About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Sunday, August 28, 2011

MWEKEZAJI ADAIWA KUPORA ARDHI YA EKARI 5000 KWA WANAKIJIJI LIPOKERA

            Wananchi wa kijiji cha Lipokera wakiwaonyesha waandishi wa Habari ardhi yao ambayo wanadai wameporwa na mwekezaji
 Wananchi wakionyesha mahindi yao baada ya kuvuna haraka haraka kwa kumuogopa mwekezaji asije akawanyang'anya
Na Thomas Lipuka,Songea.
WAKAZI wa kijiji cha Lipokela wilayani Songea mkoani Ruvuma wanamuomba Waziri wa ardhi,nyumba na Maendeleo ya Makazi  Profesa Anna Tibaijuka kuwasaidia kuirejea ardhi yao yenye ukubwa wa zaidi ya hekari 5000  iliyochukuliwa kinyemela na mwekezaji.
Wakizungumza na waandishi wa habari katika kijiji hicho baadhi ya wananchi walidai kuwa  mwekezaji mwenye asili ya Asia anayefahamika kwa jina moja la Merali  tangu mwaka 1985 alipewa ardhi kinyemela bila baraka za wananchi na kusababisha ardhi hiyo kuingia kwenye mgogoro mkubwa.
Wananchi  wamedai kuwa mwekezaji huyo alipewa  ardhi hiyo katika mazingira ya kifisadi kupitia aliyekuwa mwenyekiti wa kijiji hicho  Joseph Komba pamoja na aliyekuwa katibu wake Gervas Mbonde .
Hata hivyo walisema mwekezaji huyo alipewa ardhi  kwa maamuzi ya wananchi yenye ukubwa wa hekari 1000 mwaka 1984 na kwamba mwaka 1985 aliomba tena ardhi hekari zaidi ya 5000 ambazo alipewa bila baraka za wananchi na kuleta mgogoro ambao unaendelea hadi sasa.
``Kuanzia mwaka 1985 wananchi wa kijiji cha Lipokela hawakujua kama ardhi yao ya hekari 5000 amepewa mwekezaji hadi mwaka jana  takriban miaka 25 ndipo ilipofahamika na kusababisha wananchi zaidi ya 250 wanaolima mashamba pamoja na makazi kwenye  eneo hilo  kuambiwa kuwa eneo hilo ni mali ya mwekezaji wa kiasia’’,walidai wananchi hao.
Akizungumza kwa niaba ya wenzao Mwenyekiti mstaafu wa kijiji hicho Faustine Komba alibainisha  kuwa ardhi hiyo yenye  mgogoro ilianza kutumika na wananchi kuanzia mwaka 1993 ambao walipimiwa kihalali na uongozi wa kijiji na kuendelea kuitumia mwaka hadi mwaka bila kutambua kuwa amepewa mwekezaji kinyemela.
Komba alisema mwekezaji alipewa kisheria hekari 1000 tu upande wa kulia mwa barabara ya Songea - Mbinga na kwamba eneo lenye hekari zaidi ya 5000 upande wa kushoto ambazo mwekezaji huyo anadai kupewa kinyemera sio zake kwa kuwa ni mali ya wananchi ambazo walipewa kihalali na serikali ya kijiji.
Uchunguzi ambao umefanywa na wanakijiji wanadai wamebaini kuwa mwekezaji huyo kwa kushirikiana na baadhi ya viongozi wa kijiji hivi sasa amekuwa dalali wa kuwauzia ardhi wawekezaji wengine kutoka nchini Afrika kusini na Marekani hivyo wameiomba serikali na hasa waziri wa ardhi kuingilia kati mgogoro huyo.
Wananchi hao wakiwemo  Gofrey Lupindu,Agustino Komba,Filbert Kinunda, Vestina Hyera, Bomba Nchimbi wakizungumza kwa uchungu mkubwa ,walidai kuwa hivi sasa pia hawana imani na mwenyekiti wa kijiji aliyopo madarakani John Nchimbi ambaye anadaiwa kumsaidia mwekezaji badala ya kuwasaidia wananchi waliomweka madarakani.
Uchunguzi umebaini kuwa iwapo serikali haitachukua hatua za makusudi katika kutatua mgogoro huo wa ardhi kuna hatari ya kutokea machafuko makubwa kutokana na ukweli kuwa  wananchi wa kijiji hicho  wamedai hawapo tayari kuona mwekezaji anapora ardhi yao  kinyemela na kusababisha wananchi kuwa wakimbizi katika ardhi yao.
Uchunguzi mwingine ambao umefanywa katika kijiji hicho umebaini kuwa  mwekezaji huyo ambaye alipewa hekari 1000 na wananchi  katika kipindi  cha miaka mitatu alifanikiwa kulima hekari 15 tu na kitendo cha kutaka kuchukua hekari nyingine zaidi ya 4000 kinawapa mashaka kuwa kijiji hicho kipo katika hatari ya kuuzwa kwa kisingizio cha uwekezaji.
Afisa ardhi wa Halmashauri ya wilaya ya Songea Japhet Mungashwa amekiri kwamba  mwekezaji huyo amemilikishwa eneo la hekari 5000 kihalali kwa kipindi cha miaka 99 kwa sheria ya ardhi ya mwaka 1923 ambayo inawaruhusu wajumbe wa kijiji kupitisha maamuzi bila kushirikisha maamuzi ya wananchi wote kama ilivyo katika sheria mpya ya ardhi ya mwaka 1999.
 Wananchi hao wametoa mwito kwa serikali ya wilaya ya Songea,mkoa wa Ruvuma pamoja na Waziri  wa ardhi,nyumba na maendeleo ya makazi kufika katika kijiji hicho  ili kujionea hali halisi ya ardhi ya mashamba na makazi ambayo wameporwa  na mwekezaji.
Sheria ya ardhi ya vijiji  namba tano kifungu cha tano ya mwaka 1999 inasema kuwa Halmashauri ya kijiji haitagawa ardhi au kutoa hakimiliki ya kimila bila ya kwanza kupata idhini ya mkutano  wa kijiji ambapo katika kifungu cha sita katika sheria hiyo kinaeleza  Halmashauri ya kijiji italazimika kutoa taarifa na kuzingatia maoni ya mkutano wa kijiji kuhusu uendeshaji na usimamizi wa ardhi ya kijiji.
Kwa mawasiliano andika lipukakomba@yahoo.com




No comments:

Post a Comment