About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Monday, January 17, 2011

MHANDISI MANYANYA ALIYE DHAMIRIA KUBADILI MAISHA YA WANAWAKE RUVUMA


MHANDISI MANYANYA ALIYE DHAMIRIA KUBADILI MAISHA YA WANAWAKE RUVUMA
 
 Na,Stephano Mango,Songea.
 
HUWEZI kuzungumzia Wanawake jasiri hapa nchini bila kumtaja Mhandisi Stella Martin Manyanya ambaye ni Mbunge mbunge mtarajiwa wa Viti maalum Mkoa wa Ruvuma kupitia Chama cha Mapinduzi.
 
Ukibahatika kukutana na kuzungumza naye utabaini kuwa hana majivuno, anajiheshimu na anaheshimu wenzake pia bila kujali wadhifa wa mtu husika.  Mhandisi Manyanya anapendwa na wengi kutokana na tabia yake ya kuwa karibu na Wananchi katika hamasa mbalimbali za Kimaendeleo na harakati za utalii, ujasiliamali, elimu na michezo.
 
 Ujasiri wa Mhandisi Manyanya ulionekana pale alipoamua kujiuzulu kazi yake ndani ya shirika la Umeme Tanzania(Tanesco) Mwaka 2007/2008 wakati alipokuwa kwenye Kamati ya Bunge ya Uchunguzi wa Mkataba tata wa kampuni ya kufua umeme ya Rich Mond ili kuepusha mgongano wa kimaslahi baina ya kazi yake ndani ya Shirika hilo na ile ya bunge ambayo ilikuwa ikichunguza utata wa Rich mond.
 
Manyanya alikuwa Mwanamke pekee aliyekuwa kwenye kamati ya Bunge iliyochunguza Kampuni hiyo iliyoleta kitimtim Nchini hadi Baraza la Mawaziri likavunjika baada ya aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowasa kujiuzulu.  Mbali ya mhandisi Manyanya ambaye alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, wajumbe wengine walikuwa ni Dk. Harrison Mwakyembe (Mwenyekiti) Lukas Selelii, Mohamed Mnyaa na Herbert Mtangi.
 
Hii ikiwa ni mara yake ya kwanza kuingia bungeni lakini anaufahamu mkubwa ukilinganisha na baadhi ya Wabunge hasa wale wa rika lake na kwa wale wanaomfahamu wanasema mafanikio yake yametokana na kujiamini na kupenda kusimamia kile anachokiamini.
 
Nilibahatika kukutana na kufanya mahojiano naye hivi karibuni katika ofisi yake ya Better Life Tanzania iliyopo Mahenge, Songea Mjini Mkoani Ruvuma baada ya kuchukua muda mrefu toka tulipo panga ahadi ya kukutana kwa mahojiano, hii ilikuwa ni kutokana na muda mwingi kuwa katika huduma mbalimbali za kijamii kwenye Kata, Wilaya na Mkoa katika kushughulikia utekelezaji wake wa ilani kwa Wananchi na Chama chake.
 
Katika mahojiano yake na Gazeti hili alizungumzia historia yake, ambapo alisema alizaliwa agosti 4 mwaka 1962, Mwambao mwa Ziwa Nyasa katika Kijiji cha Kihagara, Wilaya mpya ya Nyasa, Mkoani Ruvuma.  Anasema yeye ni mtoto wa tano kati ya watoto Kumi na moja (11) waliozaliwa katika familia ya Mzee Martin Manyanya, amasema ameolewa na amebahatika kupata watoto watatu ambapo anaeleza kuwa Familia yake ndio faraja kubwa inayomwezesha kufanya kila kitu.
 
Mhandisi Manyanya hadi sasa ni mlezi wa Chama Cha Waandishi wa habari Mkoa wa Ruvuma (RPC), Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), Mjumbe wa Kamati ya utekelezaji wa Jumuiya ya Wazazi Tanzania, Mjumbe wa bodi ya Makumbusho Mkoa wa Ruvuma na Mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri ya Makumbusho ya Taifa na hivi karibuni alitetea nafasi yake ya ubunge wa Viti maalum mkoa wa Ruvuma ambapo alipigiwa kura 300 kati ya wajumbe 380 na kupelekea kuwa mshindi wa kwanza
 
Kitaalama Manyanya ni fundi mchundo (Technicianian) ambaye alikuwahi akifanya kazi katika Shirika la Madini la Taifa (Stamico) kuanzia Mwaka 1983 hadi 1986, ambapo baada ya hapo alijiunga na Chuo cha Ufundi cha Dar es salaam (DIT) na baada ya kupata Diploma aliajiriwa na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuanzia Mwaka 1992 hadi 1995 na alipata nafasi ya kujiunga na masomo zaidi Nchini Norway.
 
Manyanya anasema baada ya kurejea kutoka Norway aliendelea na kazi katika Shirika la Umeme Nchini ambako alifanya kazi hadi Novemba 2007 ndipo alipojiuzulu kufanya kazi ndani ya Shirika hilo mwaka huo,akiwa Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Ruvuma baada ya kuchaguliwa kuwa mmoja wa wajumbe wa kamati ya Bunge iliyochunguza Kampuni ya Richmond ili kuepuka mgongano wa kimaslahi baina ya Bunge na Tanesco.
 
Akizungumzia shughuli zake za uwakilishi kwa miaka mitano akiwa Mbunge wa viti maalum Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Manyanya anasema kuwa alijikita zaidi katika elimu, afya,uchumi na uimarishaji wa Chama Cha Mapinduzi kupitia Jumuiya ya Wazazi na Wanawake (UWT) na kuendeleza sekta mbalimbali za Kijamii.
 
Anasema kwa upande wa elimu, amesimamia zaidi elimu kwa Wasichana ambao kwa asilimia kubwa wamekuwa nyuma kimaendeleo kutokana na wazazi wengi kutowathamini watoto wa kike ambao wengi wao wameishia kupata ujauzito mashuleni na wengine kuozeshwa.
 
Kutokana na hali hiyo amehamasisha na kuchangia mabati, saruji na fedha shilingi milioni 59 za ujenzi wa mabweni katika Shule nyingi za Sekondari zilizopo Mkoani Ruvuma ambapo baadhi ya shule hizo zimeanza ujenzi ilikupunguza tatizo la mimba kwa Wasichana na kujiingiza katika ndoa za utotoni.
 
Anasema sambamba na kuchangia ujenzi huo amekwisha toa elimu kwa wazazi na wananchi kupitia mikutano ya hadhara juu ya umuhimu wa elimu kwa Wasichana katika Wilaya ya Tunduru, Namtumbo, Songea vijijini na Mbinga na wilaya mpya ya Ziwa Nyasa. 
 
Anasema pia ametoa vifaa vya michezo kwa Shule za Msingi, Sekondari na vijiwe vya vijana katika Wilaya zote za Mkoa wa Ruvuma vyenye thamani ya Milioni 23 ili kuweza kupunguza muda wa vijana kuzurura na kushawishika kufanya vitu viovu, kama vile uasherati, matumizi ya pombe haramu na uvutaji wa madawa ya kulevya. 
 
Anasema dhamira yake tangu alipokuwa anaingia bungeni mwaka 2005 ilikuwa ni kuona viongozi na watendaji wa CCM wanafanya kazi katika Mazingira mazuri ambapo anasema amekarabati na kuweka samani za kisasa katika Ofisi za Jumuiya  zote za Chama katika Wilaya ya Songea,Mbinga,Songea vijijini ambapo pia ametoa sh. Million 1 kwa ajiri ya jumuiya ya UWT Wilaya ya Namtumbo ili waweze kununua kiwanja kwa ajiri ya ujenzi wa jengo la kitega uchumi cha Jumuiya hiyo.
 
Kuruthum Mhagama Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Ruvuma anasema Mhandisi Manyanya ameonyesha uongozi stahiki licha ya kuwanyanyua Wanawake wengi Kiuchumi kupitia Asasi isiyo ya kiserikali ya Better Life Tanzania kwani  ameweza kuvisaidia vikundi mbalimbali vya kijamii raslimali fedha na elimu ya Ujasiriamali.
 
Viongozi wengi wanatabia ya kusahau walikotoka ambapo wakikumbushwa wanaleta jeuli lakini Manyanya amekumbuka alikotoka na amedhamiria kwa dhati kubadili maisha ya Wanawake wa Mkoa wa Ruvuma na ndio maana katika uchaguzi wa Jumuiya ya UWT uliofanyika hivi karibuni Manyanya aliibuka na ushindi wa kishindo kwa kupigiwa kura na wajumbe 300 kati ya wajumbe 380 anasema Mhagama.
 
Manyanya ameshirikiana na wanawake wa Mkoa wa Ruvuma kufungua Asasi ya kiraia ya Better Life Tanzania inayowafundisha wajasiriamali wadogo na wakati mbinu mbalimbali za kuweza kujikwamua kiuchumi,ufugaji wa kuku wa kienyeji na wa kisasa, utengenezaji wa batiki, kilimo cha uyoga na kubadilishana mawazo kwa nia ya kujengana.
 
Manyanya ambaye pia ni Mkurugenzi wa Asasi hiyo anasema azma ya asasi hiyo nikuelimisha wananchi ili waweze kuchukua matatizo waliyokuwa nayo kama changamoto na kutafuta njia za kukabiliana nazo ambazo zitaweza kupunguza au kumaliza matatizo hayo na wakati huohuo kutengeneza ajira. Anasema kuwa asasi hiyo imekuwa ikiangalia fursa za Kiuchumi na namna ya kutumia fursa hizo katika kujikwamua na umasikini ambapo toka 2006 hadi sasa Wananchi zaidi ya 3000 wamefaidika na asasi hiyo kupitia sekta za Elimu na Kiuchumi.
 
Anasema wajasiriamali wengi hawafahamu namna ya kuandika miradi (Proposal) hasa pale Benki zinapowataka kufanya hivyo ili waweze kupata mikopo stahiki ambapo kwa utaratibu uliowekwa na kituo cha Better Life Tanzania kilichopo Mahenge Mjini Songea chini ya Mratibu wa Kituo hicho Genfrida Haule Wanawake 60 na vijana 43 wamefaidika na elimu ya uandikaji wa Miradi ya ujasiriamali.
 
Ili kuhakikisha kazi ya ujasiriamali anaifanya vyema Manyanya anasema aliamua kujiunga na kituo cha Ujasiriamali cha Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDEC) ambako alichukua digrii ya pili  (masters degree) ya masuala ya ujasiriamali. Anasema elimu hiyo aliyoipata anaitumia vyema kuwaelimisha Wananchi hasa Wanawake wa Vijijini wasiojua kuandika miradi ili na wao waweze kunyanyuka na kuweza kupata mikopo  katika Benki ambapo anasema elimu hiyo ameanza kuitoa katika Wilaya zote za Mkoa wa Ruvuma .
 
Akizungumzia kilimo cha zao la uyoga anasema kilimo hicho cha kisasa cha zao hilo na urahisi wa Kilimo hicho umewavutia watu wengi kukilima ambapo anasema toka 2006 hadi sasa kituo cha Better Life Tanzania kinahudumia wakulima 8000 katika Mkoa wa Ruvuma na wakulima 260 kutoka Mikoa ya Rukwa, Pwani, Iringa na Lindi.
 
Anasema kilo moja ya uyoga wenye ubora stahiki inauzwa kati ya shilingi. 6000 hadi 8000 kulingana na soko husika pamoja na ubora wa zao ambapo anasema zao hilo limeboresha familia nyingi na hasa wanawake wa Mkoa wa Ruvuma .
 
Anasema anaishukuru Kampuni ya Bia Tanzania TBL na mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa msaada wa fedha walizozitoa kwa ajili ya ujenzi wa Maabara ya kisasa ya kuzalisha mbeguza uyoga katika Kata ya Mshangano (Mkuzo)Mjini hapa kwani maabara hiyo ikikamilika itaweza kuleta mapinduzi makubwa ya kilimo cha zao hilo .
 
Mhandisi Manyanya alitumia mahojiano haya kuomba ridhaa ya wananchi ili aweze kuwawakilisha kwenye Ubunge wa viti maalum Mkoa wa Ruvuma kupitia Chama Cha Mapinduzi kwa awamu ya pili pia amechukua nafasi hiyo kuwaomba radhi wananchi wa Mbinga ambao walimtaka agombee jimbo moja kati ya majimbo mawili yaliyopo Wilaya ya Mbinga katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Octoba 31 mwaka huu.
 
“Nawaomba radhi wananchi wa Mbinga waliokuwa na kiu ya kunitaka niachane na viti maalum nikagomee jimbo nimelitazama na kulifikiria ombi lao kwa umakini mzito na ninaheshimu nia yao lakini naomba kuwaambia kuwa sijawatosa kwani mwaka 2015 nitafanya hivyo ila kwa sasa nitaongeza juhudi katika kutetea vilio vyao kwa Wabunge watakao chaguliwa nikiwa Mbunge wa Viti maalum”, alisema Manyanya.
 
Anasema kikubwa kinachomfanya asigomee jimbo kwenye uchaguzi wa Mwaka huu ni maombi yenye uzito mkubwa ya Wanawake ambao ameshaanza nao kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, hivyo anataka aendelee kuwa nao kwa maendeleo zaidi kupitia umoja wa wanawake wa Tanzania (UWT)
 
Alisema awamu ya kwanza ilikuwa ni ya kujifunza na hivyo amejifunza mengi ambayo anatakiwa kuyatekeleza akiwa kamili kulingana na ndoto zake za kuongeza chachu na kasi ya maendeleo akiwa Mbunge wa viti maalum kwani huko ndiko ana fursa kubwa ya kutetea Mkoa mzima kuliko angekuwa Mbunge wa jimbo.
 
Naomba waniombee kupata kura ili nirudi Bungeni kwani nimejifunza na nipo tayari kuwatumikia na kwa sasa nitaendelea kuwatumikia katika viti maalum na nitatekeleza wajibu na kutimiza maombi yao nikiwa katika nafasi hiyo, alisema Manyanya.
 
Mwandishi wa Makala
Anapatikana  simu 0755-335051

No comments:

Post a Comment