Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Ruvuma Oddo Mwisho
Na Stephano Mango, Songea.
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Ruvuma kimelazimika kusitisha uchaguzi wa kura za maoni wa kumpata Mgombea Uenyekiti wa Halmshauri ya Wilaya ya Mbinga baada ya baadhi ya Madiwani kuilalamikia Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Ruvuma ambayo inadaiwa kuwa ilishinikizwa na kigogo mmoja wa CCM kukata jina la mmoja kati ya Madiwani walioomba kugombea nafasi hiyo na kusababisha kuwepo vurugu kubwa za kisiasa ambazo zimesabibisha jengo la CCM la wilaya kunusurika kuchomwa moto na watu wasio fahamika.
Habari zilizopatikana jana mjini hapa kutoka ndani ya Chama Cha Mapinduzi ambazo zimethibitishwa na Katibu wa Chama hicho Mkoa wa Ruvuma Velena Shumbusho zimesema kuwa uchaguzi wa kura za maoni wa kumpata Mgombea Uwenyekiti wa halmashauri hiyo umesitishwa mpaka hapo baadae tarehe itakapopangwa tena.
Shumbusho aliuambia Mtandao huu kwa njia ya simu kuwa uchaguzi huo umehairishwa mpaka CCM mkoa kupitia Kamati yake ya utendaji itakapopanga tena kwani hali ya kisiasa kwa sasa si shwari.
Alifafanua zaidi kuwa pamoja na kusitisha uchaguzi huo jengo la ofisi ya CCM la wilaya hiyo limenusurika kuchomwa moto na watu wasiofahamika jambo ambalo limesababisha wanachama wengi kushtushwa.
Aliwataja Madiwani wa CCM waliojitokeza kugombea nafasi ya hiyo kuwa ni Alanusi Ngahi ambaye ni Diwani wa Kata ya Kipapa, Alani Mahai Diwani wa Kata ya Maguu na Nathaniel Charles Diwani wa Kata ya Matili ambapo kamati ya siasa ya mkoa ilipokaa ilirudisha majina mawili ya Mahai na Charles jambo ambalo limeonekana kuwa na mtafaruku mkubwa baada ya baadhi ya Madiwani kuilalamikia Kamati ya Siasa kwa nini imekata jina la Diwani Alanusi Ngahi na kwamba majina ya nafasi ya Makamu mwenyekiti majina yote matatu ya madiwani walioomba yalirudishwa ambao ni Winfrid Kapinga diwani wa kata ya Ngima, Agnesi Mahangula na Prisca haule ambao wote ni Madiwani wa viti maalumu (CCM) .
Alibainisha kuwa Kamati ya Siasa ya Mkoa chini ya Mwenyekiti wake Oddo Mwisho ilikaa siku nne zilizopita na kupendekeza majina mawili ya wagombea ndio yaliyoletwa kwenye kikao cha Kamati ya Siasa ( CCM) Wilaya ya Mbinga ambayo ililidhia uchaguzi huo ufanyike lakini hakuna kigogo yeyote aliyeshinikiza kukata jina la mgombea bali ni kamati yenyewe ilifikia uwamuzi huo.
Baadhi ya Madiwani wa Halmshauri ya Wilaya ya Mbinga ambao hawakutaka majina yao yatajwe waliuambia Mtandao huu kwa nyakati tofauti walisema kuwa matukio hayo yanasababishwa na viongozi wenyewe wa CCM wa ngazi ya Wilaya na Mkoa kwani inaonyesha wazi kuwa jina la mgombea Ngahi limekatwa kwa shinikizo la kigogo mmoja ambaye ndiye kiongozi mmoja wa CCM vilevile ni kiongozi wa ngazi ya juu wa Halmshauri ya Wilaya mpya ya Nyasa ambayo inatarajia kugawanywa kuwa Halmashauri mbili tofauti
Walisema kuwa tukio hilo linahofiwa kuwa limetokana na Kamati ya Siasa ya Mkoa kutorudisha jina la mgombea jambo ambalo limewafanya baadhi ya Madiwani wagomee uchaguzi lakini swala la kutaka kuchoma jengo la CCM linahitaji Polisi waingie ndani zaidi kufanya upelelezi ili kuwabaini waarifu wenye tabia chafu za kutaka kukichafua Chama Cha Mapinduzi
Kwa upande wake Katibu wa CCM wa Wilaya ya Mbinga Anastasia Amasi alisema kuwa tukio la kutaka kuchoma ofisi yake limetokea Juni 20 mwaka huu majira ya saa za usiku ambapo alidai kuwa yeye akiwa nyumbani kwake juzi majira ya saa za asubuhi alipata taarifa za tukio hilo na alieleza kuwa alipofika kwenye eneo la tukio aliona uharibifu uliofanyika.
Alieleza zaidi kuwa baadaye alitoa taarifa kwenye Kituo Kikuu cha Polisi cha Wilaya ya Mbinga na Askari Polisi walipofika kwenye eneo la tukio walichukua maelezo ya awali kwa ajili ya uchunguzi zaidi na kufafanua kuwa kwenye eneo la tukio yalikutwa masalia ya mafuta yanayodaiwa kuwa ni ya Petrol kwenye chupa yenye ujazo wa lita moja yaliyoletwa na waalifu waliotaka kufanya tukio hilo, lakini mlango mmoja na madirisha mawili pamoja na mapazia ya madirisha hayo yaliungua na moto.
Naye Mkuu wa kikosi cha Jeshi la Zimamoto Mkoa wa Ruvuma Baraka Mvano alipohojiwa na www.stephanomango.blogspot.com kwa njia ya simu alikanusha kuwepo kwa tukio hilo na kudai kuwa ofisi yake haijapata taarifa ya aina yoyote ila anaendelea kufuatilia zaidi.
Hata hivyo Mtandao huu ulijitahidi kufanya mawasiliano ya kumpata Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma Deusdedit Nsimeki ili atoe ufafanuzi juu ya tukio hilo ziligonga mwamba baada ya kumpigia simu zaidi ya mara tatu ambayo ilikuwa haipokelewi na baadaye Mtandao huu ulilazimika kuwasiliana na Afisa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Ruvuma aliyejitambulisha kwa jina moja la Malimi ambaye alithibitisha kutokea kwa tukio hilo ambalo alidai kuwa lilitokea Juni 20 mwaka huu majira ya usiku lakini hakuna mtu yeyote anayeshikiliwa na Polisi inaendelea kufanya upelelezi zaidi ili kuwabaini watuhumiwa.
No comments:
Post a Comment