MOTO WATEKETEZA NYUMBA YA MBUNGE KAPTENI KOMBA
Na Stephano Mango,Songea
MOTO umetekeza nyumba ya mbunge wa jimbo la Mbinga Magharibi mkoani Ruvuma Kapteni John Komba na kusababisha mtu mmoja ambaye ni mfanyakazi wa benki ya wananchi Mbinga(MCD) Emmanuel Kumbulu(38) kujeruhiwa vibaya wakati akijaribu kujiokoa.
Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Lituhi akiwemo kaimu Afisa mtendaji wa kata ya Lituhi Joseph Chawala amewaambia waandishi wa habari jana kwa njia ya simu kuwa taarifa ya tukio hilo ilimfikia majira ya saa 11 alfajiri leo na alipofika nyumbani kwa kapteni komba alikuta nyumba ikiendelea kutektea kwa moto.
Chawala alisema kuwa jitihada za kuzima moto huo hazikuweza kufanikiwa kwa sababu ya vifaa duni vilivyokuwa vikitumika kuzima moto na kukosekana kwa huduma ya kikosi cha zimamoto kumechangia nyumba hiyo kuteketea.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu tukio hilo kamanda wa polisi wa mkoa wa Ruvuma Michael Kamuhanda amethibitisha kuungua kwa nyumba hiyo iliyoko katika kijiji cha Lituhi wilayani Mbinga ambayo ni mali ya mbunge Kapteni John Komba.
Kamanda Kamuhanda amesema kuwa chanzo cha moto huo ni betri za umeme jua(sola) zilizokuwa zikitumika kutoa nishati ya umeme kwenye nyumba na nyingine zikiwa zimehifadhiwa kwenye moja ya vyumba cha nyumba hiyo ambazo zilipata hitilafu na kusababisha moto ulioteketeza nyumba yote na mali zilizokuwemo.
Akizungumzia kuhusu thamani ya nyumba na mali zilizoteketea kwa moto Kamuhanda amesema thamani bado haijajulikana bali kinachojulikana ni kuwa nyumba imetekea na kila kitu kilichokuwemo ndani na thamani yake itajulikana baada ya mawasiliano na mmiliki wa nyumba hiyo kapteni komba.
Naye mkuu wa wilaya ya Mbinga kanali mstaafu Edmund Mjengwa akizungumza na waandishi wa habaro kwa njia ya simu kuhusu tukio hilo amesema kuwa yuko safarini mkoani Mbeya na taarifa ya ajali hiyo ameipata baada ya kupigiwa simu na uongozi wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga.
Amesema kuwa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya itakutana kujadili tukio hilo ili kuweza kupata taarifa sahihi na chanzo cha ajali hiyo ya moto iliyoteketreza nyumba na mali zote za mbunge huyo.
Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Mbinga Magharibi Kapteni John Komba alipoulizwa kwa njia ya simu alithibitisha kuteketea kwa nyumba yake na mali zilizokuwemo na kusema kuwa taarifa ya tukio hilo imemkuta akiwa Mbamba bay alikokuwa amekwenda kwenye ziara ya kuwasuhukuru wapiga kura wake kwa kumchagua.
No comments:
Post a Comment