MFEREJI wa maji uliojengwa kwa
fedha za Serikali kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji katika Kijiji cha
Namahoka Kata ya Ligera Wilayani Namtumbo Mkoani Ruvuma wadaiwa umesombwa na
maji ya mvua iliyonyesha hivi karibuni.
Mwenyekiti wa kikundi cha Songambele
kinachojengewa mradi huo, Gaudens Komba
amesema kuwa mfereji huo umesombwa na maji kutokana na tuta lililowekwa na
Mkandarasi kukinga mfereji huo lilikuwa dogo na baadhi ya sehemu ya
mfereji huo zilititia.
Komba alisema kuwa hiyo ni mara ya pili sasa kwa mfereji huo kutokea
dosari kwani mwaka 2007 mwezi mei Serikali ilitumia shilingi milioni 67
kujenga mfereji huo chini ya kampuni ya Legele civil works iliyokuwa
ikimilikiwa na Dastan Mtembele ambapo kabla ya kukamilika kwake
mfereji huo ulititia na kushindwa kupitisha maji kwenda
mashambani.
Aliongeza kuwa pamoja na hayo
Serikali ilitenga tena fedha kiasi cha milioni 297 kwa ajili ya kufanya
marekebisho ya mfereji huo kwa kuipatia tenda kampuni ya Modspan chini ya
usimamizi wa Ernest Mbawa kufanya kazi ya kuurekebisha mfereji
huo ambapo mpaka sasa kampuni hiyo imelipwa milioni 83 na baadhi ya sehemu
iliyofanyiwa marekebisho imesombwa na maji na zingine kutitia.
Fundi mkuu msaidizi
anayejenga mfereji huo Shafii Magoto alisema kuwa sehemu iliyosombwa
na maji imetokana na mkandarasi kuweka tuta dogo la kukinga mfereji huo
na kuruhusu maji ya mvua kusomba tuta hilo kiurahisi na kuufanya mfereji huo
kuvunjika.
Hata hivyo Magoto
alisema kuwa ujenzi wa mfereji huo umesimama kwa muda wa miezi sita sasa
kutokana na wao kutolipwa fedha yao kutoka kwa mwajiri wao Ernest Mbawa na
wanaishi katika mazingira magumu na wanashindwa kurudi kwao kutokana na kukosa
fedha za kurudia na hivi sasa wanajikita katika kufanya kazi binafsi ili
kujipatia fedha ya kula .
Mkandarasi Mbawa
kwa upande wake anawalalamikia viongozi wa kikundi cha Songambele kwa
kumcheleweshea kumwizinishia kuchukua fedha kwa wakati ili aendelee kujenga
mfereji huo na badala yake viongozi hao hupenda kuendeleza malumbano na
kuingiza migogoro isiyokuwa ya lazima na kutumia muda mwingi kushughulikia
migogoro inayoibuka kila kukicha ndani ya kamati.
Mbawa aliwataka viongozi wa kamati
kumwizinishia fedha ili arekebishe sehemu iliyosombwa na maji ya mvua na
kuwalipa mafundi wake na waendelee na kazi.
Baadhi
ya wanakikundi wakiwemo Mohamedi Mangambila na Mohamedi Akida waliuambia
mtandao huu kuwa wamechoshwa na utendaji kazi wa Mkandarasi huyo walidai kuwa
wataandika barua kwa Mkurugenzi Mtendaji wa
Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo kuomba kusimamisha mkataba wake
kwa hoja ya kushindwa kujenga mradi huo kwa wakati kuendelea kujenga mradi huo
nje ya mkataba na pia mkandarasi kutokuwa na mahusiano mazuri na
kamati.
Mhandisi wa halmashauri
ya wilaya ya Namtumbo Izakiel Nyirenda amethibitisha kuwepo na mgogoro
katika mradi huo na kusema kuwa sababu kubwa inayofanya mradi huo kuyumba ni
viongozi wa kikundi kuiona fedha katika mradi huo ni kubwa na kwa namna fulani
wanataka nao wapate mgao hali inayopelekea kuwepo na migogoro katika mradi huo
kila kukicha na mkandarasi kulazimika kutofanya kazi kwa muda mrefu na kutotaka
kumwizinishia fedha iliaendelee kujenga mradi huo.
Nyirenda alidai kuwa sehemu ilisombwa
na maji inarekebishika kwa haraka na kuruhusu maji kupita kama kawaida licha ya
wanakikundi hao kutomtaka Mkandarasi huyo kwani wanakikundi wenyewe ndio
waliopendekeza jina la Kampuni ya MODSPAN Inayosimamiwa na Ernesti Mbawa kujenga
mradi huona kuziacha kampuni zingine nne zilizoomba kujenga mradi
huo alisema nyirenda.Kampuni ya MODSPAN ilisaini mkataba wa miezi sita toka tarehe30 mwezi novemba mwaka 2011 wa kurekebisha mfereji huo ambapo mpaka mei 2012 mkataba wake uliisha na wanakikundi inaonesha wazi hawakuridhika na utendaji kazi wa mkandarasi huyo na walifia uwamuzi wa kumwandika barua mkurugenziwa halmashauri ya wilaya hiyo ya kutaka kumsimamisha mkandarasi huyo na ndipo mgogoro ulipoanzia na mradi huo ukasimama mpaka hivi sasa. Mradi wa ujenzi wa mfereji huo umesimamisha kilimo cha umwagiliaji katika eneo hilo na kuwaacha wananchi kuziba mito kienyeji na kuendesha kilimo cha umwagiliaji kwa kujichimbia mifereji yao wenyewe na kuendesha shughuliza kilimo cha umwagiliaji.
Hata hivyo mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Namtumbo Steven Nana alipohojiwa na Mtandao huu kuhusiana na mgogoro wa mradi huo wa kilimo cha umwagiliaji alikili kuwa matatizo yapo lakini hawezi kuelezea lolote mpaka awepo ofisini kwake ambako angedai kuwa angeweza kupata ufafanuzi mzuri kutoka kwa maafisa wake wa kilimo na si vinginevyo.
MWISHO
No comments:
Post a Comment