Na, Stephano Mango, Songea
SIKU za hivi karibuni nimebahatika kufuatilia mambo mawili huko Mkoani Rukwa ambayo leo nakusudia kuwajuza wasomaji wa andiko la Ukanda wa Uranium popote pale mlipo kwani naamini bila kueleza nitakuwa sijawatendekea haki wasomaji na wapenzi wa Viongozi ambao wanafanya vyema kwenye Serikali hii ya awamu ya nne
Mambo hayo ni uandikaji wa kitabu cha Sumbawanga Ng’ara na uanzishaji wa Makumbusho ya Mkoa wa Rukwa iliyopo ndani ya jengo la Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa ambaye kwa sasa ni Mhandisi Stella Martin Manyanya(MB)
Nimebahatika kutembelea Mkoa huo na kuona Makumbusho hayo pamoja na kukisoma kitabu hicho kizuri cha Sumbawanga Ng’ara ambacho kimeandikwa na Mkuu wa Mkoa huo
Licha ya mambo mazuri mengi ambayo yanapaswa kuelezwa kwa wananchi ili waweze kubadili mwenendo wao katika uendeshaji wa jamii zinazotuzunguka , leo mie nakusudia kueleza haya mawili ya kuhifadhi mazingira na kumbukumbu za maeneo yetu
Viongozi wengi nchini wanapenda kufanya vitu vya muda mfupi ambavyo vina maslahi kwao na havionekani kwenye jamii pana wala havishikiki na kusababisha kutokikidhi dhana ya Uongozi kwa maslahi ya Umma
Naamini kuwa sifa za kiongozi bora ni miongoni na kuwa kiongozi wa vitendo na sio madaraka, kuwa na uwezo wa kushawishi watu ili kufanikisha jambo bora kwa manufaa ya watu na kuleta matokeo yanayotarajiwa
Uongozi ni mchakato wa kujua njia, kuonyesha njia, kutembea katika njia hiyo ili kufikia lengo kusudiwa mahali na wakati husika, uongozi ni kipaji na taaluma, ingawa wahenga wanasema kuwa “Kiongozi mzuri ni yule asiyependa kuwa kiongozi , lakini kutokana na uzembe wa viongozi waliopo, anashawishika na kuamua kuwa kiongozi”
Licha ya kuwa uongozi ni utumishi lakini sio ubwana na pia uongozi ni vitendo na sio madaraka, hivyo uongozi unahitaji nia thabiti na moyo wa kujitolea kwa kutumia taaluma na kipaji ulichonacho
Na katika maisha ya binadamu miongoni mwa mambo muhimu ni utamaduni na mazingira ambayo yanamzunguka katika kuimarisha uhai wake, na ndio maana mie leo nakusudia kuzungumzia kitabu cha Sumbawanga Ng’ara na uanzishaji wa Makumbusho katika Mkoa wa Rukwa
Leo nakusudia kumpa ushindi wa kiuongozi Mhandisi Stella Martin Manyanya kuwa ni kiongozi ambaye ameweza kukidhi malengo ya yeye kuwa Mkuu wa Mkoa wa kwanza Mwanamke Mkoani Rukwa na hasa kwa mambo ambaye ameyafanya katika mkoa huo katika Nyanja zote
Ni mengi mno aliyoyafanya lakini kama nilivyosema kuwa kwa leo nayazungumzia hayo mawili na nikipata muda mwingine nitayazungumzia mengine ambayo nayo yanafaida kwa wananchi na mustakabali wan chi yetu
Mhandisi Manyanya amethubutu kuwa ni Mkuu wa Mkoa wa kwanza kuandika kitabu cha mazingira katika eneo lake na pia amekuwa wa kwanza kuanzisha Makumbusho katika Mkoa wake tangu wakuu wa mikoa wapya katika awamu zote mbili za Uongozi wa Rais Jakaya Kikwete walipoteuliwa
Katika hali ya kumpongeza Mkuu huyo Manyanya mzaliwa wa Mkoa wa Ruvuma, Wilaya mpya ya Nyasa katika Kata ya Kihagara nayazungumzia mambo hayo mawili aliyoyaasisi katika Mkoa wa Rukwa toka alipoteuliwa mwaka 2011 ambayo matokeo yake tumeyaona
Kitendo chake cha kuandika kitabu cha Sumbawanga Ng’ara kimefufua na kuanzisha moyo mpya wa uhifadhi mazingira kwa wadau mbalimba , pamoja na kupendesha mji kwani ukienda katika mitaa ya Sumbawanga usiku imekuwa kama mchana. Hii ni kutokana na ushirikishwajiu wa wadau mbalimbali katika uhifadhi wa mazingira kama vile Vodacom, Tigo, na wengine
Katika mambo yalioredheshwa kwenye cha Sumbawanga Ngara kwani uchafuzi uliopo unaoendana na kusambaa kwa taka ngumu umeleta athari kubwa kwa viumbe hai ikiwemo binadamu, wanyama wanyonyeshao na wasionyonyesha, wadudu ambao wengine ni muhimu katika maendeleo chanya ya ardhi,
Kuongezeka kwa mmomonyoko wa ardhi unaosababisha vina vya maji kupungua katika maziwa kama Rukwa na Tanganyika na kukauka kwa baadhi ya mito , Utiririshaji wa maji taka yenye viashiria vya sumu au sumu kamili vinavyotokana na mabaki ya bidhaa za viwandani zimekuwa na athari kwa viumbe hai waishio nchi kavu na majini na kusababisha kupungua kwa wanyama na baadhi ya aina za samaki, na wengine kubadilisha hata ladha yao ya asili.
Kwa ujumla wake uharibifu huo umechangia kwa kiwango kikubwa mabadiliko ya tabia nchi hususan, hali ya hewa katika baadhi ya maeneo, na hivyo kubadili uzuri wa asili na kupoteza baadhi ya vivutio.
Mfano ni kuhama kwa wanyama na ndege katika maeneo yao ya asili, kukauka kwa maporomoko ya maji na kadhalika.Uharibifu unaoendana na taka umesababisha miji ya maeneo ya Mkoa huo kuwa michafu na isiyovutia, milipuko ya magonjwa kama kuhara na kipindupindu, magonjwa ya ngozi kama upele, kudumaa kwaafya, kimsingi watu kuwa na afya hafifu na vifo. Matumizi ya dawa yamekuwa ya kiongezeka, gharama kubwa kwa ajili ya kutoa huduma za afya, kushuka kwa kipato kutokana na kupoteza nguvu kazi, au kuwa na nguvu kazi hafifu na kwa ujumla wake kuongezeka kwa umaskini uliokithiri hasa katika miji
Kitabu hicho ambacho kimezinduliwa na Waziri Mkuu Mizengo Peter Pinda (Mb kinatoa mwongozo wa kufanikisha Mpango wa Sumbawanga Ng’ara kwa faida ya watanzania wote nchini
Ni muhimu kukisoma na kukielewa kwa faida ya vizazi vilivyopo na vijacho kwani malengo yake ni kuona kuwa jamii ina ishi katika mazingira safi na salama , kwani hakuna maisha katika mazingira machafu na yenye viashiria vya hatari katika pumzi ya binadamu, leo ukifika Rukwa unakutana na mabadiliko mengi katika uhifadhi wa mazingira
Jambo jingine ambalo nimekusudia kulisema leo ni juhudi za Manyanya kuanzisha makumbusho katika Mkoa wa Rukwa Kwani Makumbusho ni sehemu ambayo watu wanaweza kujifunza namna ya uhifadhi bora wa mazingira kwa kuangalia watu wa kale walivyoweza kunufaika na mazingira yaliyowazunguka na mali asili zilizokuwepo kwa kupata dawa za miti shamba,chakula na vitoweo
Kupitia Makumbusho wananchi wanaweza kujifunza wajibu wao kwa nchi yao na jamii nzima inayowazunguka kwa kuangalia Mashujaa wa kale waliojitoa kwa moyo kupigana kwa ajili ya uhuru wa nchi,ulinzi na usalama wa mali zao
Uwepo wa Makumbusho ni jambo la kujivunia kwani yanaweza kutumika kujenga amani katika jamii ya watu wanaoishi kama ndugu na marafiki kwa kuangalia maisha ya watu wa kale walivyoishi kwa kushirikiana katika mambo yaliyokuwa yanawahusu wao na jamaa zao
Pia ni sehemu ambayo huwakutanisha watu wa mataifa mbalimbali wanaokuja kuzitembelea na kujifunza historia na tamaduni zetu hivyo kuifanya dunia kuwa mahali padogo kwani vitu wanavyojifunza hupelekwa nchi za mbali na kujulikana kwa watu wa mataifa mbalimbali
Nakufanya kuwa kiungo cha mabadiliko na maendeleo ya Taifa kwani kupitia Makumbusho watu wanaweza kujifunza umuhimu wa mabadiliko na umuhimu wa kila mmoja kujiletea maendeleo kwa kuangalia namna mwanadamu alivyopitia hatua mbalimbali za mabadiliko mpaka kufikia hatua tuliyopo hivi sasa
Kukuza amani na kuchangia kwa ufanisi zaidi katika kujenga amani Dunia, Makumbusho yanaweza kuandaa midahalo, kuonesha filamu, jitihada za utafiti, matembezi, mikutano ya amani na maonyesho ya utalii
Ni sehemu ambayo huvuta watalii,hukuza sayansi,hushangaza/kustaajabisha,kuelimisha,kuburudisha na hutia chachu ya uwajibikaji kwani ndani yake yana kumbukumbu zilizohifadhiwa hivyo makumbusho ni historia inayoishi
Uwepo wa Makumbusho ni wasaa wa kutafakari sisi wenyewe maisha yetu hivyo tunapaswa kuweka juhudi za kutunza makumbusho zilizopo na zinazoendelewa kujengwa
Suala la kutunza Makumbusho ni tete kulibinafsisha kwani linabeba utamaduni na utambulisho wa Taifa au jamii husika, hivyo zinawezwa kutunzwa na mtu binafsi kwa maendeleo yake, taasisi au Taifa lakini kuwepo kwenye taasisi ya umma ni kufanya uhai uendelee kuwepo
Mchango wa Tanzania kwenye tamaduni za nchi za Ulaya ni mdogo mno na hajulikani vyema, japo tumeshuhudia watu wa mataifa mbalimbali wamekuja kujifunza tamaduni, ingawa kila siku tunaendelea kutothamini utamaduni wetu kwa kuendelea kuiga tamaduni za nje bila sababu za msingi
Utamaduni wa jamii za Watanzania unastahili kukuzwa,kutangazwa na kusimamia ili nasi tuweze kuchangia utamaduni wetu kwenye mataifa mengine na ustaarabu wa ulimwengu, hivyo utambulisho binafsi na wa pamoja, kati ya kumbukumbu na historia
Makumbusho ni benki ya kumbukumbu licha ya kuwa ni sehemu ya kuelimishana na kuburudisha, pia makumbusho ni kumbukumbu ya fikra, kazi,maisha,mtazamo wa matukio ya watu mbalimbali, Viongozi na wananchi wengi leo, kuna kila kila sababu ya wananchi kutembelea na kuikuza Makumbusho yao kwa maslahi ya vijazi vilivyopo na vijavyo
Leo wakazi wengi wa Rukwa wanatembelea Makumbusho hayo kwa kasi kwani yamekuwa ya kwanza kuanzishwa katika mkoa huo licha ya kuwa ni Makumbusho ya kipekee katika mikoa yote nchini
Nimalizie makala yangu kwa kusema tunawajibika kuwaiga na kuwaenzi viongozi wenye nia ya dhati ya kusukuma guruduma la maisha ya jamii mbele, wakiwa hai au wakitangulia mbele ya mwenyezi Mungu
Mtazamo wangu na wako ndio unaotengeneza uhai wa Makumbusho na mazingira ya taifa letu, hivyo tuamue kuwa chombo cha mabadiliko kwa kuwaelimisha na kuwahamasisha umuhimu wa utamaduni, mazingira na makumbusho kwani utambulisho una uwezo mkubwa wa kuakisi maendeleo kusudiwa
Kama Mhandisi Stella Manyanya alivyomnukuu Mwandishi wa Marekani Hellen Keller alisema kwamba, “Peke yetu tunafanya machache, pamoja tunafanya mengi.” Tukijitoa sote kufanya kazi kwa bidii, ufahamu na maarifa hata yale yanayoonekana hayawezekani yatawezekana na hata yale yanayoonekana magumu yatakuwa mepesi
Maandishi haya yatuongezee nguvu ya kuanza safari yetu ya kuhakikisha kuwa Sumbawanga ina Ng’ara na Halmashauri nyingine za Rukwa zifuate na maeneo mengine nchini nayo yanapaswa kuiga kwa nguvu kubwa
Hakika siwezi kukuzuia kusoma maandishi yenye tija kwako, kwa maana ya kuwa siwezi kuzuia sikio lako kusikia lakini naweza kuzuia mdomo wako usiseme, nami kwa uhakika naweza kuzuia mkono wangu usiandike zaidi lakini siwezi kukuzuia wewe kusoma uthubutu wa kiuongozi wa Mhandisi Manyanya kwani ameonyesha njia na wengine wanapaswa kujipanga na kuonyesha uongozi tarajiwa kwa faida ya wananchi wanaowaongoza na Taifa kiujumla, na hakika uongozi hauna jinsi
Mwandishi wa Makala haya
Anapatikana, 0715-335051
Barua pepe;stephano12mango@yahoo.com
www.stephanomango.blogspot.com
No comments:
Post a Comment