MKAZI wa Tondoroni, Wilaya ya Kisarawe, mkoani Pwani, Omary
Mohamed (47), amejeruhiwa kwa kupigwa risasi na watu wanaodaiwa kuwa
ni wanajeshi katika mapishano yanayodaiwa kuhusiana na kugombea mpaka.
Tukio hilo lilitokea juzi, majira ya saa 3 asubuhi baada ya wanajeshi
hao kutembelea katika eneo lao na kukuta familia moja ikiwa imejenga
nyumba katika eneo ambalo linadaiwa kuwa ni mali ya jeshi.
Inaelezwa wanajeshi hao walijaribu kuzungumza na familia hiyo kwa
kuwasihi kuondoka, lakini hali hiyo iliibua mzozo mkali kutokana na
wanafamilia kukaidi amri hiyo.
Hata hivyo, baada ya kuona hakuna maelewano, ghafla Mohamed alipigwa risasi moja na watu hao wanaodaiwa kuwa wanajeshi.
Baada ya tukio la kupigwa risasi kwa mwananchi huyo, wanajeshi hao
walitokomea kusikojulikana na ndipo wananchi waliamua kufunga barabara
hadi polisi walipofika na kwenda kutuliza ghasia.
Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Ulrich Matei, amethibitisha kuwepo kwa
tukio hilo na kusema majeruhi huyo amepigwa na kitu chenye ncha kali na
kuwa bado haijajulikana kama waliomjeruhi ni askari ama la na kama
amepigwa na risasi.
Alisema kuwa kwa sasa anafanya mawasiliano na kiongozi wa jeshi ili
kubaini ukweli kama ni askari wa jeshi na wametumwa kwenda kwa wananchi
hao au walikwenda wenyewe.
Kamanda Matei alisistiza kuwa si rahisi kumtambua askari kwa kuwa tu
amevalia sare za polisi lakini pia ni lazima namba za wahusika
zijulikane, kambi gani na uthibitisho kutoka kwa kiongozi wa jeshi kwani
baadhi ya watu huvalia mavazi hayo kwa manufaa binafsi.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Tumbi, Peter Datani, amekiri
kumpokea majeruhi huyo akiwa na jeraha kwenye mguu wake wa kulia, na
hali yake inaendelea vizuri.
|
No comments:
Post a Comment