MADEREVA TAKSI SONGEA WAMCHARUKIA MKURUGENZI
Na Stephano Mango,Songea
MADEREVA taksi wanaoegesha gari zao kwenye eneo la soko kuu katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea Mkoa wa Ruvuma wameiomba Serikali ione umuhimu wa kusikiliza kilio chao baada ya Uongozi wa Halmashauri ya Manispaa hiyo kushindwa kuwasikiliza wala kuwajibu kuhusiana na pingamizi walilotoa la kufukuzwa kwenye eneo la Soko kuu kwa madai kuwa eneo hilo ni jirani na Benki ya Nmb tawi la Songea.
Wakizungumza na mtandao wa www.stephanomango.blogspot.com hapa jana Wawakilishi wa madereva hao Peter Vicent,Pashens Mkinga,Christopher Komba na Hussein Mhagama wameeleza kuwa kitendo cha Halmashauri ya Manispaa ya Songea cha kuwakataza kuegesha magari yao kwenye eneo la Soko kuu ni cha unyanyasaji kwani wao ni madereva wa magari madogo(taksi) ambayo yamekuwa yakiegeshwa kwenye eneo hilo kwa ajili ya kusubiri wateja wanaotoka Sokoni na wengine kwenye Taasisi za fedha ambazo zipo jirani na eneo hilo.
Walisema kuwa pamoja gari hizo kuegeshwa kwenye eneo hilo zimekuwa zikilipiwa stika shilingi 35,000 kila baada ya miezi sita kwa kila gari moja fedha ambazo zimekuwa zikipokelewa na Halmashauri hiyo.
Walieleza zaidi kuwa pia wamekuwa wakilipa ushuru wa kuegesha taksi hizo kwenye eneo hilo shilingi 250 kwa kila gari kila siku na Manispaa hiyo na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Ruvuma imekuwa ikiwatoza shilingi laki 291,000 kwa kila gari dogo (taksi) kwa mwaka.
Walifafanua zaidi kuwa wao ni wadau wakubwa kwa kuchangia maendeleo ya Manispaa hiyo pamoja na Serikali kuu lakini wanashangaa kuona kuwa uongozi wa Halmashauri hiyo umechukua uamuzi mkubwa wa kuwafukuza kwenye eneo la Soko kuu kwa kuwatumia askari wa kikosi cha usalama barabarani bila kuwapa taarifa ya maandishi ya kuwahamisha kwenye eneo hilo .
Waliongeza kusema kuwa baada ya kuona wamefukuzwa kwenye eneo hilo walimwandikia barua Mkurugenzi wa Halmashauri ya Songea ya kupinga kufukuzwa kwenye eneo la Soko kuu tangu Julai 20 mwaka huu lakini mpaka leo hawajapewa jibu la aina yeyote na juzi mchana walikwenda kufuatilia barua yao ya pingamizi kwa Mkurugenzi ambaye aliwajibu kuwa barua yao ya pingamizi alishaipata na anaamini kuwa tayari walishajibiwa jambo ambalo lilianza kuonyesha kuwa lina utata kwa vile wao walikuwa bado wanasubiri majibu toka Manispaa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Nachoa Zakaria alipohojiwa na mtandao huu jana kwa njia ya simu kuhusiana na madereva taksi hao kufukuzwa kwenye eneo walilokuwa wakiegesha magari yao na kuto kuwajibu barua ya pingamizi waliyomuandikia alieleza kuwa ana kiri kuwa ofisi yake ilipokea barua ya pingamizi ambayo walikuwa wameiandika madereva taksi ambao wanaegesha kwenye Soko kuu na kwamba zipo sababu za kiusalama zilizofanya waondolewe kwenye eneo hilo .
Zakaria alieleza zaidi kuwa eneo hilo la Soko kuu lipo karibu na benki ya NMB hivyo kwa kuweka usalama kamati ya ulinzi na usalama iliamua gari hizo ndogo (taksi) zinazoegeshwa kwenye eneo hilo ziondolewe na badala yake zipangiwe eneo jingine ambalo alilitaja kuwa eneo la wazi kwenye barabara inayotoka TTCL kwenda Hospital ya Serikali ya Songea ambapo wao wameamua kupinga maamuzi hayo kwa madai kuwa eneo hilo halina miundo mbinu mizuri ya vyoo na maji
Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo alisema kuwa Halmashauri yake inafanya utaratibu wa kuweka miundo mbinu wanayodai madereva hao hivyo wanapaswa kukubali kuhamia kwenye eneo hilo na kwamba barua yao waliyoandika ya kupinga pingamizi ofisi yake ilisha wajibu kwamba ni lazima wahamie kwenye eneo lililopangwa na si vingenevyo.
MWISHO
No comments:
Post a Comment