UTALII WA WANAFUNZI RUVUMA NI CHACHU YA WADAU KUTEMBELEA HIFADHI NCHINI
Na Stephano Mango,Songea
UTALII ni sekta inayokua na kutoa ajira takribani milioni 200 na inachangia dola za kimarekani trilioni 3.6 katika uchumi wa dunia.
Ambapo kati ya mwaka 2000 hadi 2006 idadi ya watalii wa kimataifa iliongezeka kutoka milioni 681 hadi 862.
Mapato yatokanayo na watalii wa kimataifa yaliongezeka kutoka dola za kimarekani 496 hadi dola bilioni 623 katika kipindi cha miaka hiyo.
Takwimu hizo ni za kimataifa hivyo kwa mujibu wa mchanganuo huo, Tanzania iko katika nafasi ya tano kwa mapato ya utalii katika nchi za Afrika kutokana na idadi ya watalii kuongezeka.
Sekta hiyo inachangia asilimia 17.2 ya pato la taifa (GDP) na inachangia karibu asilimia 25 ya jumla ya thamani ya mauzo yote ya nje.
Hata hivyo sekta hiyo ililiingizia taifa fedha za kigeni kwa wastani wa dola za marekani dola bilioni moja, mchango ambao ni mara tatu ya mchango wa sekta ya kilimo katika pato la taifa.
Kutokana na takwimu hizo sekta ya utalii imekuwa ya kwanza katika sekta zote zinazoliingizia taifa fedha za kigeni zinazotokana na mauzo ya bidhaa za nje.
Ingawa matarajio ya Serikali ni kuwa ikiwa wastani wa ongezeko la idadi ya watalii itakuwa kwa kati ya asilimia 10 na 20 basi Tanzania itapata watalii milioni moja ifikapo mwishoni mwa mwaka 2010.
Hata hivyo, kutokana na umuhimu wa sekta hiyo katika kukuza uchumi wa nchi kwa kuongeza wawekezaji, ajira na kupunguza umaskini kuna baadhi ya mikoa inaendelea kuhamasisha na kuvitangaza vivutio vya utalii katika maeneo husika kwa upana wake.
Miongoni mwa Mikoa yenye mikakati kabambe ya kuhakikisha vivutio vyake vyote vilivyopo katika Mkoa husika vinatangazwa ni Mkoa wa Ruvuma uliopo kusini mwa Tanzania.
Vivutio vilivyomo mkoani Ruvuma ni pamoja na poli la akiba la liparamba lenye kila aina ya wanyama na ndege, Ziwa Nyasa, Gereza la miti lililojengwa na wajerumani wakati wa vita dhidi ya Majimaji
Majengo ya Makumbusho ya mashujaa wa vita vya majimaji yenye zaidi ya miaka 100 ambayo ndani yake kuna sanamu za picha za mashujaa hao, zana zilizotumika kupigania vita hivyo, kaburi kubwa walilozikwa mashujaa 68.
Pango alilotumia kujificha nduna Songea Mbano, sehemu waliyonyongwa mashujaa wa vita hivyo, kaburi la mjerumani wa kwanza kunyongwa na wangoni Peramiho, jiwe la ajabu mbuji na vivutio vingine vingi,
Miongoni mwa hifadhi zenye upekee Nchini ni Ruhila Nature Reserve ambayo ina vivutio lukuki ambavyo vinaendelea kutangazwa kikamilifu ili vifahamike kwa watu wengi na kuongeza idadi ya utalii kusini mwa Tanzania na Taifa kiujumla.
Mkuu wa kikosi cha kuzuia ujangiri kanda ya kusini Metson Mwakanyamale anaelezea kwa ufasaha maana ya Ruhila Nature Reserve, mikakati iliyopo ya kuitangaza na changamoto zinazoikabili hifadhi hiyo.
Mwakanyamale alianza kwa kusema Ruhila ni jina la Mto ambao unapita katikati ya hifadhi hiyo, na ndio maana jina la mto huo limepewa heshima kubwa ya kubeba Nature Reserve iliyopo eneo hilo.
Mkuu huyo anafafanua kuwa Nature Reserve ni kipande cha ardhi chenye uoto wa asili ambacho kimetengwa kwa mujibu wa sheria stahiki lengo likiwa ni kuhifadhi uoto asilia ambao aupaswi kuharibiwa na shughuli za binadamu
Ruhila ni miongoni mwa hifadhi pekee nchini ambayo ni adimu kupatikana katika maeneo ya mjini lakini Mkoa wa Ruvuma umebahatika kuwa na eneo hilo zuri lenye vivutio vingi ambavyo watalii wa ndani na wa nje wanaweza kuja kuangalia pasipo kutumia fedha nyingi kwa ajili ya usafiri pindi wanapofanya utalii,kwani hifadhi hiyo ipo umbali wa kilometa 8 tu kaskazini Magharibi mwa mji wa Songea na ina ukubwa wa maili 311.
Akielezea historia ya hifadhi ya asili ya Ruhila Mkuu wa kikosi cha kuzuia ujangiri kanda ya kusini ambaye ndiye mkuu wa hifadhi hiyo Metson Mwakanyamale.
Alisema hifadhi hiyo ilianzishwa mwaka 1973 na mwaka 1974 ilizungushiwa uzio wa kilometa 8 ili kuzuia wanyama wasiende kwenye makazi ya watu wanaoishi kuzunguka eneo hilo na kuongeza kuwa hifadhi hiyo imezungukwa na vijiji 3 vilivyopo katika Manispaa ya Songea ambavyo ni Mkuzo, Mshangano na Chandarua.
Akizungumzia wanyama walioletwa wakati hifadhi hiyo inaanzishwa mwaka 1974 kutoka Arusha ni pamoja na Pofu 9, Ngorombwe 3, Nyumbu 9, Kuro 1 ambao hivi sasa hawapo na Pundamilia 10 ambao wamebaki 6.
Shughuli ya kuwaleta wanyama hao kutoka Arusha ilifanywa na mhifadhi Hashim Sariko mwaka 1975 ambaye kwa sasa ni Meneja mkuu wa pori la akiba la wanyama Liparamba wilayani Mbinga.
Mwakanyamale anasema kumbukumbu za mwaka 1981zinaonyesha kuwa wanyama walioletwa katika hifadhi ya Ruhila waliongezeka, ambapo Pofu waliongezeka kutoka 9 hadi 15.
Pundamilia waliongezeka kutoka 10 hadi 26, Nyumbu waliongezeka kutoka 9 hadi 13, Ngorombwe waliongezeka kutoka 3 hadi 5 na chatu ambao idadi yao haikuweza kupatikana ambao wameendelea kuongezeka kila mwaka,aliongeza kuwa watu wengi wa ndani na nje walipata fursa ya kujionea vivutio mbalimbali vilivyomo ndani ya hifadhi hiyo wakati huo.
Hata hivyo katika miaka ya 1986 na 1989 kasi ya matumizi ya hifadhi hiyo ilipungua sana ikilinganishwa na miaka ya nyuma, hii ilitokana na usimamizi usiozingatia utaalamu na kufanya baadhi ya vivutio kutoweka na kuharibika kwa miundombinu muhimu katika hifadhi hiyo.
Mwakanyamale alisema ili kuimarisha utalii wa ndani na wa nje katika hifadhi hiyo kulingana na Sera ya Taifa ya wizara ya Maliasili na utalii alianza kutengeneza uzio( fensi ya Senyenge) na mageti ili kuzuia wanyama wasitoke kutoka kwenye hifadhi kwenda kwenye makazi ya watu ili ulinzi wa vivutio vilivyomo visiharibiwe.
Ameeleza kuwa tayari ametengeneza (keji) bebeo la chui au simba mtoto ili atakapopatikana wasipate shida ya kumbeba ,mkuu huyo alisema pia licha ya wanyama ambao wanategemewa kuongeza uzuri wa hifadhi, kuna vivutio vingine ndani ya hifadhi hiyo.
Miongoni mwa vivutio hivyo ni miamba ambayo chatu huishi, maporomoko ambayo kobe huishi, chanzo cha mto Ruhila ambacho kimebeba jina la hifadhi na vivutio vingine vingi.
Hifadhi ina maeneo ya ufugaji nyuki pia ina vivutio vya wanyama wa aina ya Pundamilia, pongo, sungura, kobe, kakakuona,nyani na ngedere wa kila aina.
Vivutio vingine ni mandhari ya hifadhi hiyo ambayo ni ya kuvutia sana, mabwawa ya samaki, “ndege aina ya kanga, kware, bata, mwali na nyange, alisema Mwakanyamale”.
Ili kuimarisha utalii wa ndani Mwakanyamale anasema alifanya mawasiliano na Afisa Elimu wa Mkoa wa Ruvuma na wakuu wa shule za Mkoa wa Ruvuma ili waende katika hifadhi hiyo kwa ajili ya utalii wa mafunzo.
Tayari ofa hiyo iliyotolewa kwa Shule za msingi, Sekondari na Vyuo iliyoanza Disemba 2008 na kumalizika mwanzoni mwa mwaka 2010 imefanikiwa kwa asilimia 85 ambapo shule zaidi 86 zilifanikiwa kutembelea hifadhi hiyo ambapo shule 10 za kwanza kutembelea hifadhi hiyo zilipata mipira miwili kila moja.
Kwa mujibu wa mkuu huyo orodha ya ada ya kiingilio katika hifadhi hiyo kuanzia julai mosi 2009 ni kama ifuatavyo,ambapo ada ya mtu mwenye umri wa miaka 18 raia wa Tanzania kwa siku ni sh. 5,000 na raia wa kigeni atalipa dola za kimarekani 50.
Watoto wa miaka 5 hadi 17 raia wa Tanzania watalipa Shilingi 3000 ambapo raia wa kigeni watalipa dola za kimarekani 30 na watoto walio chini ya miaka mitano raia wa Tanzania na nje wataingia bure katika hifadhi hiyo.
Mwakanyamale anafafanua zaidi kuwa huduma ya kuongoza wageni kiofisi kwa gari raia wa Tanzania ni sh 30,000 na kuongoza kwa miguu kwa siku itakuwa ni sh 25,000 ,pia alisema kuongoza raia wa kigeni kwa gari kiofisi watalipa dola za kimarekani 30 na kuwaongoza kwa miguu kwa siku watalipa dola za kimarekani 25.
Alisema ada za kuchukua picha za kawaida na za video kwa siku kulingana na mpangilio maalum kutoka kwa mkuu wa hifadhi ya Ruhila siku moja hadi siku 89 ni kati ya dola za kimarekani 50 hadi 200.
Siku 90 hadi 179 ni kati ya dola za kimarekani 40 hadi 150 na siku 180 hadi 720 ni kati ya dola za kimarekani 30 hadi 100 ambapo ada ya kusajiliwa kwa muongozaji ni sh 50,000 kwa raia wa Tanzania na raia wa kigeni dola za kimarekani 2000.
Jitihada hizo tayari zimezaa matunda ambapo watalii 946 wametembelea hifadhi ya Ruhila kuanzia julai 2008 hadi septemba 2009. Pia alisema kuna shule 50 za msingi, sekondari 36, viongozi mbalimbali wa mkoa zaidi ya 80 na walimu walitembelea hifadhi hiyo.
Pamoja na uzuri wa hifadhi hiyo Bw Mwakanyamale alisema kumekuwa na ujangiri unaotokana na watu kukata miti kwa ajili ya kuezekea nyumba zao, kuni, kuchimba mizizi kwa ajili ya dawa za kienyeji, kukata nyasi na kuchoma moto ovyo.
Alizitaja changamoto zingine zinazoikabili hifadhi hiyo ni pamoja na uhaba na uchakavu wa nyumba za watumishi wa hifadhi hiyo, kwani kumbukumbu zinaonyesha tangu mwaka 1974 zilipojengwa hazijawahi kufanyiwa ukarabati. Pia nyumba zaidi ya 6 zinatakiwa kujengwa ili kukidhi mahitaji ya idara ya wanyama pori kanda ya kusini.
Changamoto nyingine ni barabara ya kwenda katika hifadhi hiyo yenye urefu wa kilometa 3.5 inahitaji kutengenezwa kwa kupandisha tuta na kuweka changarawe ili iweze kupitika wakati wote kwa uwakika.
Kwa upande wake mwanafunzik wa Shule ya sekondari ya Chandamali kidato cha pili Anuciata Mapunda mara baada ya kutembelea hifadhi hiyo na kujionea mandhari ya Ruhila Nature Reserve.
Alisema Ruhila ni eneo zuri ambalo linavutia sana na linaweza kuliingizia Taifa mapato makubwa endapo likiendelezwa kwa sababu eneo hili ni pekee nchini ambalo liko kilometa sifuri kutoka makazi ya watu hivyo watalii hawawezi kutumia gharama kubwa kufika eneo hilo.
Aliongeza kuwa ziara za masomo kwa wanafunzi huongeza chachu ya uelewa kwani kwa mwanafunzi ambaye mara nyingi amekuwa akisoma umuhimu wa utalii kupitia vitabu anakuwa na uelewa mdogo kwani hajawahi kufanya aina yoyote ya utalii hususani kwenye maziwa,mbuga za wanyama na hifadhi mbalimbali,lakini pindi atakapotembelea anakuwa na uelewa mkubwa na pale anapokuja kusoma kwenye vitabu au kusimuliwa/kuelezewa anakuwa na ufahamu mkubwa na hivyo kufanya uwezo wake kuwa mkubwa katika jambo hilo
Hata hivyo, Bw Mwakanyamale alisema ana mikakati mingi ya kuboresha hifadhi hiyo na ameiomba Serikali kumwezesha kikamilifu raslimali fedha ili aweze kukamilisha ujenzi wa miundombinu katika hifadhi hiyo na kuwataka wananchi kutembelea hifadhi zao ili waweze kujifunza tabia za viumbe, aina za viumbe hao na kujionea maliasili zilizopo katika maeneo yao na nchini kwa ujumla ili waweze kuvitunza na kuvitangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini kwa faida ya vizazi vilivyopo na vijavyo
Mwandishi wa Makala hii
Anapatikana kwa simu 0755-335051
Baruapepe;stephano12mango@yahoo.com
No comments:
Post a Comment