na kuzungumza kama ameshapewa kitu au hoja ya kuhoji!? Wabunge hawa wanaotumiwa na genge la kuandaa viongozi kiukweli ni wabunge dhaifu sana kuliko hata wale ambao wamekuwa wakitumia fikra zao binafsi bungeni; Marais watoto wakaongoze nchi zilizoendelea kama vile Amerika na UK ambako democrasia imekuwa na rais ni taasisi siyo mtu binafsi kama hapa kwetu Tanzania.

Watanzania tumeshindwa kuwatambua watu wenye busara kwa mtizamo wetu binafsi! Tunadhani kuandikwa sana kwenye kila gazeti ndiyo ubusara wa mtu, unaweza kuandikwa sana lakini ukawa huna lolote zaidi ya umaarufu wa uongo, na ukawa huandikwi sana lakini ukawa na busara zaidi kuliko wale wanaopamba kurasa za mbele za magazeti ya kila siku! Pia unaweza kutumiwa na genge la media si kwa sababu unaweza hapana, bali unatumiwa ili uwaharibie wale wanaofaa, ili wananchi wasiokuwa wadadisi wazuri wa mambo ya siasa washindwe kutofautisha ni yupi anapengwa makamasi au ni nani anajipenga mwenyewe! Siyo kila mtoto akililia gozi lazima umpe, watoto wengine ukiwapa gozi badala ya kulicheza wao hulilambalamba na kulitemea mate! Mtoto mdogo mpe pipi amumunye! Gozi licheze mwenyewe!

Kulingana na hali halisi ya nchi yetu kwa sasa nchi ambayo ina migogoro mingi ya kidini, ardhi, mauaji na vitendo vya uhalifu wa kupangwa (mafia), ufisadi uliokithiri, ubadirifu wa mali ya umma, kuzorota kwa uchumi na maendeleo ya jamii, kuzorota kwa mfumo wa elimu na afya bora nchini; tunahitaji rais mpevu mwenye busara ya hali ya juu asiyefungamana na upande wowote, mwadilifu, mbunifu na mwenye maono ya mbali ili aweze kuliokoa hili taifa ambalo tukilifanyia mizaha ya kushabikia watu wasiokuwa na sifa tutalielekeza gizani!

Ukitumia nguvu zinazoambatana na vitendo vya uhalifu wa kupangwa kwa madhumuni ya kujijengea au kuwajengea umaarufu wale wasiostahili, utakuwa hujijengi wala huwajengei bali unawabomoa! Kama hatuamini haya tusubirini ukweli wa uhalifu wote wa kupangwa utajitokeza mwishoni, na hapo ndipo tutakapoona kwamba je, wale wataalamu wa kupanga na kushabikia uhalifu huo watakuwa wamejijenga au wamejibomoa!?

Dr. Noordin Jella Email: norjella@yahoo.com Mobile: +255 782 000 131

No comments:

Post a Comment