DK. GAMA MWANADIPLOMASIA, MWANASIASA ATAKAYEKUMBUKWA DAIMA.
Na Stephano Mango, Songea.
Disemba 16 mwaka huu tunatimiza mwaka mmoja tangu Tanzania iondokewe na mwanasiasa mahili kiongozi shupavu na mwana michezo maarufu Dk. Lawrence Mtazama Gama.
Kuna mengi ambayo watu wanaweza kumzungumzia mtanzania mwenzetu huyo ambaye alifariki dunia Disemba 16 mwaka 2009 kutokana na maradhi ya kansa ya mapafu katika hospitali ya Agha khan Jijini Dar es salaam.
Mwili wa marehemu Dk. Gama ulisafirishwa toka Dar es salaam hadi Songea na kupelekwa kijijini kwake Amani makoro Wilayani Mbinga Mkoani Ruvuma ambako alizikwa Disemba 20, 2009 ambapo msiba mazishi hayo yaliudhuriwa na maelfu ya watu akiwemo Rais Jakaya Kikwete na viongozi wa kada tofauti hapa nchini.
Inaaminika kuwa kifo ni njia ambayo mwanadamu yeyote duniani hawezi kukiepuka ndio maana vitabu vitakatifu vya kidini vinakielezea kifo kwa kukifananisha na dhoruba.
Kwamba kinakuja ghafla, muda wowote na hakuna ajuaye siku wa saa ambayo kifo kitamuondoa hapa duniani hii inamaana kuwa binadamu hana mawasiliano na ujio wa kifo.
Kifo cha Dk. Gama kilionekana kuwagusa watu wengi wa kada tofauti kutokana na kazi kubwa aliyoifanya katika kipindi cha uhai wake katika nyanja za michezo, elimu,utamaduni, siasa na uchumi.
Oliver Mhaiki ambaye ni katibu mkuu Wizara ya sheria na katiba anamwelezea Dk. Gama kuwa alikuwa ni mtu mwenye hekima na upendo wa hali ya juu katika maisha yake kwani hakuwa mtu wa kukurupuka katika kujadili jambo.
Kila wakati alikuwa akisikiliza kwa umakini na kujenga hoja anapozungumza jambo la msingi na kudhihirisha uzalendo wake halisi kwa Taifa letu.
Alikuwa akichukia kwa nguvu zake zote vitendo vya ufisadi na watu wanaopewa nafasi za uongozi kujilimbikizia mali badala ya kuwatumikia wananchi
Huyo ndiye Dk. Lawrence Gama kisima cha maarifa, taaluma na ushauri kilichokauka ilhali watu bado wanahitaji kuendelea kuchota hekima na busara zake ambaye tulimpenda lakini mwenyezi Mungu alimpenda zaidi.
Mhaiki anasema, Dk. Gama atakumbukwa kwa mengi aliyoyafanya katika enzi ya uhai wake, katika kuboresha mawasiliano , Dk. Gama alisimamia kikamilifu ujenzi wa barabara ya lami kutoka makambako hadi Songea katika miaka ya 1980s.
Usafiri wa Songea hadi Dar es salaam ulikuwa ni zaidi ya siku mbili na sasa hutumia masaa 12, ambapo jitihada hizo pia zimesaidia kuongeza wawekezaji wa ndani na nje katika Mkoa na hivyo kuongeza ustawi wa wananchi wa Mkoa wa Ruvuma.
Dk. Gama akiwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma atakumbukwa katika uhamasishaji wa viongozi na wananchi katika kujiletea maendeleo.
Alikuwa kiongozi na muandaaji wa mpango mkakati wa maendeleo ya Mkoa kupitia agizo la mlale mwaka 1977 lililoainisha fursa na vikwazo, changamoto na mikakati ya kupambana na umasikini ulioukabili Mkoa wa Ruvuma .
Mhaiki anasema, mkazo mkubwa wa agizo hilo uliwekwa katika kuboresha kilimo ambapo kwa sasa ni kilimo kwanza na matokeo ya jitihada hizo Mkoa uliweza kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara.
Toka wakati huo Mkoa wa Ruvuma ulipoingizwa kwenye orodha ya Mikoa minne(4) ya awali iliyoongoza katika uzalishaji wa mazao ya chakula yakiwemo mahindi nay a biashara ( The big four) inaendelea kushikilia hadi saa.
Dk. Gama alitambua kuwa ustawi wa familia (kaya) huanzia katika kuwepo na makazi bora, hivyo alihamasisha wananchi kujenga nyumba bora kwa kutumia matofali ya kuchoma na hadi sasa ni wastani wa asilimia 70 ya wananchi wanaishi katika nyumba bora.
Marehemu Dk. Gama alikuwa kiongozi shupavu na mkereketwa wa maendeleo na atakumbukwa kwa mengi na watanzania na wananchi wa Ruvuma kwa ujumla kwani alifanikiwa kuacha alama ambazo hazifutiki kamwe.
Mhaiki anasema, Dk. Gama alikuwa akifanya kazi kwa vitendo na si kwa maneno tu au mwenye kudandia mafanikio ya wengine na kuyatumia kujiimarisha kiuongozi au kisiasa kama viongozi na wanasiasa wengi wa leo wanavyofanya.
Bali Dk. Gama enzi za uhai wake amefanya mambo mengi na kuuweka Mkoa wa Ruvuma kwenye mafanikio makubwa katika sekta ya kilimo,michezo,utamaduni,elimu,afya na uchumi.
Kwani enzi za uhai wake akiwa kiongozi wa kwa nyadhifa tofauti na kutambua umuhimu wa afya ya binadamu alifanikiwa kushawishi upatikanaji wa fedha na kuhamasisha ujenzi wa hospitali ya Mkoa wa Ruvuma , kituo cha afya cha mji Mwema, na Zahanati zingine nyingi.
Enzi za uhai wake Dk Gama alishiriki kikamilifu katika ujenzi wa barabara za lami ndani ya mji wa Songea , Soko kuu la Songea ambalo hapo awali liliungua moto na kusimamia ujenzi wa soko jipya na la kisasa, masoko madogomadogo ya Bombambili, Manzese, Lizaboni ,Mfaranyaki na Majengo .
Marehemu Dk. Gama licha ya kuwa msomi mwenye kiwango cha shahada ya uzamili (Ph. D) alikuwa tegemeo kubwa kwa wanajamii wa Mkoa wa Ruvuma na Taifa kwa ujumla kwani hilo linajidhihirisha kutokana na mchango mkubwa alioutoa katika medani za elimu, uongozi na ushauri wa kitaaluma kwenye fani mbalimbali,
Kwani alifanikiwa kuhamasisha ujenzi wa shule nyingi za msingi na sekondari kwa kuzitaja chache ni shule ya msingi Misufini, Kitanda, Lugongolo, Bombambili, Majengo, Samora, na nyingine nyingi ambapo shule za sekondari ni Msamala, Ruvuma,Makita,Londoni,Karembo,Mletele,na nyingine nyingi.
Pia alifanikiwa kujenga ofisi mbalimbali za serikali na taasisi zake ambazo mpaka leo zimekuwa ni alama tosha kwa kizazi kilichopo na kijacho katika kumuenzi marehemu Dk. Gama kwa mchango wake aliouonyesha enzi ya uhai wake.
Mhandisi Stella Manyanya ambaye ni Mbunge wa viti maalum Mkoa wa Ruvuma pia ni Mwenyekiti wa ushauri wa kamati ya Makumbusho ya Taifa ya Majimaji anamuelezea Dk. Gama kama kiongozi aliyeonyesha njia kwa kufanya mambo mengi ambayo yanapaswa kuenzishwa na kuendelezwa kikamilifu.
Manyanya anasema, Dk. Gama alizaliwa na kulelewa na familia ya kichifu kwa maana wazazi wake walikuwa machifu walioheshimika sana na kabila la wangoni ambapo naye Dk. Gama alisimikwa kuwa chifu na baadaye alimkabidhi uchifu Exaveli Zullu kuwa chifu wa wangoni mpaka sasa.
Licha ya kuzaliwa , kulelewa na kusimikwa uchifu , Manyanya anasema Dk. Gama atakumbukwa na kuenziwa kwa mchango wake wa kuthamini mila,desturi na tamaduni za kabila la wangoni.
Anasema Dk. Gama enzi za uhai wake aliwaenzi kikamilifu Mashujaa waliouawa wakati wa vita vya Majimaji kwani alifanikiwa kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa Makumbusho na kuhamasisha ujenzi huo uliokamilika mwaka 1980.
Pamoja na kukamilisha ujenzi wa jengo hilo la Makumbusho aliweza kuzijenga sanamu 12 za machidu wa kingoni, sanamu ya askari wa jeshi la wananchi wa Tanzania na sanamu ya Mwl. J.K. Nyerere.
Pia Dk. Gama kwa kushirikiana na Padri Chengula wa kanisa katoliki la Songea ambaye kwa sasa ni marehemu na baadhi ya wazee walifanikiwa kukusanya vifaa vilivyotumika kupigania wakati wa vita vya majimaji kutoka kwenye maeneo ya Maposeni, Matimila na Namanditi ambako kuna historia kubwa ya kabila la wangoni.
Manyanya anasema, vifaa vilivyo kusanywa ni Chikopa (ngao), Chibonga (rungu), Chinjenje (kishoka) jiwe lililotumika kusagia nafaka, nguo za magome ya miti na viti vilivyotumiwa na Chifu Mputa Gama ambapo vifaa hivyo vimehifadhiwa ndani ya jengo la Makumbusho ya Taifa ya Majimaji Songea na kuwa kivutio kikubwa kwa utalii wa kiutambaduni na kihistoria .
Katika sekta ya michezo , wadau wa michezo wanaendelea kumkumbuka Dk. Gama kwa ujenzi wa viwanja vya michezo vyenye ubora mkubwa nchini kama vile uwanja wa Majimaji , uwanja wa Zimanimoto uliopo Songea Mjini, uwanja wa Ally Hassani Mwinyi uliopo Tabora.
Dk. Gama ataendelea kukumbukwa kwa mipango yake ya kisanyansi aliyotumia kuanzisha timu mbalimbali na kuinua vipaji vya wachezaji vijana na kutengeneza timu zilizoleta ushindani mkubwa wakati huo ikiwemo timu ya Milambo ya Tabora chini ya wachezaji wake mahiri wakati huo Feruzi Telu , Jumanne Mikidadi, pamoja na wengine.
Timu ya Majimaji iliokuwa tishio wakati huo nchini na nchi jilani chini ya wachezaji wake mahiri Actavian Mrope, Peter Tino, Mchunga Bakari, Hussein Mwakakuruzo, Samli Ayub , Celistin Skinde Mbunda na wengineo .
Licha ya kushiriki katika kuleta maendeleo ya waruvuma na nchi kwa ujumla marehemu Dk. Gama atakumbukwa kwa michango yake aliyotoa aliposhika nyadhifa mbalimbali nchini .
Dk. Lawrence Mtazama Gama alizaliwa Januari 19 mwaka 1935 katika kijiji cha Amani Makolo Wilayani Mbinga Mkoa wa Ruvuma na kubahatika kupata elimu katika vipindi tofauti, mwaka 1944 – 1947 alipata elimu ya msingi katika shule za likwambi - Maposeni na Magagula Wilaya ya Songea ambapo alihitimu masomo ya darasa la nne na mwaka 1948 – 1952 alipata masomo katika shule ya kati ( middle school) ya Peramiho.
Mwaka 1953 – 1954 alipata elimu ya sekondari katika shule ya Ndanda iliyopo Wilayani Masasi Mkoani Mtwara na mwaka 1969 alijiunga na chuo kikuu cha Dar es salaam ambapo alisomea sheria.
Mwaka 1983 – 1985 alijiunga na chuo ckikuu cha Karlmarx nchini Ujerumani na kupata shahada ya siasa na uchumi na mwaka 1985 – 1987 alipata shahada ya kwanza ya uzamili na mwaka 1987 – 1989 alipata shahada ya uzamili (Ph. D) katika fani ya siasa na uchumi katika chuo hicho hicho.
Dk. Gama alipata mafunzo mbalimbali kwa nyakati tofauti katika nchi za Marekani, Ireland, Uingereza, Israel,na nchi nyingine na kufanikiwa kutunukiwa vyeti mbalimbali na nishani za uongozi uliotukuka.
Dk. Gama amewahi kushika nyadhifa mbalimbali ndani ya chama cha mapinduzi (CCM) 1994 – 1996 alikuwa katibu mkuu wa CCM ambapo mwaka 1995 – 2000 alikuwa mjumbe wa NEC na mwaka 1996 – 2005 alikuwa Mbunge wa Songea Mjini.
Pia Dk. Gama amewahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini ambapo mwaka 1960 – 1962 alikuwa Mratibu msaidizi wa Polisi, mwaka 1963 – 1965 alikuwa msaidizi wa Mkurugenzi wa JKT akitokea Jeshi la Polisi mbali ya wadhifa huo pia aliwahi kuwa Mkuu wa vikosi vya JKT Mgulani, Ruvu pamoja na kufanya kazi Makao makuu ya JKT
Mwaka 1970 – 1973 alikuwa mkuu wa jeshi la kujenga Taifa hapa nchini ambapo mwaka 1973 – 1976 alikuwa mkurugenzi wa idara ya usalam wa Taifa na mwaka 1976 – 1977 alikuwa mkuu wa mkoa wa Dodoma na mbunge wa kuteuliwa.
Mwaka 1977 – 1989 alikuwa mkuu wa Mkoa wa Ruvuma na Mbunge wa kuteuliwa na mwaka 1989 – 1994 alikuwa mkuu wa Mkoa wa Tabora na Mbunge wa kuteuliwa na mwaka 1996 aliteuliwa kuwa mkuu wa Mkoa wa Morogoro.
Marehemu Dk. Gama aliacha Mjane, watoto 16, wajukuu 22 na vitukuu 2 na kwa mambo hayo aliyoyafanya na mengine mengi ataendelea kukumbukwa kwa kila namna na kazi zake zitaendelea kuwa alama isiyofutika kwa watanzania wakiwemo wananchi wa mkoa wa Ruvuma.
Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi, pumzika Dk. Gama rekodi yako ya utumishi kwa Taifa itakukumbukwa na kuenziwa daima ,kwani Bwana alitoa na bwana ametwaa jina lake lihimidiwe na pengo lake halitazibika .
Mwandishi wa makala hii
Anapatikana kwa simu 0755 – 335051
Barua pepe: Stephano12mango@yahoo.com.
No comments:
Post a Comment