Na, Mwandishi Wetu, Morogoro
MFUMO wa kongano bunifu umetajwa kama mkombozi utakaoleta maendeleo endelevu Tanzania kama utazingatiwa na wadau mbalimbali.
Meneja wa Programu ya Fanikiwa Kibiashara (BDG) ambayo inafanya kazi
chini ya Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Sosthenes Sambua,
alitoa kauli hiyo mjini hapa jana wakati wa mafunzo ya kuwezesha
kongano mbalimbali nchini kujenga ubunifu na ushindani.
Mafunzo hayo ya siku nne yanayoendelea mjini hapa yanaendeshwa na
Scandnavian Institute for Competitiveness and Development (SICD) pamoja
na Pan African Competitiveness Forum (PACF) kwa kushirikiana na BDG,
Programu inayoendeshwa chini ya Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania
(TPSF).
Sambua ambaye alikuwa mmoja wa wakufunzi katika mafunzo hayo,
amewaambia waandishi wa habari kuwa mfumo wa kongano una nafasi kubwa ya
kuleta hali bora ya maisha kwa Watanzania kwa kuwa unashirikisha nguzo
tatu muhimu katika uundwaji wake ambazo ni serikali, wanataaluma au
watafiti na wazalishaji katika jamii husika.
Alisema katika ushirikiano huo kongano huja na ubunifu na njia mpya za
uzalishaji na kujenga ushindani si tu wa ndani bali pia nje ya nchi,
hivyo kuleta maendeleo.
Akitoa mfano wa mataifa mengine alisema nchi kama Sweden, Ujerumani,
Italia, Hispania, na Uholanzi zimekuwa zikitumia mfumo huu wa kongano
kwa zaidi ya miaka 20 na kuwa bado wanaendelea kuwekeza katika mfumo
huo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya washiriki katika mafunzo
hayo walitoa shukrani kwa waandaaji wa mafunzo hayo na kuahidi kufanyia
kazi ujuzi watakaopata kuimarisha kongano zao.
|
No comments:
Post a Comment